Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi na niungane na wenzangu kupongeza Wizara ya Maji chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Waziri Awesso, Mheshimiwa Naibu Waziri, Eng. Maryprisca lakini pia na Watendaji Wakuu, Katibu Mkuu Eng. Sanga na Naibu Katibu Mkuu mama yetu Nadhifa Kemikimba lakini pia na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA na Mameneja wote wa Mikoa na Wilaya zetu kwa kazi nzuri ndani ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu wa binadamu asiyeshukuru kwa kidogo hata kikiwa kikubwa hawezi kushukuru. Nishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa miradi mikubwa ya maji ambayo wametupatia ndani ya Wilaya ya Misenyi, ambapo tunao mradi wa Gera milioni 570 ambao umekamilika katika vijiji vitatu na sasa hivi nikushukuru sana Waziri kwa kutupatia extension katika vijiji vingine viwili vya Kashaka na Kashekya. Kwa hiyo, maana yake katika eneo hilo vijiji vyote vitakuwa vimefikiwa kwa kupata maji kutoka kwenye Mradi wa Gera.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, wananchi wa Misenyi wanakushukuru pia kwa mradi mkubwa wa maji wa Kyakabulanzi wa bilioni 15.1 ambao tumeendelea kufuatilia unavyoendelea kujengwa na upande wa mkandarasi hela zimeendelea kwenda kwa kiasi lakini pia na upande wa force account kutumia wataalam wetu nimeambiwa vifaa vimeendelea kupelekwa. Kwa hiyo, tukushukuru lakini tuombe basi uwezeshaji uendelee ili uweze kukamilika wananchi wa Kyaka, Kasambya na majirani pale waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, niendelee kushukuru kwa bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa miradi ambayo kutoka katika wilaya yetu imeweza kupitishwa na Wizara. Na tunaona katika maeneo mbalimbali miradi ya mradi wa maji katika eneo la Kashenye na Bushago na Bukwali tumeweza kupata fedha kiasi kwa ajili ya kupata maji lakini tumeona mradi wa Kitobo Katolelwa, Byemagwe, Byeju na Byamtemba yote imeweza kupata lakini na uchimbaji wa visima saba katika vijiji mbalimbali na kutanua mradi wa Kashaba.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Wizara ya Maji ni kuomba kwa kazi nzuri ambayo mmeshaifanya tayari, kuna miradi ambayo katika mwaka huu wa bajeti ambao unaisha tarehe 30 Juni, ilikuwa aidha ipo kwenye pipe line au imeshafanyiwa hatua za awali. Kwa mfano, tukiangalia katika eneo la Rwamachu na Rutunga Wizara mmechimba visima na wananchi wameshangilia kuona maji mengi yanatoka. Kwa hiyo, ni matarajio yao kwamba baada ya vile visima kuchimbwa tulikuwa tunaona hatua ya pili sasa ni kupeleka maji yawafikie wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini katika hii bajeti sasa 2021/ 2022 tunaona kwamba tumeacha nyuma. Niombe Mheshimiwa Waziri najua bajeti sio kubwa sana tunagawana kilichopo, lakini basi wananchi wa Rwamachu na Rutunga waweze kuona sasa mradi unawafikia. Lakini sambamba na hiyo, Wizara imechimba visima katika kijiji chetu cha Ruano na Nyalugongo na yenyewe visima tayari vimechimbwa. Kwa hiyo, tungefarijika kuona sasa baada ya uchimbaji na wananchi kujitoa kwa ajili ya kushirikiana na Wizara na kuona maji yanawafikia basi, ndani ya bajeti hii ya 2021/2022 na eneo hilo liweze kuwekewa umakini ili bajeti iweze kutengwa wananchi hawa wapate maji.

Mheshimiwa Spika, lakini niombe kumkumbusha pia Mheshimiwa Waziri katika Kijiji chetu cha Kashasha chanzo kipo ni mradi wa Mbale ni extension ya kujenga matenki na kusambaza maji wa mserereko kwa wananchi wa Kijiji hicho cha Kashasha ili waweze kupata maji. Na katika bajeti ya mwaka huu ambao unaisha tarehe 30 Juni ilikuwa imetengwa hela kadhaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huo unafanikiwa. Kwa hiyo, nikuombe sana Wizara yetu ya Maji iweze kutusaidia katika maeneo hayo kwa kiasi kikubwa naamini, kama miradi hii itatekelezwa ndani ya Wilaya ya Misenyi angalau upatikanaji wa maji utakuwa umefikia takribani asilimia 72 au 75.

Mheshimiwa Spika, lakini tunaendelea kushukuru kwa kuanza maandalizi ya miradi mbalimbali katika Kata yetu ya Minziro kwa Vijiji vya Minziro, Kalagara na Kigazi. Naamini na wananchi hao baada sasa ya upembuzi ukikamilika na vijiji vingine vya Rwamashonga lakini tumeona Mwemage kote kazi inaendelea pamoja na Kyazi. Niombe sana kuungana na wenzangu suala ambalo limekuwa likitatiza kidogo kwenye miradi yetu ya maji na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuombe Wizara kwa juhudi kubwa ambazo imeendelea kufanya na sisi kama kuna vikwazo vingine basi, ni kuliambia Bunge Tukufu kusaidia hasa cash flow ya miradi ambayo tayari iko kwenye pipe line inaendelea. Naamini kama fedha zikiwa zinakuja kwa wakati ingesaidia sana Wilaya fulani haivuki ikiwa na miradi viporo kwenda katika mwaka wa fedha unaofuata. Ikishavuka miradi haijatekelezwa na ilikuwa kwenye bajeti iliyopita inakuwa ni shida kidogo, maana yake mwaka ujao tunategemea tupate sasa miradi mipya kuliko hii ya nyuma ambayo haikutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuombe sana kwa juhudi kubwa mnazozifanya tuna Imani na Wizara kwa utendaji kazi wa Waziri na Wasaidizi wako wote, tunaamini haya yote yataweza kutendeka na wananchi wataendelea kupata maji na tutafikia asilimia zile ambazo zinaendana na sera ya maji katika vijiji na miji na tupate maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kwa Wilaya ya Misenyi niseme wananchi wanafarijika sana na kwasababu, vyanzo vya maji ni vingi tunaendelea kupata matumaini hayo.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)