Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi. Niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote kwa kutuletea bajeti nzuri, lakini ombi langu tuweze kuweka nguvu katika kutafuta fedha ili mipango hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza, nimeiona barabara ya Tengeru – Moshi – Himo ipo kwenye bajeti ambayo inasababisha msongamano mkubwa sana pale Moshi. Pia nimeuona Uwanja wa Ndege wa Moshi ambao ni muhimu sana katika utalii na biashara, niwapongeze sana Wizara. Vilevile katika bajeti nimeona barabara za Chuo cha Polisi au Shule ya Polisi Moshi, nipongeze sana na kushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ni kuhusu barabara kuu hizi zinazojengwa na TANROADS, haswa barabara ya Moshi – Arusha, katika maeneo mengi haziwi na mitaro. Sasa maji yale ambayo wanayajengea makalvati na madaraja na kwa sababu ya nature ya Mkoa wetu wa Kilimanjaro na Manispaa ya Moshi huwa ni mteremko, kuna Kata za Ng’ambo, Msaranga, Mji Mpya na Miembeni zinaathirika sana na maji haya ambayo yametengenezewa makalvati lakini hayajawekewa mitaro kuyaelekeza katika mito. Niombe sana Serikali iangalie uwezekano wa kutengeneza mitaro ili maji haya yasiendelee kuleta maafa kwenye makazi ya watu (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara ambayo kwa muda mrefu tumeiombea upgrade na tulishaipanua na tayari watu walishavunja nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara hiyo. Barabara hiyo ni ya Sokoine ambayo inaanzia katika roundabout ya YMCA kwenda mpaka KCMC inaenda kuungana na barabara ya Mwika. Barabara ile inaunganisha barabara mbili za TANROADS, kwa sababu tulishaiombea ije TANROADS ili iweze kuunganishwa na kupanuliwa basi tunaomba tafadhali sana Serikali iangalie umuhimu wa kui- upgrade barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ambayo haipo moja kwa moja kwenye Jimbo langu lakini ni ya muhimu sana kwenye Jimbo la Moshi Mjini. Barabara ya TPC – Mabogini – Kahe na baadaye itaenda kuungana mpaka Chekereni. Barabara hii ina umuhimu kwanza kwa sababu ndiyo inayoleta chakula katika eneo la mjini, lakini pia hatuna maeneo kwa ajili ya bypass. Barabara hii ikiweza kutengenezwa inaweza kutusaidia ili iwe ndiyo bypass kwa ajili ya kuhamisha malori na kuondoa msongamano mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara iliyokuwa ya Arusha ya zamani inaitwa Old Arusha Road barabara hiyo ilikuwa ya TANROADS lakini baada ya TANROADS kuhamisha barabara kupeleka kwenye barabara hii mpya ya Arusha barabara ile imetekelezwa, lakini ina umuhimu sana iwapo lolote linatokea kwenye barabara kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuitengeneza barabara ya Old Arusha Road ambayo inaanzia Moshi inakwenda Moshi Vijijini mpaka Jimbo la Hai. Barabara hii inaumuhimu sana katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisimalize bila kuongelea kidogo kuhusu TARURA ambayo ni sehemu ya bajeti hii. Tunayo matatizo mengi sana katika maeneo yetu na yalizungumziwa sana. Lipo lile suala la kupata fedha, mimi niendelee kusisitiza ni muhimu sana TARURA waongezewe fedha ili angalau waweze kusimamia barabara za mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uzoefu wangu wakati fedha hizi zilipokuwa zinaletwa, halmashauri tulikuwa tunanunua mitambo, magreda na mashindilia kwa hiyo gharama za kurekebisha barabara haswa hizi ambazo siyo za lami inakuwa ni rahisi. Nitoe ushauri TARURA wawezeshwe kununua mitambo ili kazi iwe rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)