Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nikuunge mkono kwenye eneo la Wizara kusimamia gharama za uchimbaji au gharama za miradi. Mheshimiwa Waziri na timu yako kama walivyosema wenzangu mnafanya kazi nzuri sana, lakini kule wilayani na mikoani lazima timu yenu pia ishuke ihakikishe inasimamia miradi yote ambayo Serikali imetoa fedha. Tuna mradi wa maji Masukuru, tulilalamika tukasema kwamba mradi ule ulifanywa chini ya kiwango. Nasisitiza kiwango ni kitu cha muhimu sana kwa sababu pesa ikitolewa ni lazima ifanye kazi sawasawa na thamani ya pesa iliyotolewa.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie juu ya Wizara hii hasa walipoanzisha Jumuiya ya Maziwa kwa maana ya Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na mengineyo mmefanya kitu kizuri. Mkoa wa Mbeya una vyanzo vingi vya maji lakini tukitumia Ziwa hili la Nyasa kama ambavyo mmefanya Ziwa Victoria mtakuwa mmetatua tatizo kubwa sana la maji katika Mkoa mzima wa Mbeya wenye majimbo saba. Nafahamu ni fedha nyingi lakini tutakuwa tumetatua tatizo la muda mrefu la wananchi wetu kukosa maji sehemu za Nyanda Juu Kusini na maeneo ya Mbeya jambo ambalo sio sahihi kabisa kwa sababu tayari tunavyo vyanzo vya maji vingi lakini mpaka leo miaka 59 ya Uhuru hatujapata maji ya bomba maeneo mengi sana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwa weledi mlio nao msimamie fedha za Serikali kama alivyosema Mheshimiwa Spika kwamba Wizara hii mnapata fedha za misaada na mikopo tatizo ni mipango na viapaumbele ambavyo ni vyema tukavisimamia.
Mheshimiwa Spika, ukienda katika Wilaya ya Rungwe kuna maeneo ambayo kama nilivyosema yana vyanzo vingi vya maji lakini ukienda maeneo kama ya Kimbira hukuti maji, ukienda sehemu za masoko au sehemu za Buliaga ambako ni mjini kabisa utakuta maji ni shida. Si hivyo tu watu wengine wanapata maji lakini bili za maji zinapokuja pia ni tatanishi. Kuna wakati unaenda kulalamika kwa nini bili yangu mimi nalipa hela nyingi wanakuambia tumekosea, sasa hii ni kwa wale ambao wana uwezo wa kwenda kufuatilia. Kwa hiyo, tunaomba wanaosimamia mambo ya bili na utoaji wa maji maeneo kama hayo uwe wa vigezo vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niliwahi kusema hapa Bungeni kwamba kuna maeneo yanakuwa ni vyanzo vya maji, kwa mfano kwa kule Rungwe sehemu za Mpumbuli na Kasyeto, wao wana chanzo cha maji lakini cha kushangaza mabomba yanapita kama alivyosema Mheshimiwa Tunza wao hawana maji yanaenda sehemu za Ushirika na sehemu zingine wale wenye chanzo cha maji hawapati maji. Nafikiri hatuwatendei haki Mheshimiwa Waziri, najua labda ulikuwa hauna taarifa nakutaarifa sasa kwamba tunahitaji watu wa Kasyeto na wao wapate maji maana chanzo cha maji kinatoka kwao.
Mheshimiwa Spika, suala la ukosefu wa watendaji kazi, nimeona hapa katika hotuba ya Waziri wana upungufu wa wafanyakazi 1,500 na kuendelea. Tunahitaji watu hawa wapate watenda kazi ili kusudi iwe rahisi kuwafikia watumiaji wa maji. Tunaona wakati mwingine hata bili zinachelewa kusomwa kwa sababu anayesoma bill labda ni mmoja kwa eneo kubwa la sehemu husika. Kwa hiyo, mtakapokwenda kuomba watumishi iwape kipaumbele ili kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukweli maji ni uhai na ukimtua mama ndoo kichwani unakuwa umesaidia uchumi wa Taifa kuongezeka. Muda mwingi wanawake wanautumia kwenda kufuata maji mbali na kupoteza muda wa kutafuta pesa kwa ajili ya familia. Kwa hiyo, tunaamini Mheshimiwa Aweso na timu yako mkifanikiwa kusaidia kutatua tatizo la maji mtakuwa mmesaidia Tanzania kuwa ni nchi ya kati katika uchumi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niendelee kuipongeza timu nzima ya Wizara ya Maji lakini pamoja pamoja na pongezi nyingi tunataka mama atuliwe ndoo kichwani maisha yaendelee. Ahsanteni sana. (Makofi)