Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sisi sote kuwa hai na kukutana kwenye Bunge hili leo. Maji ni uhai. Sisi watu wa Mtwara nafikiri katika mikoa ambayo inaongoza kutokuwa na maji ya uhakika ni pamoja na Mkoa wa Mtwara. Leo ninataka niongelee mambo muhimu matatu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, naishauri Serikali, sehemu ambapo maji yanaanzia au yanakotoka kama ni kisima, kama ni mto, kama ni bwawa muanze kuwapa huduma wale halafu yaendelee sehemu nyingine. Kumekuwa na changamoto kubwa sana, unakuta chanzo cha maji kipo pale, wameweka mabomba lakini maji yanakwenda kupatikana sehemu nyingine na wale watu ambao wanaishi pale kwenye kile chanzo cha maji hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, kuna Kata moja inaitwa Naliendele. Kuna mradi mmoja wa maji unaanzia Mtaa wa Mbawala chini, huko mbawala chini wenyewe wanaona mantenki, wanaona mabomba lakini hawapati maji. Ile inakatisha tamaa. Mradi ule pia nimeona umeuzungumzwa kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kwa sababu unasuasua, tunaomba ukarekebishwe ufanya kazi vizuri kama alivyoandika kwenye hotuba yake ili kusudi wananchi wale wapate maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine huduma ya maji ni huduma lakini kwa wakati mwingine ni biashara. Kumekuwa na masuala ya kusuasua sana, wananchi wanalalamika sana, mtu anakwenda Idara ya Maji, wanamfanyia tathmini analipia, lakini kuja kuunganisha maji inachukua muda mrefu. Vifaa hakuna, mita hakuna, mabomba hakuna.

Mheshimiwa Spika, unapotaka kufanya biashara wakati unatoa huduma ni lazima ujidhatiti. Kwa hiyo, suala hili nalo pia katika Manispaa ya Mtwara Mikindani lipo, watu wanalipa lakini wanachelewa kuunganishiwa maji kwa sababu ya ukosefu wa vifaa. Tunaomba wenye mamlaka walifanyie kazi kwasababu tumeongea sana. Ukiona nakuja kuongea huku Bungeni, nimeanza kuongea kwenye Baraza la Madiwani. Tunaomba lifanyiwe kazi ili mtu akilipa fedha yake anataka huduma ya maji, basi apatiwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine la mwisho kubwa ninaloliongelea ni mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma kuleta katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mradi huo ukipita katika baadhi ya Vijiji vya Jimbo la Mtwara Vijijini.

Mheshimiwa Spika, kama unakumbuka nilikuwepo kwenye Bunge lililopita. Huu mradi kuandikwa kwenye hotuba za Waziri umeandikwa sana, lakini haujawahi kutekelezwa kwa hatua yoyote. Hata leo Mheshimiwa ameuandika, nimeuona na nimeusoma. Ameandika kwamba huu mradi umetengewa shilingi bilioni sita; shilingi bilioni moja kutoka Serikali yetu ya Tanzania na shilingi bilioni tano kutoka Benki ya Afrika. Ombi langu kubwa tunaomba sasa isiwe historia.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kubwa, tunaomba sasa isiwe maneno matupu, huu mradi uende ukafanyiwe kazi na sisi watu wa Mtwara tunatamani tupate maji safi ya baridi na salama. Kwa mfano sasa hivi ukija Manispaa ya Mtwara Mikindani maji tunapata hatuwezi kumkufuru Mungu tukasema maji hatupati, maji tunapata, lakini Mheshimiwa Waziri anayajua ladha ya yale maji, akasema ili tutatue tatizo la maji ni lazima huu Mradi wa Mto Ruvuma ufanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, huu Mradi wa Mto Ruvuma ni mradi mkubwa na naamini ukifanyiwa kazi utakwenda kutatua changamoto ya maji kwenye majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara ikiwemo Mtwara Manispaa, Mtwara Vijijini, Nanyamba, Tandahimba na Newala kule Nanyumbu huu mradi utakwenda kufanya kazi kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Mtwara walio wengi ukiacha Mtwara Mjini na hizi sehemu kidogo za mjini hawajui kufungua maji bombani.

Mheshimiwa Spika, RUWASA wanasema maji bombani sisi kule kwetu tunasema maji ya kuokota. Mtu unasubiria mvua inyeshe yale yanayotiririka chini ndiyo yaingie kwenye kisima. Watu kila siku wanaumwa matumbo, watu wanaumwa typhoid kwa sababu ya maji ya kuokota. Sasa leo sitaki kuongea sana Mheshimiwa Waziri ameandika mradi huu na hii siyo mara ya kwanza kuandika, naomba kwa heshima na taadhima, mradi huu uende ukafanyiwe kazi. Ni bora afanye mradi mkubwa hata ikiwa kwa awamu, lakini ukiisha unakwenda kutatua changamoto kubwa ya maji ambayo inaukumba Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, naishi Mtwara na najua ukipita Mtwara unakuta mashimo yanayoitwa visima, kama mtu hujazoea unaweza ukashangaa. Tunataka nasi tuvute maji majumbani kwetu yaliyo safi na salama ili kusudi tuweze kuishi kama Watanzania wengine, tunalipa kodi kubwa sana kwa nchi hii, tunaongeza pato la Taifa kubwa sana kwa nchi hii kwa sababu sisi tunazalisha korosho ambayo ni among of the big five cloves zinazoleta pesa katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naamini nimesikika na nimeeleza yale yaliyoko moyoni kwangu. Ahsante sana. (Makofi)