Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Kwa sababu dakika tano ni chache, napenda niseme yaliyomo ndani ya moyo wangu, bajeti hii haikugusa kabisa maeneo ya Nyang’hwale hata sehemu moja. Kuna ahadi za Viongozi Wakuu kuanzia Mheshimiwa Rais Kikwete alikuja 2010 akatuahidi Barabara ya kutoka Kahama - Nyangh’wale kwenda Busisi itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 Mheshimiwa Jakaya alikuja kwa mara nyingine akatuahidi vile vile. Mwaka 2015 mgombea mwenza ambaye sasa hivi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan alikuja kwenye kampeni na akatuahidi kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka 2015, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye kampeni zake alipokuja, alituahidi ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu kuanzia mwaka 2010 mpaka leo hii 2021 haijawahi kuwekwa ndani ya mpango hata siku moja, hata bajeti hii nimeangalia hakuna mpango wowote ambao umewekwa ujenzi wa lami wa barabara hiyo. Wakati barabara hiyo inaunganisha Mikoa mitatu Shinyanga Geita na Mwanza. Barabara hiyo itafungua uchumi wa Nyang’hwale kwa sababu Daraja letu la kutoka Busisi - Kigongo Feri litakapokuwa liko tayari, kutoka Busisi kwenda Kahama ni kilometa chache sana kuliko kuzunguka Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nasema kama mwakilishi wa Jimbo la Nyang’hwale, kwa kweli sijaridhika, naomba bajeti hii tuwaondoshe hawa Mheshimiwa Waziri na timu yake ikajipange upya. Kwa sababu kila Mbunge amesimama hapa anamlalamikia Mheshimiwa Waziri na Wizara yake hakuna hata Mbunge mmoja aliyeridhishwa na bajeti hii. Kwa hiyo naomba nitoe hoja, Wabunge wenzangu mniunge mkono, Wizara hii iweze kuondoka wakajipange upya Wizara hii

Waheshimiwa Wabunge, naomba mniunge mkono. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Mheshimiwa Amar kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Gwajima.

MHE. ASK. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nimpe taarifa ndugu yangu na rafiki yangu kwamba Urais siyo mtu Urais ni taasisi. Anapoahidi Rais imeahidi taasisi ya Urais, kwa hiyo namshauri kwamba kama vile mimi nilivyoahidiwa pale Wazo, Mheshimiwa Rais alipopita pale akaahidi bilioni tano kwa ajili ya mafuriko, naamini Taasisi ya Urais itayatimiza hayo kwa hiyo namtaarifu avute subira tutatimiziwa tu nampa taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa yake Mheshimiwa siwezi kuipokea kwa sababu wananchi wangu hawatanielewa, niunge ama niache, ninachoomba ni kwamba mniunge mkono Wizara hii ikajipange upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, wamevunja kanuni.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mmeeleweka. Mheshimiwa Amar malizia mchango wako. Ngoja kwanza Mheshimiwa Amar nifafanue jambo moja, maana, ngoja kidogo.

Waheshimwia Wabunge, naona mmesimama hapa kwa wingi baada ya kusikia neno Mheshimiwa Amar alikuwa anasema anataka kutoa hoja ili Bunge limtume Mheshimiwa Waziri akajipange upya ndo aje humu ndani. (Makofi)

Sasa Waheshimiwa Wabunge taratibu tulizojiwekea sisi wenyewe haziruhusu hiki ambacho anasema Mheshimiwa Amar. Kwa hiyo malizia mchango wako Mheshimiwa.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika…

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Charles Mwijage.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji na wengine wote waliozungumza kama yeye, kwamba sisi Wabunge tunapaswa tunapochangia tumweleze Waziri na Serikali kwamba hizo pesa za barabara zote wakazipate wapi, kwamba Serikali sasa ingeamua iende ikope tujenge barabara halafu sisi tutalipa na watoto wetu hata kama ceiling itazidi. Naomba kumpa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana nilimpa fursa amalizie muda wake mjadala anaousema Mheshimiwa Mwijage yuko sahihi, lakini siyo katika mjadala ngazi hii, siyo mjadala wa ngazi hii. Ngazi zinazofuata hapo baadaye Waheshimiwa Wabunge yale aliyoyasema Mheshimiwa Mwijage tutaweza kuyatumia huko mbele. Kwa hiyo tuanze kutafakari wale Wabunge ambao wanatamani mambo yabadilike kutokana na haya yaliyowekwa humu basi waanze kutafakari namna ya kuishauri Serikali ipate wapi hizo fedha, lakini siyo kwenye mjadala wa ngazi hii ambapo tunajadili bajeti za kisekta. Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, hata wewe jana umelalamika sana jimboni kwako na wengine wote tunalalamika hivyo hivyo, lakini pia tukumbuke kwamba tunapowakusanya wananchi na kuwaeleza mipango ya Chama na Serikali itafanya nini mtakapotupa ridhaa, ni haya sasa ya kuwatengenezea yale ambayo tuliwaahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mimi kama Mbunge mwakilishi, kazi za Mbunge ni tatu; kuishauri Serikali, kuisimamia Serikali pamoja na kutunga sheria. Sasa leo hii mimi kama mwakilishi wa Jimbo nakuja hapa nakaa naunga tu mkono wananielewaje mimi wale kule?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tuelewane vizuri, nitaruhusu hii taarifa lakini Mbunge atakayesimama kwenye taarifa asiwe anachangia kwamba na Jimboni kwangu kunafanana na wewe, awe anampa huyo taarifa juu ya kile anachokichangia.

Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji kwamba barabara hii ya Busisi - Nyang’hwale Kahama haina umuhimu tu kwenye Jimbo la Nyang’hwale isipokuwa ina umuhimu mkubwa sana katika Jimbo langu katika Kata ya Chela, Kata ya…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hayo ndiyo niliyokuwa nayasema sasa, yaani Mbunge hujapata nafasi ya kuchangia unataka utumie kwenye taarifa kuchangia. Sasa kuanzia sasa hivi nitakuwa nawakata tu, Mheshimiwa Iddi kaa chini. Kuanzia sasa hivi ukisimama ukataka kuchangia unamkosea yule anayechangia kwa sababu kwenye Taarifa Rasmi za Bunge zitaonekana ulimpa taarifa halafu unazungumzia mambo ya kwako wewe, tafuteni fursa ya kuchangia Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2010 nilipata kura nyingi sana na Chama na Kiongozi Mkuu wa nchi alipata kura nyingi sana. Mwaka 2015 hivyo hivyo, 2020 hivyo hivyo kwa imani kubwa ya kwamba tutawatengenezea barabara wananchi hawa. Mwaka 2025 nitaenda kusimama niseme nini, lakini pia Wabunge wote wamelalamika kwa nini wasitoke wakajipange upya?

Mheshimiwa Naibu Spika, hii si mara ya kwanza mimi ni awamu yangu ya tatu, tuliwahi kuiondosha Wizara ya Maji ikaenda ikajipanga upya, leo hawa vipi? Wabunge wote wamelalamika, mimi sina hata kilomita moja leo miaka 12, nitawaeleza nini wananchi. Naomba sasa kwamba Mheshimiwa Waziri safari hii sijui niunge mkono, sijui namna gani, lakini akajipange upya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.