Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nitazungumzia mambo matatu. Jambo la Kwanza, mwaka 2010 wananchi waliokuwa wanaishi karibu na ile Barabara ya kutoka Geita kwenda Usagara walilipwa fidia zao, lakini wananchi kama tisa hivi wakasalia wakidai jumla ya shilingi milioni 30. Tangu mwaka 2010 mpaka leo wananchi hao wanadai milioni 30, wanaidai Serikali, haya ni mambo ya aibu, milioni 30 kudaiwa na wananchi maskini, waliowanyang’anya maeneo yao wakapitisha barabara. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hilo alichukue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kule Misungwi tuna hili Daraja la Kigongo kwenda Sengerema, daraja hili wale wakandarasi walipewa tender hiyo na sasa wanaendelea vizuri na ujenzi, lakini cha kusikitisha wamevamia milima ya wananchi wanaponda kokoto wanachukua bila utaratibu bila malipo ya aina yoyote. Mheshimiwa Rais alivyopita pale jambo hili liliibuliwa na wananchi na Mheshimiwa Rais akaagiza twende tukalishughulike. Tumekwenda kushughulika na jambo hilo tukaonyeshwa dharau ya juu, akaja Mheshimiwa Waziri tukamweleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kumjulisha kwamba tangu ameondoka hakuna kilichofanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri, yeye ndiye Waziri wa Ujenzi, anakuja pale anatoa maelekezo kwa wakandarasi aliowapa tender mwenyewe lakini bado watu hao hawafuati alichowaagiza. Hii nayo ni aibu kubwa. Nitoe ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, tupunguze sana kutoa tender hizi za ujenzi kwa wakandarasi wa Kichina wana dharau sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunashindwa kutengeneza wakandarasi wetu wenye nguvu ndani ya nchi yetu, tunashindwa nini kuwawezesha watu wetu wa ndani ili waweze kujenga barabara zetu na miradi mingine. Pale kwenye ule Mradi wa Kigongo – Busisi wale Wachina wanatengeneza, lakini hakuna mkandarasi mwenza wa Tanzania anayeangalia nini kinajengwa ili keshokutwa tujenge na sisi wenyewe madaraja yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumewaacha wale Wachina, wanajenga wanavyotaka wenyewe, wakijenga chini ya kiwango hakuna anayejua, wakiweka mawe badala ya cement hakuna anayejua, mwisho wa siku tunakabidhiwa vitu hivi vikija kuanza kuharibika hakuna anayeweza kuvikarabati mpaka tuwatafute Wachina wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kweli tupo serious, otherwise nataka nitoe mfano mmoja, waulizeni Wazambia walifanywa nini na Wachina. Waliamua kukabidhi nchi yao kwa Wachina, leo tunavyozungumza kila kitu kimekamatwa na Wachina. Sasa na sisi tunarudi kulekule, madaraja yote Wachina, barabara zote Wachina, makalvati Wachina, majengo yote Wachina, kila kona Wachina, kila mtu Mchina sasa tunafanya nini? Hivi kweli hatuna, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu pale, hivi hajafundishwa mainjia vijana wetu wa Kitanzania wanaoweza kujenga madaraja. Sasa kama hajafundisha maana yake tunapotezeana muda sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hilo Waziri aliangalie, lakini hapo hapo kwenye hilo daraja kuna vijana wetu wameomba kazi, wanaozunguka maeneo hayo, wanaoishi katika maeneo hayo, mpaka kesho hakuna hata mmoja anayepewa kazi pale. Wale Wachina wana watu wao, tunaambiwa kwamba ile kampuni ya Kichina imeingia hapo miaka ya 70 au 60 kwa hiyo wana watu wao sijui wanawatoa wapi kuja kufanya kazi pale Misungwi, lakini wale watu wa Kigongo Ferry pale hawapati kazi, hata ndogo ndogo zile hawapewi. Mheshimiwa Waziri alikuja Misungwi nikamwambia jambo hili, lakini tangu ameondoka hakuna kilichofanyika. Sasa kama ni mambo ya porojo, basi tuendelee kupiga porojo, mwisho wa siku hakuna kinachofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, nizungumzie kuhusu Shirika la Ndege. Sisi kule Mwanza unaingia kwenye mtandao unafanya booking, tunaipongeza Serikali kwa kununua ndege nyingi za kutosha, lakini unaingia unafanya booking unaambiwa ndege imejaa. Wakala anakwambia hebu subiri nikufanyie sarakasi upate tiketi ya kwenda Dar es Salaam, anafanya sarakasi yaani wakala wa tiketi naye amekuwa bosi sasa hivi, anafanya sarakasi unapata tiketi ya bahati nasibu, ukiingia kwenye ndege hakuna watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yaani tunahujumiana sisi wenyewe kwa wenyewe na huu mchezo Mheshimiwa Waziri nataka nimwambie, huu mchezo upo kwenye Wizara yake. Unafanya booking hakuna nafasi, ukiingia kwenye ndege ukibahatisha hukuti watu kwenye ndege bombardier ile inasafiri na watu 15 watu 20, lakini kwenye kutafuta unaambiwa tiketi zimejaa, tafuta usafiri mwingine. Hapa tunamkomesha nani? Ni nani tunamkomesha, tunajikaanga kwa mafuta yetu wenyewe Watanzania, ndege hizi mwisho wa siku zitakuwa ni za kupigia picha, watu wanatafuta tiketi, tiketi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo hilo, ukifanya booking kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam unaambiwa tiketi laki tano. Ukiangalia kwenye ile ndege nyingine sitaki kuitaja jina hapa unakutana na tiketi ya laki mbili, halafu ukilipa hiyo laki tano ukiingia kwenye ndege hakuna watu, kwa nini Waziri asiweke bei reasonable ili watu wengi wa kawaida wapande ndege na ndege zetu zijae. Tunamhujumu nani? Tunahujumiana sisi wenyewe Watanzania, mwisho wa siku hizi ndege zitakuwa ni ya kupigia picha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS Mwanza unaweza ukazunguka nchi nzima ukitoka Dodoma hapa utaenda vizuri, utaenda vizuri ukishaona kibao kinasema, sasa unaingia Mkoa wa Mwanza unaanza kukutana na sarakasi za mabonde, viraka, mabarabara yasiyoeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, maeneo mengine wanataka lami na sisi tunataka hayo hayo mabonde yadhibitiwe TANROADS Mwanza kuna shida gani? Kwa nini ukifika Mwanza tu ndio unakutana na mabonde kuinama unaingia kwenye majaluba mule mule kwenye lami kuna majaluba mule mule kuna matuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hebu iangalie vizuri Mwanza kuna shida gani Mwanza ni mkoa mkubwa huo ndio ukweli, haya mabonde mabonde ni aibu tunatiana aibu. Kama hatuwezi kutengeneza barabara basi tuseme hatuwezi kutengeneza barabara, lakini sio kila siku tunaziba viraka mara kiraka hiki kimepasuka hapa, mara kinazibwa hapa. Hizo gharama mara mia tano zikatengeneze mabarabara mapya huko Kusini kama hamuwezi, kwa sababu imeonekana kama ni deal. Kila mwaka mnatengeneza mabarabara hii ni deal ya watu kila siku mnaziba viraka, kwa sababu ya deal kila siku deal. Pale Wilayani kwangu Misungwi kuna kilometa karibia 20 kila mwaka TANROADS wanatengeneza barabara kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu naona huu ni usanii na tunaiba pesa za watu. Jambo la mwisho limesemwa hapa kwamba, daraja la Busisi lisiendelee kujengwa mpaka ipatikane certificate ya mazingira. Yaani unaaga kwa mumeo kwamba nakwenda kazini kuja kusema kitu kama hicho kwamba, daraja lisijengwe eti kwa sababu hakuna certificate ya mazingira! Sisi tunasema hivi mazingira ni ya kwetu, daraja ni la kwetu, ziwa ni la kwetu, kila kitu ni cha kwetu tunahitaji daraja lijengwe na kwa wakati na likamilike na tunahitaji kwa muda mfupi. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)