Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Naibu Spika, sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika Wizara hii japo nimeona malalamiko mengi sana ya Wabunge kuhusu suala la barabara na kuna uwezekano mkubwa sana Serikali ikawa haina bajeti kubwa kwa ajili ya barabara lakini inawezekana pia ikawa hawajajipanga vizuri kwenye mgawanyo kwa ajili ya barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara za upande wa jimbo langu; kuna barabara ya kutoka Ifakara - Ulanga kujengwa kwa kiwango cha lami, imekuwa bingwa kuongoza kutajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu lakini mpaka leo hii sijaona hata kilometa moja ambayo imetengewa barabara ile ili wananchi wangu wa Ulanga waweze kupata barabara ya lami. Hata kama ni kwa kilometa chache basi mgawanyo ule ungezingatia kidogo kuona kwamba watu wengi wana uhitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mbunge mwenzangu jana alitaka kuruka sarakasi hapa kuona kwamba kuna mtu ana lami anaomba bajeti ya kurekebishiwa lami yake wakati sisi wengine hatuna lami na hatujawahi hata kuiona. Sijui huwa wanatumia vigezo gani, kiukweli inaumiza sana.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja na special case kabisa, kwenye jimbo langu kuna daraja liko kwenye Kijiji cha Ikangao ambayo inaunganisha Kata mbili za Ilonga na Ketakeli. Daraja lile limekatika na linahudumia zaidi ya watu 28,000 na wanafanya shughuli za maendeleo ikiwemo ni pamoja na kilimo. Watu wale mwaka jana walilima ufuta walikuwa wanauza Sh.3,000 kwa kilo, baada ya daraja lile kukatika wakawa wanauza ufuta kwa shilingi 1,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia suala la kilimo ni lazima tujue kwamba bila barabara hakuna kilimo ambacho kitaenda kwa sababu mazao yale hayawezi kufika sokoni kabisa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri mara Bunge litakapoisha nifanye naye ziara kwenye jimbo langu kwa sababu jimbo lile limesahaulika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri yupo hapa, naomba daraja hili liende likajengwe, mimi sitaki kujua fedha zitatoka TARURA au TANROADS.

Naomba wananchi wangu wakajengewe daraja hili kwa sababu lisipojengwa tena mwaka huu ina maana biashara zitakuwa zimekufa na wale wananchi mwaka ujao inawezekana wasilime kabisa kwa sababu hawana wanakoweza kupeleka bidhaa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tutaendeleza sana kudumaza uchumi wa nchi hii kama hatutazingatia suala la barabara. Barabara ni muhimu sana, huwezi kuzungumzia viwanda kama hujazungumiza barabara, huwezi kuzungumzia kilimo kama hujazungumzia barabara. Kwa hiyo, mimi niwaombe sana, inawezekana kweli Wabunge wengi wamelalamikia suala la barabara, kuna uwezekano kwamba mkatakiwa kwenda kujipanga vizuri lakini pia hata kama mkienda kujipanga naomba sana daraja hili lipewe kipaumbele ili wananchi hawa waweze kuendelea shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madaraja mengine ambapo wananchi tumejipanga kwenda kufanya kazi wenyewe kujenga daraja lile kwa sababu watu wanakufa kwa ajili ya kuliwa na mamba. Tumesema tutaenda kufanya kazi na wananchi wangu kwa kuweka hata daraja la mbao ili waweze kuendelea na shughuli zao lakini hili ni daraja kubwa sana ambalo linaunganisha watu wengi sana. Hawa nimezungumzia wananchi wachache 28,000 kutoka kwenye hizi kata mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)