Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri na watendaji wake kwa hotuba nzuri ambayo ameisoma. Kwa mara ya kwanza Tanzania imeweza kuuza dhahabu nje yenye thamani ya dola bilioni tatu na mauzo ya thamani ya dola bilioni tatu ya dhahabu sehemu kubwa zaidi ya 60% karibu 70 ya dhahabu hii, inatoka kwenye Jimbo la Geita Mjini kwenye mgodi wa Geita Gold Mine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili mauzo kama haya ya dola bilioni tatu yaweze kuendelea lazima uchimbaji wa madini ambao kuna mgodi mkubwa kule wa Barrick na mgodi mkubwa wa GGM uwe supported na miundombinu ambayo tumekuwa tukiizungumza. Sasa iko Barabara ya kutoka Geita kwenda Kahama ambayo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amesema ameiweka kwenye mpango wa kuijenga, lakini ametenga bilioni sita kilomita karibu 140. Ni barabara muhimu sana katika mchango wa uzalishaji huu wa dhahabu lakini katika mawasiliano kwa sababu hii ndiyo barabara inayounganisha Mkoa wa Geita pamoja na Mji wa Kahama ambapo magari makubwa yote ya mizigo mikubwa yanayokwenda kwenye Mgodi wa GGM na Mgodi wa Barrick yanapita kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iliombwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na Mbunge anaitwa Mheshimiwa Mabina. Alikaa miaka yake 10 akaondoka, akaja mwenzangu marehemu Donald Max naye akaiomba naye akaondoka, nilikuja mimi mwaka 2015 nimeiomba sasa mwaka 2021 kuna dalili za kuanza kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni maoni yangu kwa Mheshimiwa Waziri barabara hii ina umuhimu mkubwa sana, siyo tu mkubwa kama ambavyo watu wengine wanafikiria, ni kwa sababu ni strategic, hii barabara ina umuhimu mkubwa kutokana na mizigo mikubwa ambayo inapita kwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa GGM, kwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Kakola, lakini kuna Mgodi mwingine mkubwa wa Dhahabu wa Nyanzaga ambao unaanza Sengerema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitisha malori makubwa yenye mitambo mikubwa ukayapitisha kwenye daraja linalojengwa hili daraja halitadumu, ndiyo maana Wabunge wote waliotangulia waliomba barabara hii ya Geita kupitia Kakola kwenda Kahama iweze kujengwa, na ni barabara
ambayo mchango wake kwenye uchumi unaonekana wazi, kama leo tumefikisha dola bilioni tatu. Mwanzo nchi hii mapato makubwa ya forex yalikuwa kwenye utalii, sasa hivi mapato makubwa ya forex yako kwenye dhahabu. Dhahabu kama ndiyo madini tunayoyategemea, matarajio yangu ni kwamba barabara hii itapewa umuhimu mkubwa, tutaweka pesa za kutosha siyo bilioni sita ambazo zimewekwa sasa hivi ambazo naona ni kama vile bado tunafanya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, jana Mheshimiwa Mbunge mmoja alizungumza kuhusu performance ya ATCL na akasema unaweza kwenda kukata tiketi ukaambiwa ndege imejaa, lakini baadaye ukiingia kwenye ndege ukashangaa ukakuta ndege iko nusu. Sasa jambo hili linafanana kidogo na jambo hili. Tumejenga Uwanja wa Ndege wa Chato, wananchi wanataka kuutumia uwanja huo, lakini ili uweze kutoka pale kwenye uwanja wa ndege kwenda Katoro kwenda Chato kwenda Biharamulo kwenda Geita ni lazima kwenye mipango ya Wizara wakati wanajenga uwanja ule wangefikiria jambo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kwenda China tulipelekwa na Bunge, tukateremka kwenye Uwanja wa Ndege wa Fuzhou, kutoka uwanja wa ndege huu kwenda kwenye mji tunaopelekwa ilikuwa ni kilometa 120, lakini facility zimetengenezwa na wenye uwanja, kuna mabasi pale ya kupeleka wale watu. Sasa mtu anajiuliza nikate tiketi ya laki sita kwenda nikatue Chato, halafu nitafute gari ya kunitoa kilometa 110 kunipeleka Geita au kilometa 100 kunipeleka Chato, haiwezekani! Sasa lazima Wizara ije na mpango wawe na airport shuttle ambazo ni za kwao, ambazo zitarahisisha watu wanaopanda ndege kwenda kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ndege zetu zina bei kubwa sana sababu ni nini? Ndiyo maana haziwezi ku-perform. Bei ya ndege ni sawa na kwenda Dubai. Sasa kwanini tusitengeneze bei ambazo zinafanana na network na nchi yetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)