Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia na hasa kupata nafasi ya kuzungumza baada ya Mheshimiwa Mchafu kuzungumza ili tu uniruhusu nimpe kataarifa kidogo kwamba tutakapocheza Simba na Arsenal tutawafunga sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri lakini niipongeze zaidi Kamati kwa sababu wasilisho lao limesaidia hata uchangiaji wetu kwenda vizuri. Wamefanya kazi nzuri sana. Amesema mambo mazuri sana katika hoja ya Wizara hii. Nizungumze machache sana nikianzia hasa yanayohusiana na Jimbo langu la Mwanga. Sehemu ya ninachotaka kuzungumza, kimeguswa juu ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mwanga lina Kata 20 na katika hizo, Kata 6 ziko kwenye maeneo ya mipakani na pengine kwa kumbukumbu nikizitaja tu. Kuna Kata ya Kileo, Kivisini, Jipe, Kigonigoni, Kwakoa na Kata ya Toloha. Zaidi ya nusu ya maeneo haya ukiingia na simu yako ya mkono kuna mahali unafika unaambiwa karibu Safaricom, sasa Safaricom na haya ma-bundle ya vijana wetu akifika kule hapati mawasiliano. Ni kijana wa bodaboda alikuwa kule, mteja wake anamtafuta hampati, wanapoteza income. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wenzetu wa TCRA wanapotoa leseni pia wana jukumu la kufuatilia mambo ya udhibiti ubora. Wasiachie haya makampuni yanawekeza kule halafu hawajali juu ya ubora wa huduma zao wanazozitoa kule wanaendelea kutuumiza. Hili jambo nashukuru kwamba Mheshimiwa Ndugulile alishaanza kunong’ona na sisi Wabunge ambao tunatoka kwenye maeneo ya mipaka naamini kabisa kwamba atalitilia mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko kata nyingine ya Mlimani ambayo kuna mnara wa Halotel lakini ule mnara unatumia solar, sasa kule kwetu ni kama Uswisi. Wakati mwingine hatuoni jua kutwa nzima. Kwa hiyo, siku kama hakuna jua basi na mawasiliano hakuna. Mimi sidhani kampuni kubwa kama ile inasubiri umeme wa REA, wavute nguzo ziende pale ili mawasiliano yaweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tu baada ya hapo nije tu kwenye hoja moja ya Kitaifa ya TTCL ambayo imezungumzwa sana na ninasema hivyo kwa sababu ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ukurasa wa 96 imezungumzia juu ya kuwekeza kwenye shirika hili la mawasiliano. Shirika hili tunapozungumzia juu ya kulifufua, kupata National Telecom, nafikiri ni sawasawa na tulipokuwa tukizungumzia habari ya kupata National Carrier ATCL, kwamba ni jambo la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika nchi nyingi, mashirika haya, hizi National Telecoms ni mashirika makubwa sana ukianzia Egypt Telecom ni shirika kubwa tu, ukienda BOTNET Botswana ni shirika kubwa, China Telecom ndiyo usiseme na Ethio Telecom ya Ethiopia, turnover yake kwa taarifa za 2020 ilikuwa ni dolla bilioni 1.35. walipoelekea tu kutaka kutoa asilimia 45 ya hisa wawekezaji walifoleni pale kwa sababu ni shirika ambalo lina tija kubwa sana. TTCL, halikadhalika tukiwekeza kwa ile miundombinu ya msingi ambayo tayari ilikuwepo, tukiwekeza na kuiboresha inaweza ikawa kampuni kubwa, ikaleta ajira nyingi na ikaleta kodi nyingi ukiacha faida nyingine nyingi ambazo zimezungumzwa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza kidogo hapa, kuna watu walitaja juu ya uwekezaji kwenye Sekta hii ya Mawasiliano. Hawa watu walionunua TIGO na ZANTEL, Exim nilisoma kwenye gazeti la East African, lazima nikiri hii ni taarifa ya kwenye gazeti wana mpango wa kuwekeza mbali na fedha walizonunulia, wanawekeza dola milioni 400 ndani ya miaka mitano kufufua haya mashirika. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba sisi tukizungumzia uwekezaji mdogo mdogo tutaendelea kucheza hapa hili shirika halitafufuka na tutaendelea kupata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mchango wangu ni mfupi kwa sababu mengi yamezungumzwa. Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)