Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hii Wizara. Kwanza tu nimpongeze dada yetu, ndugu yetu Mheshimiwa Prof. Ndalichako, anafanya kazi kubwa sana kwa kweli. Hii ni pongezi bila unafiki, anafanya kazi kubwa sana. Wizara hii toka ameishika tumekuwa na mabadiliko makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo shule zilikuwa zinaitwa za vipaji au shule maalum; ukienda pale Mara kuna Alliance, kuna Tabora, kuna Msalato, kuna Nganza na maeneo mengi. Amefanya kazi kubwa ku-renovate zile shule zimekuwa nzuri sana. Shule zile zinavyojengwa, hata kama imejengwa Bukoba, Tabora na kadhalika, watoto wetu wote wa Kitanzania wanaenda kusoma pale. Kwa hiyo, amefanya kazi nzuri sana, mama tunatakiwa kukupongeza kwa kazi nzuri, kuwapongeza na watumishi wako wote waliofanya kazi hiyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza jambo la corruption of mind; na katika hili namshukuru sana Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wetu. Alikataa jambo la corruption of mind. Hivi kweli asingekuwa yeye, hili suala la corona huku kwetu leo ingekuwaje? Tungevaa mabarakoa mpaka yakavunja kila kitu. Kwa hiyo, akakataa corruption of mind kwa maana ya kwamba siyo kila kitu unachokiona ukifanye wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza Wabunge wengi hapa leo, hivi kuna haja gani watoto wanaokaa kwenye ardhi ya udongo mwekundu ukaambiwa wavae uniform nyeupe kila siku? Kuna haja gani? Kuna vitu vingine Mheshimiwa Prof. Ndalichako unatakiwa uvitazame, kwamba jamani hivi kweli hili tunaenda nalo mpaka lini? Nasema hiyo ni corruption of mind. Juzi tu kuna mtoto ameniuliza swali, ni mwanangu mdogo tu, kwamba hivi baba, Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanzania ni nani? Nami nimekaririshwa huko primary nikasema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Akanicheka, nikasema huyu mtoto amekuwaje? Akaniambia hapana baba, Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, kwa sababu Tanganyika iliishia 1962 na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanzania alianza 1964. Ni nani sasa? Rashid Kawawa, si nikakaa kimya. Corruption of mind! Yaani tunakaa, tunakariri vitu, hatuna uwezo wa kubadilisha kwamba hili liendeje na lifanye kazi gani? Mama nakushukuru umefanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kuhusu kile kituo changu cha VETA. Chuo cha VETA mama nimekutembelea sana na nimekuja kwako sana. Kuna shule inaitwa Mgeta Primary ina Chuo cha Ufundi, inafundisha ufundi pale, imesajiliwa kwenye ufundi, inafanya mitihani miwili; ya kawaida na ufundi. Mama naomba ukumbuke kwenye hicho Chuo cha VETA, kipindi hiki kwa kweli, utakuja nayo tu, kwa sababu uliniahidi kwamba mwaka huu utaondoka nayo, nami nakubali kwamba ukija uje vizuri kwenye hiyo VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nane katika Jimbo langu la Bunda; kuna Shule ya Hunyali, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Chamuriho, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Salama, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Milingo, haina walimu wa sayansi; Shule ya Mtomalilo haina walimu wa sayansi, Shule ya Nyamanguta, haina walimu wa sayansi; Shule ya Makongoro, haina Walimu Sayansi; na Makongoro High School, haina Walimu wa Sayansi. Kama katika shule wanahitajika Walimu 24 wako watano au sita. Naomba tafadhali kwenye huo mgao wa Walimu uweze kupata nafasi ya kunisaidia kwenye jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, mimi huwa nasema na huwa tunaimba hivi bila Mwalimu mambo yangekuwaje? Hivi inakuwaje yule Mwalimu ametutumikia miaka 24 na yeye hakujenga chuo wala hakujenga barabara, leo mkienda kujenga chuo nyumbani kwake, chuo kinakaa pale kama maganda fulani, hivi hivi anajisikiaje pale kwenye kaburi lake, hivi kama hakukuwa na haja ya kwenda kujenga pale kwa nini waende kujenga? Wametoa Walimu, wametoa kila kitu na kila jambo liko pale, lakini chuo hakipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mwalimu pale kwenye kaburi lake anajisikiaje? Kama Wizara haijawa na mpango maalum jamani wa kwenda Butiama, isiende, ili yule mzee akae vizuri kule, hivi anaonaje wameenda kumjengea chuo wanaliita jina lake na chuo hakipo miaka 14; majengo tumewapa bure, kila kitu tumewapa bure, hivi inakuwje? Hii nayo inaleta tatizo sana kwenye jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nilitaka tu nimkumbushe mama VETA ni muhimu sana. (Makofi)