Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza kabisa nianze kwa kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri hasa kwenye mambo ya ujenzi. Nianze kwa kuchangia kwa kuzingatia mambo mawili kwanza hotuba ya Rais lakini pia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na pia nikijikita kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Nitajikita zaidi kwenye jimbo langu la Makete kwasababu ndipo ambako tuna changamoto kubwa ya barabara hasa hasa kutokana na kwamba sisi ndio wilaya pekee Nchini tuna miezi minane ambayo mvua inanyesha bila ya kusimama. Kwa hiyo Makete ina uhitaji mkubwa wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza nataka nizungumzie barabara ya kutoka Isyonji – Makete kwa maana ya kupitia Kitulo ambayo ukisoma kwenye ripoti kwa maana ya hotuba ya waziri ipo kwenye ukurasa namba 148 lakini ukisoma kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi iko kwenye ukurusa namba 74. Hii barabara kwanza niseme ni barabara ambayo Mheshimimiwa Rais aliagiza alipofika Makete akawaahidi wananchi kwamba barabara hii itajengwa tena Rais mwenyewe ni huyu huyu Mama Samia Suluhu Hassan akasema barabara hii itajengwa. Na niwaombe Mheshimiwa Waziri, ninajua kwamba ipo katika mkakatati wa kutangazwa barabara hii ili iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ninaizungumzia barabara ya Makete kutoka Isyonjo kuja Makete kupitia Kituro ni kwa sababu moja barabara hii ndio oxygen ya uchumi wa Wilaya ya Makete. Ni oxygen kwa mantiki ipi ni kwamba barabara hii inapita kwenye mbuga ya Kituro, hifadhi pekee ya tofauti kabisa ndani la Bara la Afrika, hifadhi ya Kituro inategemea barabara hii ya kutoka Isyonji kuja Makete. Lakini pia nazungumzia barabara hii ni kwa sababu, barabara hii ndio inabeba uchumi mzima wa wafanyabiashara wa Makete na kwa zaidi ya miaka 30, 40, 50 ambayo tangu nimezaliwa barabara hii wananchi wangu wanateseka kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili barabara hii ndio inapeleka karibia wagonjwa wote wanaotokea Mkoa wa Mbeya kwenye hospitali bora za Nyanda za Juu Kusini, Hospitali ya Ikonda. Wagonjwa wengi wanatoka Mbeya wanapita pale lakini wengi wanafia njiani kutokana na changamoto ya barabara hii. Barabara hii ni kitovu cha uchumi wa Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri; kwa uhitaji mkubwa tulionao barabara hii ni vyema tangazo likatoka mapema wananchi wakatangaziwa kwamba barabara hii inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumzie barabara nyingine, barabara kutoka Chimara, Matamba, Kitulo; kwanza nizungumze jambo moja kwamba Waheshimiwa Mawaziri hasa hasa Wizara ya Ujenzi, ukiangalia Wabunge wengi hapa wana ahadi nyingi za viongozi ni vyema Wizara ya Ujenzi ikawa na benki ya ahadi za vongozi kwa wananchi wetu. Kwa sababu gani? Viongozi wakubwa wa Serikali wanapokuja kuahidi hizi barabara wanafanya wananchi waamini kwamba hizi barabara tayari zinakwenda kujengwa. Barabara ya Chimala, Kitulo, Matamba ambao ni kilometa 51 ni ahadi ya Waziri Mkuu Pinda hadi leo hii haijawahi kujengwa. Sasa wananchi wa Matamba, wananchi wa Makete wanaamini kabisa Waziri Mkuu akisema ndio tayari imeshatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema wizara ikaanda benki ya statistics takwimu za ahadi zote za viongozi zilizotolewa kwenye majimbo mbalimbali ili tukawasaidia, tukawasaidia Wabunge hawa barabara hizo zitengenezwe. Ahadi ya Rais ni utekelezaji; kwa hiyo, ni vyema Wizara ya ujenzi ikaamua kufanya hicho kitu kuandaa takwimu zile ili kwenye bajeti hapa muweze kubeba pia viongozi wetu wa kitaifa wasionekane walivyoviahidi haviweze kutekelezeka. Zaidi ya miaka 10 ninayoizungumzia toka Mheshimiwa Pinda alipokuwa Waziri Mkuu hadi leo barabara ya Chimala, Matamba, Kitulo kilometa 51 tu, hadi leo hii haijajengwa. Kwa hiyo. niwaombe ni vyema mkaingalia barabara ile kwa jicho la ukaribu sana. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu kingine nizungumzie barabara ya kimkakati ambayo inatoka Songea inakuja Ludewa, inapita Lupila inakuja Ikonda, inakuja hadi Bulongwa kwa maana kupitia Ruvuma hii ni barabara ambayo inapita kwenye mpaka kati ya Tanzania na Malawi. Ni barabara ya kimkakati niiombe Serikali na hasa hasa nimpongeze Meneja wangu wa Mkoa wa TANROADS Injinia wetu Sharua ni mama ambaye anachapa kazi sana pale Mkoa wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana kwasababu gani, changamoto ya mvua yote tunayoizungumzia lakini barabara kama hii haijawahi kuhudumiwa mama yule anapambana na mfuko wa fedha ni mdogo kwa maana ya TANROADS lakini mama yule anapambana usiku na mchana kuhakikisha kwamba barabara hizi zinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe wizara muiangalie Mkoa wa Njombe kwa jicho la karibu miezi nane mvua zinanyesha mkoa huu barabara huwa zinafungwa takribani miezi mitatu, minne watu hawafanyi shughuli za kiuchumi na wakati sisi ni wazalishaji wakubwa wa mbao, wazalishaji wakubwa wa parachichi, wazalishaji wakubwa wa viazi vya chips ambavyo mnavitumia, mngetukumbuka ili tuweze kutumia mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili kule Makete kuna mradi mkubwa ambao unakuja wa ujenzi wa bwawa la Lumakalya, ukitoka kwenye lile bwawa kuja kuitafuta Mbeya ambako kutakuwa na power plant ni zaidi ya kilometa 200 lakini hapo hapo kwenye lile bwawa unaweza ukatengeneza barabara fupi ya kilometa angalau 17 tu ambayo toka kipindi hicho Waziri Profesa Mwandosya anaipigania barabara ya kutoka Madiyani - Lufliyo kuelekea Tukuyu ni barabara fupi sana ambayo ingeweza kusaidia hata huu mradi mkubwa wa kimkakati wa umeme ukajengwa ili iweze kusaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Ujenzi, mtusaidie barabara hizi zijengwe. Kuna sehemu nimesema viongozi wangu, hakuna heshima yoyote ile ya Ubunge, na heshima ya Ubunge wangu yoyote ile haitokani na tai au suti nzuri nilizovaa ni hii miradi kuona inatekelezwa ndio heshima yangu ya Ubunge. Heshima ya Waziri haitokani na kusoma vizuri bajeti ni utekelezaji wa bajeti hizi, watu wengi wanalalamika hapa, kuona kwenye Ilani zimo, kwenye kitabu cha Rais imo, lakini kwenye kitabu pia cha waziri mwenye imo lakini barabara hizi zinaishia kwenye makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, heshima ya bajeti kama hizi ni kuona zinatekelezwa, fedha zinatoka. Watu wametoa mawazo hapa kujenga miradi mikubwa ya zege ya matrilioni kwa own source tunaiumiza Nchi labda tuache mfumo huo twende kwenye mfumo ambayo hizi fedha za own source ziweze kusaidia kujenga barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mheshimiwa Waziri, heshima yako itatokana na utekelezaji wa Ilani, heshima yangu na Ubunge wangu 2025 utagemeaje na kwamba barabara ya kutoka Makete kwenda Kitulo hadi kufika Isyonja imetekelezwa ndio heshima ya Ubunge wangu, heshima ya Ubunge wangu sio uzuri wa tai niliyonayo ni kuona kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mambo mengi lakini barabara za Makete naamini zitakumbukwa kwenye wizara hii. Mungu abariki sana. Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)