Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Kwanza kabisa naomba niwapongeze viongozi wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi yetu ya kutengeneza barabara. Wizara hii toka tupate uhuru imefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Marehemu mama yangu aliniambia, hapo zamani wanatoka Songea walikuwa wanatembea kwa mguu wakati anakwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Loleza, wanatembea kwa mguu kutoka Songea mpaka Njombe wiki nzima, ndiyo wanapata usafiri kwenda Mbeya kusoma Sekondari ya Loleza. Ukitazama katika miaka hii, kazi kubwa imefanyika. Kwa hiyo, hatuna budi kuwapa pongezi wataalam na viongozi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika eneo ya barabara kuu zilizoingizwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 73, pamoja na barabara mbili za kimkakati Kitaifa zipo katika Mkoa wetu wa Ruvuma ambazo zipo katika Wilaya ya Namtumbo; Barabara kutoka Mtwara – Pachani - Ligela – Lusewa – Magazine - Lingusanguse hadi Narasi Wilaya ya Tunduru. Barabara ya pili ni kutoka Lumecha – Hanga – Mputa – Kitanda – Londo – Malinyi – Lupilo hadi Ifakara Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara katika barabara hii ya Mtwara – Pachani na Rasi – Tunduru ambayo ina wakazi wengi sana zaidi ya 140,000 na ina vijiji visivyopungua 39 na mitaa 10 iliyopo katika Tarafa ya Sasawala au Kata ya Lusewa. Eneo hili lina uzalishaji mkubwa sana wa mazao ya chakula na biashara na ndiyo njia ya kwenda mpakani Msumbiji pia. Kwa hiyo, strategically pia liko kiusalama ili ukihitaji kupeleka deployment kwa haraka katika maeneo ya mpakani katika eneo hilo barabara hii pia inahusika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, kwanza naishukuru Serikali, nimeona upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika. Nimeona katika hotuba ya Waziri ukurasa 41. Nawashukuru sana Serikali. Wisi wananchi wa Wilaya ya Namtumbo tunachoomba ni kufanyiwa ujenzi wa barabara hii haraka iwezekanavyo na tutashukuru sana ikianza kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara hii ya Lumecha – Londo – Malinyi – Lupilo – Ifakara Mkoani Morogoro nayo ni barabara ya kimkakati Kitaifa. Inafungua maeneo ya fursa zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro katika maeneo ya kilimo, utalii na usafiri. Barabara hii ukipitia njia ya kutoka Ruvuma kwenda Dar es Salaam kupitia Njombe mpaka Makambako na barabara hii ikikamilika inapunguza zaidi ya kilometa 350. Kwa hiyo, itaifungua na kupunguza gharama ya mafuta kwa maana ya kilometers lakini itasaidia sana kwenye maeneo ya kiutalii na pia itafungua pia mazao mbalimbali kusafirishwa na kulima katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mimi nilipata kuwa Mwenyekiti mwenza wa uratibu wa ujenzi wa ufunguzi wa barabara hii, wakati huo tunakata pori barabara hii na kujenga madaraja. Mwenyekiti mwenza mwenzangu alikuwa Mheshimiwa mzee wetu Dkt. Ngasongwa ambaye yeye alikuwa Mbunge wa Malinyi kipindi cha 2005 – 2010. Kwa hiyo, tulikuwa na Kamati ya uratibu wa barabara hii ambayo ilikuwa na Wajumbe Wakuu wa wilaya zote mbili; Ulanga na Namtumbo. Kulikuwa na Mameneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma na Morogoro, pia kulikuwa na ma-DED wa Halmashauri zinazopita barabara hii na Mkuu wa iliyokuwa Selous kwa sababu barabara hii inapita katikati ya Selous. Sasa tulikuwa tunakata miti ya Selous.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ile ilishauri na ilisimamia vizuri ujenzi wa madaraja kwa ukamilifu; Daraja la Mto Londo, Mto Mwatisi na Mto Fuluwa. Yalijengwa kwa ukamilifu na tumeifungua ile barabara, lakini Kamati ilishauri wakati ule na nilisahau Mjumbe mmoja alikuwa anatoka katika Wizara ya Ujenzi, Eng. Kilowoko. Kamati ya Uratibu wa Ufunguzi wa Barabara hii ilishauri pamoja na ufunguzi wa barabara hii, lakini TANROADS mikoa, Mameneja wa Mikoa wawe wanatenga fedha kwa ajili ya kuweka lami nyepesi katika maeneo korofi na ya miinuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, tulifanya hivyo katika eneo la Namtumbo. Tumekuwa tukiweka nusu kilometa au robo kilometa kwenye maeneo ya miinuko, yale korofi na maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki kabisa. Imesaidia sana na katika kipindi hiki naweza kutoa ushuhuda hapo nyuma katika eneo linaloitwa Kata ya Hanga kwenda mpaka Kata ya Kitanga kupitia Mputa na Naikesi, wakati wa mvua barabara ilikuwa haipitiki kabisa, lakini baada ya kufanya utaratibu huo wa kuweka lami nyepesi katika vipande vidogo tu korofi imekuwa inapitia miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, unaweza ukakuta barabara ya kilometa 120 lakini sehemu korofi haziwezi kuzidi vipande vipande vya kilometa 20. Kwa hiyo, tunaweza tukaanza kutenga fedha za kuweza lami nyepesi sehemu za miinuko nusu kilometa, sehemu hii labda kilometa moja, utakuta kwamba tunaondoa kabisa malalamiko ya wananchi, lakini pia barabara hizo zinapotika throughout the year wakati Serikali inajipanga kutengeneza barabara hizo kwa kiwango kamili cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo ushauri wangu kwamba Serikali iwe inatenga sehemu kidogo kidogo ya kuweka lami nyepesi ili barabara ziweze kupitika moja kwa moja. Kama hii tuliyoifanya sisi ya kutoka Lumecha – Hanga – Mputa – Kitanda mpaka Londo kutokea Norogoro. CCM hoyee! Ah! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye barabara ya Mtwara – Pachani…

NAIBU SPIKA: Jamani, mwacheni Mheshimiwa Vita Kawawa anawaza Uchaguzi wa Kigoma. (Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye barabara yetu hii ya Mtwara – Pachani ambayo inapita Ligela, inapita Lusewa - Magazine – Lingusanguse na mpaka Nalasi tuna mto unaoitwa Sasawala na katika kipindi hiki cha mvua mto huo daraja lake kubwa limekuwa washed away na mvua hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru TANROADS Mkoa wameenda kutuwekea kivuko tu kidogo cha kuweza watu kupita. Tunashukuru kazi ile wameifanya, lakini tunaiomba Serikali itutengee fedha ili kulikarabati lile daraja. Ndiyo daraja kubwa ambalo tunalitegemea katika Wilaya yetu ya Namtumbo na Tunduru. Naomba nikushukuru na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)