Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia hii nafasi. Jambo la kwanza, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu kwa ujumla kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa sababu upatikanaji wa maji safi na salama ni moja ya vipaumbele; na ni kipaumbele cha nne kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025. Kwa hiyo, nampongeza sana kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa na mwelekeo ambao ametupatia kwa kweli unatupa matumaini makubwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, napenda kushauri; kwa muda mrefu tumekuwa tunapitisha bajeti kwa figures kubwa sana, lakini upatikanaji wa hizo fedha kiuhalisia umekuwa ni mdogo sana. Ukiangalia katika miaka yote ambayo tumepitisha bajeti, ukija kusoma uhalisia wa fedha ambazo zimepatikana kwenda kutekeleza miradi ni kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, hata sasa hivi nimepitia ripoti ya Kamati nikaangalia ni kiasi gani cha fedha ambazo zimepatikana? Utakuta wanasema fedha zilizopatikana mpaka sasa hivi na ambazo zimekwenda ni shilingi bilioni 376.4, sawa na asilimia 53.3. Kwa hiyo, hii inatia wasiwasi kidogo. Miradi tunaipanga vizuri, kazi tunazipanga vizuri, lakini fedha zisipokwenda inakuwa ni vigumu sana kuweza kutekeleza hiyo miradi ambayo tumekusudia.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo la Vwawa kuna mradi mkubwa pale Makao Makuu ya Vwawa ambao ulikuwa unatekelezwa, tulipata shilingi bilioni 1,500 kutoka kwenye chanzo cha Mantengu kwa ajili ya kusambaza maji katika Mji wa Vwawa. Mradi huu ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na alipokuja kuzindua akatoa tena fedha shilingi milioni 100 ili kuhakikisha kwamba usambazaji wa maji unaenea katika ule Mji wa Vwawa.

Mheshimiwa Spika, pia Waziri aliyekuwepo alitoa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima vitatu virefu ili visaidie katika kuongeza mtandao wa upatikanaji wa maji. Cha kushangaza, mpaka leo bado kuna shida kubwa ya maji katika Mji wa Vwawa na yale maji hayajasambazwa, zile fedha sielewi zimefanya nini? Vile visima toka vimechimbwa zaidi ya miaka karibu mitatu bado havijaanza kufanya kazi kwa kisingizio kwamba hakuna fedha za kuunganisha ili viweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa hilo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na kazi nzuri anayoifanya, basi hebu akalimulike hilo ili vile visima ambavyo vimeshatumia fedha, basi vikafanye kazi ili wananchi waweze kunufaika na upatikanaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kusema, kuna mradi wa maji wa pale Kata ya Ihanda, ni wa muda mrefu sana, umekuwa na shida, ambao ungesambazwa katika vijiji mbalimbali pale Ihanda. Ulikuwa na matatizo. Mmetoa shilingi milioni 200, bado maji hayajapatikana. Tumechimba kisima, mpaka sasa hivi bado ni shida. Hebu naomba mkalifuatilie mlifanyie kazi ili wananchi wa Kata ya Ihanda na vijiji vyote vinavyozunguka eneo lile viweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, kuna Kata ya Ipunga pale, kuna Vijiji vya Mpera, Ipunga yenyewe, vinahitaji maji. Vinaweza kupata maji kutoka kwenye mto kwa njia ya mserereko, lakini mpaka sasa hivi bado kumekuwa na changamoto ule mradi haujaweza kutekelezwa. Hiyo imekuwa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, kuna Vijiji cha Msiya, Weruwan, Iganduka na maeneo mengine ya Isararo yanayozunguka. Pale tungeweza kupata maji ambayo yangetoka; kuna mradi mkubwa ambao uliwahi kusanifiwa miaka ya nyuma kutoka Rukururu – Mlangali ambao ulikuwa ni wa vijiji 14. Ule mradi kama ungetekelezwa, ungeenda katika vijiji vingi sana na hivyo wananchi wa kule wangeweza kupata maji kutoka katika hayo maeneo. Mpaka Vijiji vya Ibembo vingeweza kupata maji, lakini mpaka sasa hivi ule mradi haujatekelezwa na mpaka sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa maji katika vijiji.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana hata takwimu mnazozisema kwamba upatikanaji wa maji vijijini umefika asilimia 80, sijui labda kwenye majimbo ya wenzangu, kwenye jimbo langu sidhani kwa sababu vijiji vingi bado havina maji safi na salama. Kwa hiyo, hizo takwimu labda pengine zina- fit zaidi kwenye maeneo mengine kuliko katika Jimbo la Vwawa.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa maji ambao ulitekelezwa kutoka kwenye Kijiji cha Idiwiri kwenda Iyura na ukaenda katika vijiji saba. Sasa kitu cha ajabu ni kwamba ule mradi yale maji yanatoka kwenye Kata ya Idiwiri, kwenye Kijiji chenyewe cha Idiwiri ambapo maji yanatoka hakikupata maji; Kijiji cha Iromba ambako maji yanatoka hakijapata maji; Vijiji vya Mafumba havina maji; vijiji vingine maji yanatoka pale yanaelekea kwenye vijiji vingine.

Mheshimiwa Spika, sasa wananchi wa maeneo yale wamekuwa na malalamiko makubwa kwamba wanatakiwa kutunza vyanzo vya maji, wanatakiwa kuhakikisha maji yanakuwepo, lakini wao wenyewe hawajapatiwa maji. Namuomba Mheshimiwa Waziri, hebu lipe uzito, liangalie hilo eneo ili nao waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, kuna Kata ya Nanyara; kuna Vijiji vya Songwe, Songwe - Rusungo, Namronga na maeneo mengine. Kuna mradi wa maji wa mwaka 1972 ambao kwa kweli mabomba yamechakaa sana, umekuwa haufanyi kazi. Mpaka sasa hivi kumekuwa na shida sasa ya upatikanaji wa maji na kwa sababu wakati ule wana-design ule mradi wananchi walikuwa ni wachache, sasa hivi wamekuwa wengi, bado hakuna upatikanaji wa maji wa kuweza kutosha katika lile eneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba katika miradi ambayo wanaenda kuitekeleza kwenye vijiji, basi wakaliangalie hilo eneo ili vijiji vile viweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kuna Kijiji cha Ihoa, Welutuu na Ruvumbila, naomba sana tukaviangalie.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)