Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mama Samia kwa kuendelea kumwamini Waziri Awesu na kwa kweli naomba nimpongeze sana Waziri Awesu, kama kijana ameitendea haki Wizara, pamoja na Katibu Mkuu na wasaidizi wake. Niseme wazi kwamba mimi binafsi kama Mbunge wa Geita ninakufurahia sana kazi zako na tungependa na Mawaziri wengine wawe kama yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona Waziri Awesu anavyohangaika na anavyopangua na sisi wengine tumepita huko kwenye ukandarasi kandarasi, tunaona jinsi ambavyo anajaribu kurekebisha hata huko kwenye Wizara yake, kwa sababu wizi mkubwa naamini kabisa unaanzia kutoka Wizarani, unateremka kule chini. Nitoe mfano mmoja, kulikuwa na huu mradi nasoma hapa wa miji 16, lakini sijui wametumia formula gani kwa kweli nawapongeza sana mpaka wametoa miji 29, hizo ndiyo akili tunazitaka, wasomi wawe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, tunaona hata sisi tunachimba, lakini kwenye visima bado, Waziri atafute akili nyingine kwa sababu ukiangalia, leo mimi kama Musukuma nikitaka kuchimba maji kisima changu hapa Dodoma kwa kutumia mitambo ile ile na utaalam ule ule, haiwezi kuzidi milioni tisa au milioni 10, lakini ukienda kwenye kisima kinachochimbwa na Serikali milioni 37, inakuwaje huo utaalam? Kwa nini tusiende kwenye utaratibu mwingine, tukaweza hiyo milioni 33 mpaka 35


ikachimba visima vinne mpaka vitano. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kuona namna ya kuwabana wataalam wake waweze kurekebisha ili tuweze kupata maji kwa wingi na kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuniwekea mradi kwenye Jimbo langu nimeona ameweka Vijiji vya Nkome, Senga, Nzera, Rwezera, Idosero, Sungusira na Kakubiro, namshukuru sana, lakini kauli yake ni nzuri sana, hivyo Waziri asinizingue term hii kwa sababu bahati nzuri mradi huu ulikuja kubuniwa na Profesa Mkumbo akiwa Katibu Mkuu na Katibu Mkuu wa sasa Sanga ndiye alikuja kufanya upembuzi yakinifu. Sasa Mheshimiwa Waziri hii ni mara ya pili ananiahidi akinizingua bajeti ijayo nitamzingua mara mbili.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tutakapomaliza suala hili la bajeti hata katikati hapa tukimbie akaone jinsi sisi Wanajimbo la Geita tulivyo wavumilivu, asilimia 92 ya Jimbo langu ni ziwa, lakini sisi tunaugua kichocho tunachota maji machafu, halafu maji yamevutwa yanaletwa mpaka Dodoma. Sasa hivi vitu nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, term hii asinizingue, tumekuwa wavumilivu vya kutosha, aone namna yoyote ile, baada tu ya bajeti hii, naomba tufungue mradi wa maji kwenye vijiji ambavyo ameniahidi. Nami namwahidi nitampa ushirikiano wa kutosha na hata akitaka utaalam wakati wa kuandaa BOQ aniite ili maji yatoke kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aendelee na moyo huu. Nimekuwa Mbunge kwa awamu ya pili, hii bajeti Mawaziri huwa wanaugua tumbo, bajeti ya Wizara ya Maji, lakini naona leo mishale ni michache sana. Hii ni ishara nzuri, anapoitwa anaitika na anapoitika anaenda anatoa action ndiyo maana watu wanamshauri na kumwambia aboreshe pale alipovuruga.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ningeomba Mheshimiwa Waziri, kama hatakuwa na nafasi kwa muda wa karibu kutembelea Jimbo langu, basi namwomba


Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametembea na Wabunge wengi huko, aje na Jimboni kwangu angalau nitembee naye aone hivyo vijiji ambavyo…

SPIKA: Unamwomba Naibu au unamwomba Waziri?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, namwomba Naibu Waziri anaweza ….

SPIKA: Marufuku. (Kicheko)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, Nakushukuru sana. (Makofi)