Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja ya Wizara yetu ya Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza michango mingi sana ya Waheshimiwa Wabunge ambayo ni mizuri sana. Moja katika mambo ambayo ni muhimu sana huko tunakokwenda ni suala zima la barabara zetu. Katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi barabara ambazo zipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 nadhani hizo zipewe kipaumbele namba moja na barabara ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na zenyewe ziwe katika vipaumbe vya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Jimbo la Swola kuna barabara inayotoka Manawa - Misasi - Swola - Mwakitolyo - Kahama imefanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2010 na ilikuwa ndani ya Mpango wa Millenium Challenge Funds. Baada ya zile fedha kuondoka barabara hii imesahaulika mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa barabara hii inaunganisha Majimbo ya Mwanza Mjini, Misungwi, Solwa na Msalala kwa maana ya Jimbo la Kahama. Majimbo matano au sita yanaunganishwa na barabara moja hii. Wafanyabiashara wa Rwanda, Burundi na nchi zote jirani huwa wanakuja mpaka Solwa na Nyabukande kwa ajili ya biashara ya mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni ya Solwa - Old Shinyanga na yenyewe imo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi yenye urefu wa kilometa 60. Mimi nipo kwenye Kamati ya Miundombinu na nilimueleza Waziri jambo hili, tupo pamoja sana katika utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwenye hotuba ya Waziri nimeona airport ya Shinyanga Ibadakuli, zimewekwa shilingi bilioni 3.6. Mwaka huu airport ya Shinyanga inakwenda kujengwa baada ya kuilalamikia kwa muda mrefu. Naishukuru sana Serikali kwa kutusikiliza awamu hii. Sasa hivi wananchi wa Shinyanga watakuwa hawaendi tena Mwanza baada ya kukamilika airport hii tutakuwa tunapandia hapo hapo Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongelee suala zima la bandari. Tanzania hii kuna bandari 89 lakini 66 zipo kwa mujibu wa Sheria Na.17 ya mwaka 2004 na zinasimamiwa na Wizara moja kwa moja. Kati ya bandari hizi, bandari 12 zipo kwenye Bahari ya Hindi, bandari 24 zipo Ziwa Victoria, bandari 19 zipo Ziwa Tanganyika, bandari 11 zipo Ziwa Nyasa na kuna bandari nyingine ndogo ndogo. Bandari ni kitu kikubwa sana, Bandari ya Dar es Salaam inachangia kwenye Pato la Taifa zaidi ya asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua tani milioni 9 alizosema Mheshimiwa Waziri, ukatoa mizigo ya transit ukaacha mizigo ya ndani, kodi ya bidhaa ni zaidi ya kontena laki moja na elfu arobaini mpaka kontena laki moja na elfu sitini ni 2.5 trillion to 3 trillion per year bandari peke yake inaisaidia TRA kukusanya mapato ya nchi. Kwa hiyo, bandari siyo jambo la mzaha mzaha hivi, ni jambo kubwa lakini ipo kama idara ndani ya Wizara ya Uchukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua Bandari ya Durban wanahudumia tani milioni 31, Bandari ya Beira wanahudumia tani milioni 7 na target yao ni kwenda tani milioni 11 kwa mwaka, ukichukua Bandari ya Mombasa wanahudumia tani milioni 12 kwa mwaka na hizi bandari ni washindani wakubwa sana wa Bandari yetu ya Dar es Salaam. Nakumbuka wakati ule tuliongea sana hapa ilikuwa kuna tatizo kubwa sana tuliingiza sheria ya kutoza VAT on auxiliary goods kwa maana ya transit ikatusababishia matatizo makubwa mno nchi jirani wote wakaondoka wakaenda kutumia Bandari ya Mombasa. Tulipoongea hapa Serikali yetu ilikuwa sikivu ikaondoa na sasa hivi wateja kutoka Rwanda na Zaire wamerudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nataka kumalizia, naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu afikirie bandari iwe Wizara kamili ili tuweze kutoka kwenye milioni 9 twende kwenye milioni 12, 15 mpaka 20 ili iweze kuchangia kwenye asilimia zaidi ya hamsini ya Pato la Taifa. Bandari siyo jambo dogo, Singapore asilimia 80 ya mapato yao yanatoka kwenye bandari.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)


NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza umeniongezea dakika moja ungenipa dakika mbili ningeshukuru sana. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)