Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI):
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuniwezesha kuwepo hapa kujibu hoja ambazo zimechangiwa na Wabunge pamoja na Kamati ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikushukuru wewe kwa kutuongoza pia nimshukuru Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nikiwa kama mama basi sitamuangusha katika kutekeleza na kumsaidia majukumu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Dkt Philip Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiongoza na kutuongoza katika nchi yetu. Kipekee nimshukuru Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii Dkt Dorothy Gwajima kwa upendo na ushirikiano wa hali ya juu ambao amekuwa akinipa wakati wa kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa michango yao mizuri na maoni yao waliyotupa tutajitahidi kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge wote wananchi wa Chama cha Mapinduzi pia niwashukuru watanzania wote niwape pole watanzania wote kwa kuondokewa na viongozi mbalimbali katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kujibu hoja za kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, kuhusu Serikali kutoa ajira kwa maafisa wa jamii na maafisa wa jamii kuwa katika vyuo vyetu vilivyoanzishwa na wataalamu hawa kutosha kuwepo wakiwa hawana ajira. Wizara imepokea ushauri wa Kamati. Aidha Wizara inaendelea kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kutatua changamoto za upungufu wa maafisa wa maendeleo ya jamii maafisa ustawi wa jamii katika ngazi za mamlaka za Serikali za Mitaa kadri bajeti ya Serikali itakavyoturuhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maendeleo kwa vyuo vya maendeleo ya jamii kuongezwa lakini pia fedha zilizotengwa zitolewe zote kwa wakati hasa kuzingatia vyuo hivi ndivyo vinavyotegemewa kuanzisha maafisa maendeleo ya jamii ambao ndio nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imetoa ushauri kwa kamati aidha, mwaka 2021/2022 Wizara imeandaa fedha kiasi cha shilingi milioni 3.6 kwa ajili ya ujenzi wa ukarabati wa maendeleo na miundombinu ikiwemo kumbi za mihadhara mabweni, maktaba na majengo ya utawala katika vyuo vya maendeleo kwa jamii ya Ruaha shilingi milioni 600, Rugemba shilingi milioni 500, Uyole shilingi bilioni moja na Mlale shilingi milioni 500 na Monduli shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango itafanya kazi kwa utaratibu na kuhakikisha kwamba fedha hizo zilizotengwa kwa mwaka 2021/2022 zitatolewa kwa wakati ili kutekeleza kazi zilizopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bajeti ya kuwezesha utekelezaji wa mipango kuzuia ukatili wa kijinsia kutengwa na kutolewa wakati badala ya kutegemea fedha za nje. Wizara imepokea ushauri wa kamati kwa mwaka 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 791 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali za kutokomeza ukatili wa kijinsia. Wizara itaendelea kutenga fedha za ndani kwa ajili ya kulingana na ukomo wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika kujibu hoja aliyoitoa Mheshimiwa Bahati Keneth Ndimbo Mbunge wa Viti Maalum kuhusu vituo vingi vya wazee kuwa nje ya mji na vinahatarisha maisha ya wazee kutokana na kuwa mbali na vituo vya afya. Pia kuhusu huduma za afya zinazotolewa katika vituo vya wazee kupata huduma ya kwanza tu ambazo haziwasaidii wazee wanaoishi katika vituo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia na kutoa huduma kwa wazee katika makazi 13 inayomilikiwa na asilimia kubwa ya makazi hayo yapo mjini. Mfano Fungafunga ambayo iko Morogoro Manispaa ya Morogoro, Ipuli Tabora Manispaa, Nunge Kigamboni, Njoro Moshi Manispaa, Magugu Babati Mjini, Kalandoto Shinyanga Manispaa, Makumbi, Misingwi, Mwazange Tanga Jiji, Nyambange Musoma Manispaa, Kilima Bukoba Manispaa na Kibirizi Kigoma Manispaa. Makazi yaliyo nje ya mji ni Muheza na Sukumahale Singida hata hivyo Serikali imeandaa kuisimamia huduma hizi kuhakikisha uwepo wa wahudumu wa afya katika makazi ya wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya wazee na halmashauri ikiwemo vituo vya afya katika maeneo ya makazi yaliyopo upatikanaji wa huduma hizo zimeimarishwa. Hata hivyo juzi mimi katika ziara yangu toka nilipochaguliwa nimetembelea Kituo cha Nunge na kuona wazee wako vizuri sana na niliwauliza wahudumu wa afya wakaniambia wanapatiwa huduma zote dawa zipo hawana wasiwasi na wanashukuru sana Mheshimiwa Rais wao Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumteua mwanamke ambaye ataendeleza kuwalea Wazee wale kwa kushirikiana na Serikali ambayo ya Awamu ya Sita inayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hoja ya Mheshimiwa Ritta Kabati Viti Maalum Watoto saba waliobakwa na mwanaume mmoja kati ya Mkoa wa Iringa Serikali iangalie sheria kulinda Watoto hawa. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa karibu unaofanywa na masuala ya haki ya ustawi wa jamii ya mtoto tumeipokea taarifa na ufuatiliaji kama sehemu ya utekelezaji wa Wizara kupitia MTAKUWA.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ili kuhakikisha haki zote zinalindwa Serikali imeongeza idadi ya mahakama za watoto kutoka mahakama tatu mwaka 2015/2016 hadi kufikia mahakama 147 mwaka 2021. Pia Serikali itaendelea kuratibu utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa mashauri ya watoto mahakamani. Kupitia maafisa utawala wa ustawi wa jamii vilevile Serikali inaendelea kuimarisha dawati la jinsia la Watoto katika vituo vya Polisi ambapo hadi kufikia Aprili 21 madawati 420 yameanzishwa nchi nzima ili kuhakikisha mashauri ya Watoto yakiwemo ubakaji yanasimamiwa kwa umakini kwa lengo la kulinda haki za Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tokea niteuliwe nimeamua kuandaa mikakati ambayo tutashirikiana na TAMISEMI na Mahakama na Ofisi ya Mambo ya Ndani ili kuweka mikakati hii ambayo kukomesha ukatili wa watoto katika nchi yetu, na suala hili tutapita halmashauri zote katika mikoa yote ya Tanzania kuelimisha suala hili ambapo mikakati yetu itakapokuwa sawa Waheshimiwa Wabunge nakutakeni muwe ni walezi na kutoa ushauri na hoja ambazo mtakazozitoa katika kuelimisha wananchi maana nyinyi kama mlivyoweza kuwahadaa wananchi wakakupeni kura mkafika hapa nafikiri na nyinyi ni rahisi kuwahadaa watu hawa hawa…

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Noah Lembris.

T A A R I F A

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri ametumia lugha ambayo kidogo ina washushia Waheshimiwa Wabunge hadhi au Bunge hili kwamba tumewahadaa wananchi kuwadanganya ili waweze kutuchagua hivyo ningeomba atumie lugha ya staha au arekebishe kauli yake.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri nadhani ulikusudia kusema kuwashawishi.

NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba nimepokea hoja nilikusudia kuwashawishi lakini katika kutekeleza na kuhamasisha wananchi imenibidi nitumie hoja ya haraka haraka kuwahadaa samahani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wenzangu nakuombeni mikakati ambayo tutakayoipanga mtusaidie kwa wananchi kuwahamasisha ili kutokomeza ukatili katika nchi yetu na mimi nitakuwa pamoja time yoyote wakati wowote na tutatoa matangazo na namba za simu mikoa yote hadi vijijini ili likitokea suala hili niweze haraka kusimamiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawatahadharisha ambao Wakurugenzi mahakama ma-DPP ambao wanadhorotesha kesi hizi tutakuwa sambamba, mtu ambaye tutamgundua anadhorotesha kesi hizi basi hatua za haraka tutazichukua ama kumuhamisha kumuweka mtu mwingine ili ukatili huu uondoke hapa nchini. (Makofi)

Kuhusu hoja ya Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas ambayo inahusu kuandaa namna bora ya kuwapatia watoto yatima walioko kwenye vituo hati za kuzaliwa ili ikiwezekana waanze shule huku ufuatiliaji wa hati zao ukiendelea. Kuhusu watoto yatima wasio na vyeti vya kuzaliwa naomba nipokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Aidha, Wizara itaendelea kuwasiliana na RITA, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia ili kuhakikisha kuwa watoto yatima wote kwenye vituo wanapatiwa vyeti vya kuzaliwa na kuendelezwa kielimu ili kupata haki yao ya msingi mpaka hapo watakapoanza kujitegemea wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Norah Mzeru aliongelea suala la wanawake kukumbukwa katika masuala ya afya na kuwawezesha kiuchumi ili kuweka mazingira bora kuanzia ngazi ya halmashauri. Serikali inaendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia programu mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Kupitia mpango huu, Serikali imewezesha wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu katika Benki ya TPB na asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali inaendelea kuwaunganisha wanaweke wajasiriamali na taasisi kutoa mafunzo ili kuwajengea uwezo wa kibiashara wa usindikaji wa bidhaa na matangazo ya biashara kwa njia za mitandao. Halikadhalika, Serikali inawawezesha wanawake wajasirilimali kushiriki maonesho ya kibiashara ya Sabasaba na Nanenane, program za uwezeshaji wanawake kiuchumi na makongamano ya kibiashara ili kujua mahitaji ya masoko ya bidhaa zao. Hivyo, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza afua na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, anauliza Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha wazee wanapata Bima ya Afya. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea na zoezi la uchambuzi wa wazee ili kuwapatia vitambulisho vya matibabu. Hadi kufikia Machi 2021 jumla ya wazee wanaume 1,834,995 na wanawake 1,002,567 wametambuliwa ambapo wazee wasio na uwezo 1,042,403 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo. Aidha, Serikali inaendelea kukamilisha rasimu ya Muswada ya Bima ya Afya kwa wote wa mwaka 2020 ili kuwawezesha wananchi wote wakiwemo wazee kupata huduma za matibabu kwa mfumo rasmi na ulio mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja na kuwapongeza Wabunge wote waliotoa hoja zao katika kurahisisha utendaji wa Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Nawashukuru sana kwa michango yenu. (Makofi)