Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Serikali pamoja na Waziri wa Viwanda kwa hotuba yake nzuri ambayo inaleta changamoto na watu wote tunaipongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wana msemo wao, wanasema: “asiyesikia la mkuu, badala yake, huvunjika mguu.” Kwa nini nimesema hivyo? Nimesema hivyo kufuatana na mazingira ya maongezi. Tunapokaa hapa, ni kwa ajili ya kuchangia mawazo ya wananchi waliotutuma. Kwa hiyo, usiposikiliza mawazo ya wananchi waliotutuma, matokeo yake ni kwamba tutakuja kuvunjika miguu, utakaporudi kwenye uchaguzi unakuwa huna la kwenda kuongea kwa wapiga kura wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la viwanda. Bahati nzuri Wizara ya Viwanda ina Waziri makini na Watendaji wake makini. Tunasema hivyo kwa nini? Kwa muda mfupi tumeona Katibu Mkuu pamoja na Waziri wamezunguka sana katika maeneo kuangalia viwanda gani vimekufa na vipi viamshwe. Naomba sana na nataka nirudie kauli yangu ambayo niliitoa wakati ule wa mipango, hapa hatupo kupendezana, tupo kwa ajili ya kujenga nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kwamba mwaka huu tunataka Tanzania ya Viwanda, sikatai, naiunga mkono mia kwa mia; lakini naomba nirudie Mheshimiwa Waziri. Tunaposema viwanda, tunaviangalia viwanda vilivyokufa; na kama tunaangalia vilivyokufa, ni namna gani tutavianzisha viwanda vilivyokufa ili vije vijengwe viwanda vingine? Leo hii kiwanda cha General Tyre Arusha kingekuwa kinafanya kazi, Watanzania wengi wangekuwa wanaingia pale kufanya kazi, badala yake tunasema tunajenga viwanda. Tufufue Arusha General Tyre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kiwanda cha kutengeneza magodoro Dodoma, kilikuwa kiwanda kikubwa na wananchi wa Dodoma walikuwa wanakitegemea sana, badala yake kiwanda hiki kimehamishiwa Dar es Salaam. Wale wafanyakazi ambao wangeweza kusaidia au wangeweza kupata kazi hapa, Dodoma watapata kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanga nimemsikiliza mchangiaji mwenzangu pale, katika mikoa ambayo ilikuwa ni mikoa ya viwanda; ilikuwa kama mikoa mitano au minne; Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Sasa hivi ndiyo imekuwa mikoa maskini kuliko mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Kiwanda cha Foma kimeondoka Tanga kinakwenda Dar es Salaam. Kwani Tanga hakuna wananchi? Leo hii Kiwanda cha Chuma, kilikuwepo Tanga, hakuna! Leo hii hata Viwanda vya Mkonge, wanafanya kuungaunga maskrepa ili kufungua viwanda vya mkonge ambapo mkonge mmeweka katika zao la biashara. Leo hii ninapokwambia, kuna viwanda vya mkonge, acha viwanda ambavyo vinataka kujengwa, wafanyakazi wake wanayanyaswa kama watoto wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shamba la Kwa Shemshi, kuna Kiwanda cha Mkonge ambacho wafanyakazi wametoka bara; imagine kama mimi Maji Marefu, nimetoka Songea, nilikwenda kule kama Manamba; na wengine wametoka Kigoma, wengine wametoka Usukumani, wamekwenda kule kama Manamba; lakini Manamba yake ilikuwa ni kwenda kufanya kazi. Leo hii shamba hilo linabadilishwa na watu zaidi ya watatu; wametumia kigezo gani? Wametumia sheria gani? Hatua ya mwisho, wafanyakazi wanafukuzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapomwambia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, shamba la Kwa Shemshi wafanyakazi wamefukuzwa na wanaambiwa hawalipwi na shamba hilo limeingiwa na Mwarabu, alipotoka hajulikani; kwa mkataba gani, haujulikani. Sasa mnaposema kwamba Watanzania wanatakiwa wakafanye kazi, watafanya kazi gani? Sina maana kwamba Mwarabu ni wewe Mheshimiwa Keissy, hapana, naona unaanza kujitutumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani naona huyu ananisumbua kwenye message zangu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nairidhia sana Serikali yetu hii, naomba sana tuangalie kwa mfano Kiwanda cha Urafiki Dar es Salaam, kilikuwa kina wafanyakazi chungu nzima, wako wawekezaji wa Tanzania wana uwezo, kama akina Mheshimiwa Bakhresa, Mheshimiwa Mengi, na Waheshimiwa wengine ambao wanafanya kazi vizuri, hakuna upungufu. Leo tunaleta Wachina, tunawaambia waje wafanye biashara. Badala ya kufanya biashara, wanafanya ni kiwanda cha kutengeneza mbao. Kilikuwa kiwanda cha kutengeneza nguo, kinabadilishwa kinakuwa kiwanda cha kutengeneza mbao. Ndiyo mikataba yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ya kuendeleza viwanda vyetu ni nini? Maana yake ni kwamba viwanda ambavyo havifanyi kazi, ambavyo vilikuwa vimekufa vipewe watu ambao ni wazawa wenye uwezo wa kufanyia kazi, badala ya kutegemea majitu yanayotoka nje, yanakuja hapa kuchukua viwanda vyetu kwa ajili ya kukopa pesa zetu, wanapeleka huko, halafu wanatuambia Watanzania ni walalahoi. Nani mlalahoi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga kulikuwa kuna Kiwanda cha Saruji, hakipo; kulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, hakuna; kulikuwa na Kiwanda cha Sabuni ambao ni Gardenia, hakuna; kulikuwa kuna Kiwanda cha Foma, kimehamishiwa Dar es Salaam; kulikuwa kuna Kiwanda cha Chuma, hakuna; kulikuwa kuna Kiwanda cha Matunda Korogwe, mpaka scraper zimetolewa; kulikuwa kuna kiwanda cha kutengeneza ceiling board kipo Mkumbara, lakini cha kushangaza kiwanda kile sasa kimekuwa cha kuchoma mkaa. Maskrepa yameondolewa yamepelekwa sehemu nyingine. Morogoro kulikuwa kuna viwanda chungu nzima, badala yake vinakuwa ni nyumba za kufugia mbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu zangu, Mheshimiwa Waziri yupo makini na bahati nzuri safari hii Mawaziri wote wapo makini. Mnafanya kazi kwa kujituma bila kuangalia itikadi ya Vyama. Naomba sana, tusianze kusema tunajenga viwanda vingine, nendeni Bagamoyo mkaanzishe Kiwanda cha Sukari. Hizi kesi tunazopata za sukari, hatutazipata. Nendeni kule APZ, nendeni Kigoma, kaangalieni Kiwanda kile cha Mawese, kimefikia wapi? Kaangalieni viwanda vya kutengeneza samaki, hebu tuangalieni ukanda huu wa Pwani, ni wapi kuna kiwanda cha kutengenza samaki? Vipo kule ziwani, Mafia hakuna.
Hebu tufanyeni. Tusifanya kazi kwa mazoea. Tufanye kazi kulingana na mazingira ya Watanzania, wanatakaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaseme haya kwa sababu naipenda sana Serikali yangu na ukimkuta mtu hapa kazi yake ni kuja na kuiponda Serikali na kuitukana, nafikiri ana upungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacholilia sana ni kwamba tuifanye kazi yetu, wote tuungane, tusiangalie itikadi ya Vyama, tujaribu kukupa mawazo mazuri. Mheshimiwa Waziri, mtu anapokupa mawazo mazuri, usiangalie Chama chake, angalia huko tunakotoka, tuna matatizo gani? Tukisema tuangalie kwamba huyu anatoka sehemu nyingine, hatutapata nafasi nzuri ya kuwa na viwanda vizuri na bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama kuna tatizo kubwa, Mheshimiwa Waziri anza kuangalia Mkoa wa Tanga ambao ulikuwa ni Mkoa wa viwanda. Viwanda ambavyo vipo, vinaweza kupokea vijana zaidi ya 20,000 badala ya kujenga viwanda vipya ambavyo havitakuwa na maana, havitatusaidia lolote wakati viwanda vya zamani vipo na majengo yake yapo. Hapa kwanza inapunguza gharama ya watu kuanza kutafuta utaratibu mwingine. Una viongozi wazuri ndani ya Wizara yako, wote ni watu watendaji. Nimewapitia kupitia Kamati yangu ya PAC, tumewaona ni wazuri. Naomba tuzitumie nguvu zetu kwa kushirikiana na sisi Wabunge ili mwone tutafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muheza kuna matunda, kiwanda hakuna. Kiwanda cha Gossage Tanga kimekufa; Sumbawanga huko ndiyo usiniambie, walikuwa na Kiwanda cha Maziwa, hakuna kitu. Sasa niliona niyaseme haya kwa sababu Kilimanjaro kulikuwa na Kiwanda cha Kahawa, hakipo tena; kulikuwa kuna Kiwanda cha Magunia hakuna; leo tunataka tujenge vingine. Tuanze vya magunia Kilimanjaro, tuanze kile cha Kahawa Kilimanjaro, tukimaliza hivyo ndiyo tunajenga viwanda vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, sitaki kupoteza muda sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.