Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Ghati Zephania Chomete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maji. Kwanza kabisa nampongeza Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri aliyoitoa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia ninampongeza kwa juhudi anazoendelea kuzifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kuhakikisha inaboresha miradi ya maji nchi. Nampongeza sana Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, nampongeza Naibu Waziri wa Maji Maryprisca kwa kazi nzuri wanazozifanya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo. Wamefanya kazi nzuri katika Manispaa ya Musoma kwani hivi sasa wananchi wanapata maji mazuri ya bomba kwa kiwango cha kuridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, Mkoa wa Mara ambao una wilaya nyingi sasa maji ni pungufu sana.

Naomba mradi wa kutoka Ziwa Victoria, ule ambao unaanzia Wilaya ya Rorya uhakikishe Wilaya ile ya Rorya pamoja na vijiji vyake vinapata maji. Hivyo hivyo, Wilaya ya Tarime pamoja na Vijiji vya Nyamwaga mpaka Nyamongo wahakikishe vinapata maji. Niombe Serikali ihakikishe mradi huo wa kutoka Ziwa Victoria unawasaidia wananchi wa Wilaya ya Tarime kwa sababu mpaka sasa wanateseka sana hawana maji. (Makofi)

Mheshimiiwa Spika, vilevile Musoma Vijijini, Butiama pamoja na vijiji vyote vinavyozunguka zile wilaya havina maji. Bunda kuna miradi ya maji mpaka sasa miradi ile inasuasua, niombe Serikali kupitia Wizara hii ya Maji iangalie miradi yote iliyoko Bunda inatekelezeka. Mfano Mwibara kuna mradi wa maji ulipelekewa shilingi milioni 510 wa kutoka Namuhura kuelekea Kwibara lakini unasuasua. Kuna mradi wa kutoka Buramba, Kibara mpaka Kisorya mpaka sasa miradi ile inasuasau. Niombe Serikali yangu sikivu kupitia Wizara hii ya Maji ihakikishe miradi ile inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya Serengeti kuna mradi wa chujio la maji katika bwawa Manchira. Mradi ule ukitekelezeka unasaidia sana Mji wa Mugumu pamoja na vijiji vile vinavyozunguka pale ili wananchi wa maeneo yale waweze kuondokana na kero hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna sera ya kusema kwamba tunamtua mama ndoo kichwani, niwaombe sana Wizara ya Maji wahakikishe wanatua ndoo kichwani wale wanawake wa Mkoa wa Mara maana wanateseka sana. Akina mama wa Mkoa wa Mara ni wachapa kazi, wanaamka asubuhi kwenda kutafuta maji. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sikivu iuangalie kwa jicho la pili Mkoa wa Mara ili kusudi tuweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Rorya, Kata ya Komuge kuna mradi wa maji. Mradi ule ulishatengewa shilingi bilioni 1.3 lakini sasa toka umetengewa fedha hiyo ni miaka mitano sasa umepelekewa shilingi milioni 300 tu. Niombe Serikali ihakikishe mradi ule unatekelezeka. Nasisitiza Serikali ihakikishe inapeleka pesa hizi kwa wakati lakini ihakikishe pia inatekeleza miradi yote iliyowekwa katika Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete. Nilikuwa sijamfahamu, sasa sijui ni katika Waanchari au Wanyichoka au Mkurya au Mjaluo au Mngorebe au Msweta au… Kuna makabila bwana. (Kicheko)

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mtimbaru. Mkurya Mtimbaru.

SPIKA: Naam.

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mimi ni Mkurya Mtimbaru. (Makofi)