Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia nafasi hii pia kwa kuzisemea barabara ambazo kimsingi zimeshakuwa kwenye ahadi za ilani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu ilani ni mkataba wetu sisi na wananchi na hasa kwa Chama Cha Mapinduzi ambapo 2015 kuja mwaka 2020 tuna barabara ambayo imewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi, barabara ya Karatu – Haydom – Dongobesh kuja Singida kwenda Sibiti, Lalago.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeiona katika kitabu chetu hapa, na barabara hii imeahidiwa na Rais wetu mpendwa, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kutoka 2015 kuja 2020. Lakini pia juzi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Sita amekuja Dongobesh ameahidi barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara moja tu iliyobaki ambayo inaunganisha mikoa minne ambayo haikujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii inatoka Jimbo la Karatu kuja Jimbo la Mbulu Mji, maana yake inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inatoka Mbulu Mjini kuja Haydom kwenda Singida, maana yake inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. Na kutoka pale inaelekea Maswa, maana yake unakutana na Mkoa tena ule wa Simiyu, na kwenda pia Shinyanga kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nieleze kwamba barabara hii ndiyo barabara iliyosahaulika moja kwa moja. Ni barabara chache mno ambazo hazikuunganishwa kwa lami kwa mikoa hii. Kwa hiyo, masikitiko yangu nataka nioneshe Mheshimiwa Waziri aelewe.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Yahaya Massare.

T A A R I F A

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumpa taarifa mchangiaji anayechangia sasa hivi, Mheshimiwa Flatei, si barabara hiyo tu iliyosahaulika, ni pamoja na barabara ya Mkiwa – Itigi – Rungwa – Makongorosi kutokea upande wa Mkoa wa Singida, imesahaulika toka Uhuru. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Naona taarifa za nyongeza za barabara. Sasa sijajua na mimi nikupe taarifa nyongeza ya barabara nyingine; Mheshimiwa Flatei Massay, unapokea taarifa hiyo?

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hii ya Mheshimiwa Massare naipokea kwa moyo mweupe, na ile ya kwako naipokea kwa sababu najua kuna barabara imesahaulika ya kutoka pale Mbeya kwenda mpaka Tunduma kule, hali ni mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze tu Waziri aelewe kwamba wameteuliwa na Mheshimiwa Rais sasa wamekuwa Mawaziri wako watatu, yaani Waziri na Manaibu wawili. Tangu Uhuru, Mbulu imeanzishwa 1905, haina barabara. Ukiangalia Mbulu kwa maeneo yote barabara ziko nyingi; barabara ya kutoka Dongobesh kwenda Babati, kilometa 63, imeahidiwa pale iko kwenye ilani, hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tunapouliza maswali, mimi nimeleta barabara hii mara 20 ndani ya Bunge hili, nimeuliza maswali 20, nimechangia kwenye mchango wa namna hii ninavyoongea hii ni mara ya tano. Na barabara hii acha tu nikwambie, ina magari mengi. Na kwa uchumi wa watu wa Mbulu, Singida, Karatu, Simiyu, Meatu, hakuna namna yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe, mara ya kwanza nimekuja kusema barabara hii nikaambiwa iko kwenye upembuzi wa awali, nikatulia. Nimekuja 2017 wakasema iko kwenye upembuzi wa kati, nikatulia. Nimekuja tena wakasema iko kwenye upembuzi yakinifu, nikatulia. Juzi hapa wananiambia sasa iko kwenye design and building; natuliaje sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mbulu wametutuma hapa kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. Sasa nikuombe unisikie leo; nifanyeje ile nieleweke? Kwenye ilani ipo, kwenye ahadi za Rais wetu ipo, wametuambia bajeti iliyopita iliwekwa kwenye kitabu cha bajeti inaonekana kilometa 50 zitajengwa kwa kiwango cha lami. Leo naona huku wamepunguza tena imekuja kilometa 25. Sasa nawaza kwa nini tunafanyiwa hivi. Kama rasilimali tunagawana katika Tanzania nchi yetu tugawane kwa usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani, naitwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, nimekuja huku niambie tufanyeje sasa. Kama tumetumwa, tumeeleza na uwakilishi upo eneo hili halijengwi. Leo naangalia kitabu cha bajeti hapa, sitaki kusema vibaya lakini mnielewe tu ndugu zangu kwangu hakuna barabara ya lami. Lakini wengine nimeona hapa siyo sahihi, wamewekewa bajeti ya kufanya ukarabati wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukarabati wa barabara, sisi hatujawahi kuiona barabara ya lami kabisa, wengine humu wana ukarabati. Kwa nini sisi tutakutana lini na changamoto hii kuisha? Wengine wana ukarabati; nini maana ya ukarabati? Wameshakaa na barabara, muda umefika hali yao imeshakuwa nzuri, barabara inakarabatiwa. Sisi ambao barabara hakuna hata kilometa moja lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Ujenzi ijue; nikipata nafasi kwenye kushika shilingi nitaishika mpaka ya mwisho ili kuhakikisha barabara hii inafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hii password ya kwamba kila siku upembuzi yakinifu, upembuzi wa awali, upembuzi wa kati; lini unaisha ili barabara hii ikajengwe kwa kiwango cha lami? Wananchi wanataka kusikia haya, wananchi wanataka kuona greda zinaanza kazi na barabara inajengwa.


Mheshimiwa Naibu Spika, na nimeshaomba mara nyingi, kuna Hospitali kubwa ya Haydom kule, maeneo haya watu hawawezi kupita, barabara imeharibika. Ni kweli wanajenga, sikatai, wanajenga kwa maana ya rough road, lakini kila ikijengwa, kila mwaka lazima barabara ile ijengwe ya Haydom – Mbulu – Hydom – Sibiti – Lalago, kilometa 389.

Mheshimiwa Naibu Spika, nifanyeje? Ni mtaalam wa sarakasi, au niruhusu basi sasa hivi nipande hapo nipige sarakasi tatu, nne, ili Naibu Waziri na Waziri wajue kwamba huyu Mbunge amechukia. Niruhusu basi naomba. Nipige? Nipige sarakasi kadhaa hapa? Niruhusu, mimi najua Kanuni haziruhusu, basi niruhusu nipige wajue kwamba kwamba nimetumwa na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kuiomba barabara. Nipige?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nipige?

WABUNGE FULANI: Piga!

NAIBU SPIKA: Usipige. Tunafahamu unajua sana kupiga sarakasi lakini…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, najua sarakasi, sasa nafanyaje?

NAIBU SPIKA: Mimi nakulinda, usije ukaumia kwenye viti.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ilani ipo; ahadi ya Marais ipo; ahadi nyingine zipo; nipige? Mimi naomba nipige kabisa. Nipige? Maana hali ilishakuwa mbaya, wananchi wanataka barabara, Waziri haelewi; Haydom – Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti; nifanyeje? Kwenye ilani ipo, kwenye kila kitu ipo, nifanyaje? Nipige? Sasa nafanyaje? (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri aje kwende wind up yake pale asiposema barabara hii anajenga lini kwa kweli humu ndani hatutaelewana, kama ni kuvunja sheria tutazivunja zote na kama kupiga nitapiga zote humu ndani. Haiwezekani wengine wapate barabara, sisi tunaongea kila siku habari ya barabara humu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, twende moja kwa moja kwenye eneo lolote la bajeti hii. Wenzetu wana billions kadhaa, sisi tuna bilioni tano tu; itajenga barabara lini? Kilometa 389. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, wewe ni mgeni lakini wamekuja wengi; amekuja Prof. Mbarawa kaona barabara ile, amekuja Engineer Nditiye kaona barabara ile, kaja Naibu Waziri kaona barabara ile, nampongeza amekuja kuona. Sasa akija kuona wananchi wanajua naam, barabara inajengwa, mwaka unapita, miaka inapita; inakuaje sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, principles zetu ni kwamba iko kwenye ilani, principles zetu ni kwamba ahadi za wananchi, principles zetu ni kwamba Marais wameahidi, sasa mama Samia Suluhu Hassan niwaambie ni mama mzuri sana, kashaahidi. Na amesema kazi iendelee. Sasa kazi inaendelea kwingine, Mbulu Vijijini haiendelei? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwaka huu wa fedha barabara mtangaze ili ijengwe ili wananchi wale ambao miaka yote wamekuwa wakitutuma humu, ametumwa Maru amekaa miaka 25 hakupewa; katumwa Akunayi naye kaka hakupewa, tumetumwa mimi na Issaay, tusipewe tena?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mungu awabariki. Sasa sijui niunge mkono, sijui niache? Naunga mkono kwa shida sana. (Makofi)