Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kushukuru na kuwapongeza sana Wizara ya Ujenzi kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya. Niwapongeze sana kwa mara ya kwanza kabisa barabara yetu ya kutoka Nata – Mugumu sasa imeingizwa katika ujenzi kwa kiwango cha lami, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunawashukuru kwa ajili ya kuonesha mpango wa kuanza kujenga barabara ya lami kutokea Tarime kuja Mugumu. Vilevile nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza TANROADS Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuiomba sana Wizara ya Ujenzi kutoa kipaumbele na commitment ya kutosha katika barabara ya Makutano – Nata - Mugumu. Barabara hii ni ya muda mrefu sana, imeanza kulimwa toka mwaka 2013 tayari kulipelekwa pale makampuni ambayo ilikuwa ni joint venture ya makampuni kumi. Ujenzi wake umeanza lakini umeendelea kusuasua sana, sasa hivi ni takribani miaka kumi barabara ile haikamiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia hata pesa ambazo zimekuwa zikiendelea kutolewa bado haituridhishi kama kuna commitment ya kutosha, hakuna priority katika barabara ile. Ukiangalia mwaka 2014/2015 kulitengwa shilingi bilioni 5.6 tu, 2015/2016 kukatengwa shilingi bilioni 2.2, mwaka 2016/2017 kukatengwa shilingi bilioni 12, mwaka 2017/2018 shilingi bilioni 9 na ukiendelea bado bajeti ile imeendelea kupungua kutoka shilingi bilioni 12 mpaka bajeti ya mwaka huu 2021/2022 kumetengwa shilingi bilioni sita tu, barabara ya kilometa 125.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ikumbuke barabara hii ya Makutano – Nata – Mugumu ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha. Barabara hii kwa mujibu wa Mpango na Dira ya Maendeleo ya nchi yetu tulikuwa tumejiwekea kwamba lazima kipaumbele kitolewe kuunganisha barabara zote za mikoa. Sasa barabara hii ya kuunganisha Mkoa wa Mara pamoja na Mkoa wa Arusha bado haijajengwa lakini barabara za mikoa mingine tayari wamejenga. Tunaomba sana Wizara iongeze commitment kubwa ya fedha katika barabara hii ili kuhakikiisha kwamba sasa inakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna mkandarasi yuko pale sasa hivi lakini kuna shida ya menejimenti. Mimi nimewatembelea mwezi huu wa tano mwanzoni, pesa imetolewa tofauti na sehemu zingine pale watu wale bado hawajaanza kupambana kuhakikisha kwamba wanajenga barabara ile. Niombe sana Wizara muweze kupita pale na kusimamia mradi ule kwa karibu sana ili uweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile wameanza kuilima lakini bado fidia haijatolewa. Niombe sana Wizara iende kuhakikisha kwamba fidia zinatolewa na watu wale wanaweza kupata nafasi tena ya kuchukua maeneo mengine wafanye kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Uwanja wa Ndege wa Serengeti sasa uingizwe katika upembuzi yakinifu. Pia naiomba Wizara hii, kuna barabara ambazo zinapaswa kufanyiwa review tena ziingiwe katika barabara za TANROADS; tayari Wabunge wengi wamelalamika kwamba fedha haitosheleza katika TARURA, sasa ni vema tupeleke barabara nyingine zinazoweza kufaa kutokana na umuhimu wake katika uchumi, ziingizwe katika barabara za TANROADS. Katika Jimbo langu, barabara ya Mesaga – Masinki; barabara ya Mugumu - Mbalibali mpaka Machocho mpaka Nyansurura ni muhimu sasa ziingie kuwa barabara za TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara inayotoka Musoma kwenda makutano ya Nyakanga mpaka Rung’abure, ujenzi wake wa lami unasuasua. Mheshimiwa Waziri tunashindwa kuelewa kuna mpango gani pale? Mbona barabara ile inajengwa kidogo kidogo sana na barabara ile inaunganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Mji wa Musoma ambao ni Makao Makuu ya Mkoa? Tunaomba barabara ile iongezewe fedha ili ikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba kuwepo na msukumo mkubwa wa ujenzi wa barabara hizi. Pia namwomba sana Waziri pamoja na Wizara yote kwa ujumla, waangalie sasa uwezekano wa kuzifanyia upembuzi yakinifu barabara mpya ambazo zina umuhimu mkubwa sana kiuchumi ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara inayotoka Nyansurura ikipita Majimoto mpaka Iramba mpaka Sorisimba ni muhimu sasa ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)