Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Mimi dakika zangu sijui kumi, saba, tano nitaongea kitu kimoja tu, nitaongea kitu kimoja ambacho ni kikubwa sana fedha za miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuanzia Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne, ya Tano hadi hii awamu ya sita, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inajitahidi sana kupeleka fedha za miradi ya maji kwenye Mikoa kwenye Wilaya kwenye kata hadi kwenye vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee kitu ambacho naomba Serikali inisikilize vizuri Waziri unisikilize vizuri, miaka ya 1970, 1971,1972 na 1973 nilikuwa msichana mdogo ambaye nilikuwa Sekondari nina akili timamu kuanzia mwaka 1970 hii ilikuwa ni Awamu ya Kwanza, nakumbuka wakati pale kijijini kwetu,ninatokea Same Kata ya Kihurio Kijiji cha Uzambara miaka hiyo ya 1970 hadi 1974 nakumbuka Serikali ilileta mradi wa maji kwenye Kata yangu ya Kihurio, Kijiji cha Uzambara. Mradi ule Mheshimiwa Waziri ulikaa kwa muda mrefu sana kwanini? Serikali ya Chama cha Mapinduzi inapeleka fedha za mradi nyingi sana kwenye Mikoa, Wilaya na Kata lakini wakishapeleka ile miradi wanaachia uangalizi wa ile miradi wananchi ndio waangalie ile miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakumbuka ni vema nifanye comparison mwaka 1970, 1971, 1972 hadi 1980 mradi ulioletwa kwenye Kata yangu ya Kihurio, mradi ulikuwa unaangaliwa na kijana mmoja akiitwa Ally Mabomba, kijana huyo ameajiriwa na Serikali ndiye kila saa 12 asubuhi mnaona maji yanatoka amekwenda kufungua maji kwenye chanzo huko, huko kwenye tenki maji yanapotokea saa 12 jioni Ally Mabomba anakwenda kuyafunga yale maji siku nzima Ally Mabomba anazunguka na Baiskeli kuangalia mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameajiriwa na Serikali anazunguka siku nzima na baiskeli yake Kijiji kwa Kijiji kitongoji kwa kitongoji anaangalia mradi wake wa maji mahali kuna kasoro anarekebisha yeye. Sasa tuangalie sasa hivi miradi yetu inakwendaje? Serikali inapeleka fedha nyingi sana za miradi nyingi sana, miradi ile inawekwa vizuri inajengewa matenki, wanafanya kila kitu miradi ile ikishaisha kunaundwa kamati ya maji sijui huko kwenye Kata zetu na vijiji vyetu wale ndio wanaoangalia ile miradi kule kwenye Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni Mbunge hiki ni kipindi cha tano na tangu nimekuwa Mbunge kumekuwa na miradi kuanzia bendera, mradi wa kihurio, Mradi wa Ndungu, mradi wa Mahore, mradi wa Kalemau miradi hii inaletwa na Serikali mtakaa miezi sita, saba mradi umeharibika wanaanza kupelekana mahakamani fedha zimeliwa wanaanza kusumbuana huyu ndiye amekula, ile Kamati inayoangalia ule mradi sio, ni kamati wananchi wameichagua wenyewe na ninaona kama Mbunge lakini hakuna mtu mwenye taaluma hata kidogo ya miradi. Sasa nimeomba nizungumzie hili na Waziri unisikilize vizuri tuleteeni fedha za miradi ya maji huko kwenye Majimbo yetu. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ile mkishaiweka vizuri fanyeni kila mahali penye mradi kuwe na mtaalam anayeangalia mradi ule. Ama sivyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi mtaendelea kutumia pesa nyingi sana kupeleka miradi ile lakini kwa sababu uangalizi wa ile miradi siyo, inakuwa hamjali tena, mkisha-install mradi wa 20 milioni, kama sasa hivi kuna mradi mkubwa unakuja huko umetokea Same, Mwanga, Korogwe umechukua mabilioni ya pesa mradi ule utakapoingia kwa wananchi naziona pesa ni nyingi sana, mimi kwa sababu nimekaa muda mrefu kwenye Majimbo miradi mingi inakufa sana kwa sababu Serikali hawarudi kuangalia ile miradi. Tunafanya sherehe, mradi tumeanza, tunachinja kuku na ng’ombe baada ya hapo hatuwaoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta tunatengeneza Kamati ya Maji sijui wanakusanya hela wanaiba huko huko, wanagombana huko huko hata koki wanashindwa kutengeneza. Mheshimiwa Waziri mtakuwa mnatuletea pesa ambazo hazitoi matokeo mazuri. Sisi tunawashukuru sana mnapotuletea pesa na mnapoanzisha hii miradi kwenye kata zetu ahsanteni sana lakini rudini muiangalie ile miradi, kila mradi uwekeeni mtu kama yule kaka aliyekuwa anaitwa Ally Mabomba, nimekaa naye kuanzia 70 mpaka 78. Marehemu mama yangu alivuta maji kutoka pale ambapo jumuiya yote tunachota maji akaweka uani yale maji nimeyachota kwa miaka nane sasa hivi hakuna kitu kama hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilisimama hapa kuiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ahsanteni sana mnatuletea miradi mingi sana lakini mkishaiweka ile miradi wekeni wataalamu wa kuiangalia. Nilikuwa na moja tu la kuzungumza, nashukuru kama Serikali imenisikiliza lakini naomba hili tuliangalie na Waheshimiwa Wabunge huko mliko kwenye Majimbo yenu mhakikishe Serikali ikiweka miradi inaleta wataalam kuangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)