Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nami nianze kwa kumpongeza Waziri mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa kuweza kuwasilisha hotuba yake vizuri, hotuba nzuri iliyosheheni ubunifu mkubwa na ninaamini kwamba atakwenda kutekeleza kama walivyoainisha kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba tunamshukuru Waziri kwa sababu ni mtu mnyenyekevu sana. Mimi toka nije hapa Bungeni sijaona Waziri amenifuata akaniambia pale kwako vipi mambo? Kwenye mambo ya mawasiliano yako sawa? Sijaona. Sijaona mwingine aliyenifuata akaniambia vipi maji? Sijaona; lakini yeye ameweza kuja kwetu na kutuuliza kwamba vipi tunaonaje mambo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kwa kuamini kwamba zile Kata zetu za Kirua Vunjo, Marangu, Mwika na Makuyuni ambapo pia tuko mpakani, lakini zaidi ni kwamba vijiji vingi vimepakana na Mlima Kilimanjaro na msitu. Kwa hiyo, kule mawasiliano yanakuwa ni vigumu sana. Naamini tutatafuta mbinu ya kupeleka minara au kupeleka njia nyingine za mawasiliano kwa hawa watu walio kule kwenye mpaka na kwenye vijiji ambavyo kusema kweli hawapati mawasiliano sasa hivi na kidogo wanayopata ni ya Kenya, hata kama ni redio pia zinapatikana za Kenya na siyo sehemu nyingine. Kwa hiyo, nataka niwaombe watekeleze hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kukazia mambo machache. Natumai yanaweza yakawa yamezungumzwa, issue ni kwamba ni lini tutaweza kufungamanisha mifumo yetu ya utambulisho wa wananchi? Utambulisho wa wananchi umekuwa ni tatizo kubwa. Ukitaka kwenda kwenye Passport unaambiwa jaza fomu zile zile ambazo unajaza unapokwenda NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mahali utakapokwenda utajaza; hospitali utajaza, utarudia na bado una kitambulisho chako cha NIDA, lakini bado ukienda hospitali hawawezi kutumia kile kitambulisho waka-access zile data kwa sababu ile database inaonekana kwamba bado haijafungamanishwa ili iweze kuwa accessed na wadau wote wanaotaka kupata taarifa za mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufungamanisha huko pia kunawezesha kabisa hata kuongeza usalama kwa sababu ukweli ni kwamba mtu anapofanya makosa; na kama anajua kwamba namba ya NIDA aliyonayo, yale makosa yataandikishwa kule, basi anakuwa na uwoga zaidi kwa sababu inakuwa ni rahisi kumfuatilia mtu makosa aliyofanya na mazuri aliyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na inakuwa ni rahisi sana hata kwa mabenki kuweza kumfahamu huyu mtu ni wa namna gani wanaku-access katika database ile ambayo itakuwa imefungamanishwa kwa watu wote, iwe ni simu na kila kitu kitakuwa kule. Naamini kwamba kwa zile reference bureau nazo zitaingiza database yao huko. Kwa hiyo, tutakuwa tunaweza kufanya mambo kama hayo. Nchi zote zilizoendelea zinafanya hivyo, mtu anakuwa na namba moja, hawi na namba mbili, na ninaamini kwamba kitambulisho kinakuwa ni kimoja siyo viwili ili mtu yule aweze kutambulika kila mahali anapokwenda na saa yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba sekta ya TEHAMA ndiyo inayokuwa kwa kasi zaidi sasa. Sasa tumeunda Wizara ya Teknolojia na TEHAMA kwa ujumla. Nataka niseme hivi, fursa zilizopo ni nyingi sana, nchi nyingine zimeamua kufanya kwamba TEHAMA ndiyo sekta ya muhimu kuliko zote; nchi kama Rwanda mnafahamu. Nia yake ni nini? Ni kwa sababu wako vijana wengi wanapokwenda shule na kwenye vyuo wanajiunga kwenye hii fani, lakini kuwatumia inakuwa vigumu. Kwa sababu hakuna mitandao inayofanya kazi vizuri kwenye maeneo yale ambayo vijana hao wanamalizia shule zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna mkonga, kwa nini hatuwezi kuwezesha Wifi ikapatikana kwenye maeneo mengi tu hata kwa bure? Nami nakubaliana na mwenzangu aliyesema kwamba TTCL ikiwezeshwa ikatumia mkonga huu ikawekeza vizuri kwenye maeneo mengi ya vijijini, siyo mijini tu, vijijini zaidi kwa sababu kuna fursa. Sasa hebu niulize kwa mfano, masoko sasa hivi hayatafutwi kwa mtu kusafiri kwenda kuangalia soko, mtu anatumia simu, hii simu imekuwa ni ofisi, huhitaji ofisi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nawaambia wapigakura wangu kwamba hii simu ni ofisi yenu, huna haja ya kwenda kutafuta mnunuzi wa ndizi Dar es Salaam wakati unaweza ukapiga ndizi yako picha ukaituma kwa rafiki yako Dar es Salaam akakwambia nitumie kwa shilingi fulani, umeshafanya biashara. Kwa hiyo, biashara unaweza ukaifanya kwa kutumia tu kiganja chako na uwe na simu, lakini iwe janja kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niombe hiyo kwamba kweli tufanye hivyo. Pia Wizara ione namna ya kutoa mafunzo kwenye vyombo vya Habari; kwenye TV na kwenye redio, kueleza watu ni fursa zipi zinafunguliwa kwa kuwa na uwezo wa kuwasiliana nchi nzima na nchi za jirani, hata dunia nzima inawasiliana na hii simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vile vile lazima gharama zipunguzwe. Sasa tutapunguzaje gharama? Nafikiri kwamba tunavyozidi kuongeza mtandao, hasa huu wa TTCL; na tunaamini kwamba wataweza kuleta ushindani ambao utalazimisha wale wengine ambao wanafanya tu biashara waweze kushusha bei zao, lakini ni lazima TTCL ifanye kazi kwa nguvu zaidi. Kwa hiyo, naomba kwamba kuwepo na hivyo vipindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mheshimiwa alizungumzia kuhusu technology hub. Tuna COSTECH, imeweza kuanzisha incubation centers na hizo incubation centers ndiyo zinachukua na zinashindanisha; unaweza ukatangaza kwamba watu wenye uwezo hasa wale waliosoma IT, ambao wana ubunifu wowote wa teknolojia, waweze kufikisha pale. Hiyo ndiyo njia ambayo itaweza kuwaajiri hawa vijana na pia ku…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kimei kwa mchango mzuri.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)