Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GOWDIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, pia, niipongeze Wizara kuanzia Waziri mwenyewe mwenye dhamana ya Wizara na Manaibu wake lakini pia na Chief Executive wa TANROADS mzee wetu Mfugale. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Kwa Mkoa wangu wa Morogoro pale Meneja wa TANROADS Mkoa Mhandisi Ntije, Mheshimiwa Waziri ikikupendeza aendelee kubaki na sisi Wanamorogoro tunamuhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepongeza Wizara kwa lengo kuu moja kwa sababu nimeona ukiangalia bajeti ya Waziri aliyowasilisha imeelezwa tunakwenda kuanza ujenzi wa barabara sasa ya kiwango cha lami ya kilometa 50 kutoka Ifakara kwenda Mlimba – Kihansi. Tumetengewa kwenye bajeti bilioni 7. Ukifanya hesabu ya kawaida unaona kama kuna kilometa saba au nane hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini itoshe kusema kilometa 50 kwa bilioni 7 kwa kweli Waziri hebu tafakari tuone namna gani tunaweza kufanya ili wananchi wa Mlimba waone wanakwenda kupata barabara hii kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nimeona kwenye hotuba yake tunakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu wa kilometa 220. Barabara hii inaitwa Morogoro – Njombe – Boda yenye urefu wa kilometa takriban 220, hilo ni jambo jema na sisi tunataka kusema tu kwamba wana Mlimba wamesikia hakika tunaipongeza Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kuhusu upembuzi wa yakinifu wa barabara hii ya kilometa 220 ya Kihansi – Mlimba – Taweta – Madeke. Tangazo la kutafuta mkandarasi mshauri lilifanyika miezi mitatu iliyopita. Kwa hiyo, unavyokuja kuhitimisha bajeti yako jieleze tu ni lini sasa kazi hii ya upembuzi yakinifu inakwenda kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ni suala zima la reli yetu ya TAZARA, ni mdau wa reli ile kwa sababu inapita Jimboni kwangu. Inaunganisha Dar es Salaam mpaka kule kwako Mbeya. Tumekuwa na vituo vidogo vinaitwa Hot stations na wananchi wa Mlimba ni wadau wazuri kwa sababu ni biashara na wanakuwa wanasafiri na watu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hot station inaitwa Chisano hot station, mpaka leo walifunga. Mheshimiwa Waizri, unavyokuja kuhitimsha bajeti, tusaidie ni lini wananchi wangu wa Tisano kata ya Tisano wanakwenda kupata Hot station hii ili nisishike shilingi yako na nitakusudia kushika shilingi kwa sababu hot station ni jambo la kuamua tu na ni biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe hot station zote kwenye reli hii ziboreshwe kwa sababu wananchi hawa wanaotumia reli hii ya TAZARA wakati wa mvua wananyeshewa na mvua kwa sababu wanakwenda wanasimama tu njiani wanasubiri treni. Lakini jua likiwaka, wanawakiwa na jua. Kwa hiyo, kwa sababu ni biashara, kujenga mahusiano mazuri na wadau hawa wa hii reli ya TAZARA ni muhimu sasa Wizara muelekeze TAZARA wajenge vituo hivi vidogo kuboresha mazingira walau nyakati za mvua waweze kujistiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema tutafakari kwa kina ni namna gani tumegawanya miundombinu ya barabara Kitaifa. Leo hii kuna wenzetu wengine wanajadili barabara za Kata na Kata lakini kuna Watanzania hawafahamu tunavyozungumzia tumejenga barabara za lami Watanzania hawaijui lugha hii. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali, hebu kipaumbele kianze kuunganisha mikoa yetu yote tumalize, twende kwenye wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wenye barabara za kutosha mpeleke fedha za maintenance, sisi wengine tujengewe barabara kwa sababu wananchi wa Mlimba hii barabara ya Morogoro – Njombe – Boda ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Njombe. Nadhani ipewe kipaumbele cha kwanza halafu wengine wafuatie kwa sababu nchi ni moja, walipa kodi ni Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii maeneo mengine sitaki kuyataja, kuna Mbunge mmoja alikuwa anzungumza hapa anajadili barabara kitongoji na kitongoji, jamani nchi hii ni ya kwetu sote! Nchi ya Watanzania wote, wale ambao wameshajengewa barabara wakarabatiwe zile zilizojengwa ndiyo zijengwe mpya, hatuwatendei haki Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wasiwasi wangu kule kwenye Wizara tuwatazame wale wataalam wetu. Nina wasiwasi wanatoka mikoa fulani. Kwa hiyo, wanavyoandaa bajeti wanaandaa kwa makusudi ya kuangalia kwao wanakotoka, hii sio sawa sawa. Mheshimiwa Waziri katika hili naomba mkatafakari kwa kina, mchunguze hata kuangalia ukabila kabila kidogo. Samahani sisemi ukabila…[Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
NAIBU SPIKA: Hayo ondoa sasa hivi. Ondoa tu sasa hivi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: … sizungumzii hiyo, sisemi hiyo....
NAIBU SPIKA: Ah! Wewe yafute ili yasiwepo kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiondoe hiyo. Ninachotaka kusema ni kwamba watafakari kwa kina katika uandaaji wa bajeti tunazingatia vigezo gani? Yamkini kuna mambo fulani ambayo sisi wengine tunaamini ah! Sitaki kuendelea kusema maana nitaharibu huu mchango wangu. Itoshe tu kusema kwamba nashauri Serikali tujikite kwenye vipaumbele hasa barabara zinazounganisha mikoa na mikoa, twende kwenye wilaya. Tumalize kwanza hizi! Mkoa wa Morogoro unaunganishwa na Mkoa wa Njombe, Mkoa wa Morogoro unaungana na Mkoa wa Songea. Tukamilishe kwanza barabara hizi. Ahsante. (Makofi)