Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ambayo ni ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema naomba ninukuu dira na dhima ya Wizara ya Afya. Dira yao inasema hivi; ni kuwa jamii yenye afya bora na ustawi inayochangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu mmojammoja, jamii na Taifa. Dhima ya Wizara ya Afya inasema hivi; kutoa huduma endelevu za afya zenye viwango vinavyokubalika kwa wananchi wote bila kikwazo cha fedha kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia na usawa wa jinsia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nimesema nitangulize dira na dhima ya Wizara ya Afya? Ni kwa sababu ya mambo ambayo yanaendelea kutendeka katika utoaji wa huduma wa Wizara hii. Nakwenda kwa CHF iliyoboreshwa ambayo ndiyo inayopatikana katika mazingira tunayotoka na wananchi wetu ndio wanayoipata. Sasa CHF iliyoboreshwa iko hivi; wananchi wanatoa ile 30,000, wanaambiwa watakwenda kutibiwa kwenye zahanati, lakini kinachotokea, wakifika pale kwenye zahanati wanaandikiwa tu na Daktari waambiwa dawa nenda katika dirisha lile pale uende ukafuate.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo imetokea kwenye mazingira yetu, mimi natoka Kalenga mazingira yako hivyo; Isimani hivyo hivyo na maeneo mengine iko hivyo hivyo. Kwa hiyo kunakuwa na uhaba wa dawa, hawapati dawa kwa CHF hiyo iliyoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii inasababisha nini; unakuta kwamba mtu anakwenda pale labda ana 10,000 ambaye siyo mtu anayepata ile huduma ya CHF, anahudumiwa na Daktari pia pale, tena hao wanashughulikiwa harakaharaka na akienda pale ananunua dawa kama yule. Sasa watu wameona kwamba hivi huduma ya afya ni bure ama ni ya kulipia hata kama una CHF au NHIF.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna hata hii bima ya NHIF ambayo watumishi wapo katika kada hizo, Walimu na watumishi wengine walipo katika sekta hizo vijijini wanalalamika kukosa dawa katika zahanati. Ukikosa unaambiwa uende mjini ukadai, kuna fomu ukajaze ukijaza hiyo fomu ndiyo utakwenda kuchukua dawa. Sasa imagine unatokea Pawaga ama unatoka Magulirwa, umekwenda Kalenga ambayo unafika kwanza mjini halafu unakwenda Kalenga hizo kilometers. Sasa unakwenda kule kwenye zahanati unatibiwa unarudi tena mjini uandikiwe na hao Maafisa Afya ambao wako Gangilonga pale Iringa Mjini; natolea mfano wa Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaleta gharama kubwa sana kwa wananchi. Matokeo yake wameona kwamba hii CHF ni kama siyo msaada kabisa, hata NHIF. Kwa hiyo niishauri Wizara kutokuwepo kwa dawa ni changamoto kubwa sana na hii inafanya wananchi wasiiamini Serikali au NHIF kwa sababu hakuna dawa, watu hawatajiandikisha wengi kwenda huko. Ukiangalia unakuta kwamba kuanzia mtoto wa mwaka mmoja, mtoto anayezaliwa mpaka miaka mitano kupata kile kitambulisho cha NHIF ni siku 90. Kwa hiyo unakuta wanaona kwamba kuna changamoto; naomba wabadilishe na waboreshe hicho kwa sababu ni changamoto kubwa ambayo wanaipata wananchi wanaona kwamba hakuna haja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunataka twende kwenye Bima ya Afya kwa Wote na Waziri amezungumza hapa, tunataka Bima ya Afya kwa Wote. Bahati nzuri sisi wakati huo Bunge lililopita, mimi nilikuwa katika Kamati ya Huduma, tulikwenda Rwanda, wengine walikwenda Ghana na wengine walikwenda mahali pengine, lakini tulikuta wenzetu wamefanikiwa kuwa na bima ya afya kwa wote, waliweka mkakati maalum kwa nchi yao kuhakikisha wananchi wanapata bima ya afya kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kuna fedha imetengwa pale kwa mchakato, lakini tuliambiwa kwamba ni Bunge lile utakamilika lakini tumekuja hapa naona Waziri tena ameweka mchakato. Watueleze lini wanakamilisha ili tuwe na Bima ya Afya kwa Wote na wananchi wetu waweze kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja katika kipengele cha watumishi wa afya; tuna changamoto kubwa ya watumishi wa afya; sekta ya afya vijijini na mijini nadhani, kuna changamoto kubwa. Unakuta kuna mganga mmoja ndio anayehudumia wananchi wote walioko pale. Uzuri Kamati imetoa takwimu kwamba ni asilimia 53 ya uhaba wa watumishi wa sekta ya afya. Mheshimiwa Waziri atueleze wanaajiri lini ili waweze kukimu hii asilimia 53 ya watumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, hawa watumishi wa afya wamekuwa wakipata adha nyingi; wamekuwa hawapandishwi mishahara, hawalipwi marupurupu yao na changamoto hizo ambazo zipo. Wanakosa morali ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zile call allowances walikuwa wanapata, tunaomba wawape; kuna postmortem allowance, wanafanya kazi kubwa mno hawa Madaktari wetu, kazi ni kubwa. Ukiwa mgonjwa ndiyo utajua kazi kubwa wanayoifanya hawa Madaktari; wawape hiyo allowance na motisha nyingine ambazo zinapaswa wapate hawa Madaktari, wanafanya kazi kwa weledi mkubwa na mazingira yao ni magumu, tunaomba wawape hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja katika kipengele cha wazee. Wazee wa nchi hii ni watu ambao wamechangia sana katika maendeleo ya nchi yetu, lakini pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi yetu Serikali bado haiwatambui katika huduma ya afya. Wazee wanakwenda kwenye madirisha yale, tulisema kutakuwa na madirisha ya wazee, naomba Wizara ituambie ina madirisha mangapi mpaka sasa katika Halmashauri mbalimbali zilizopo nchini ya kupata dawa za wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, Serikali imechukua hatua gani kwa wale ambao hawajatekeleza hilo agizo katika halmashauri zetu? Maana wazee wanakaa wanahangaika huko tunakotoka. Ni lini Serikali sasa itagharamia kuwapa bima ya afya wazee ili waweze kutibiwa. Tunajua wazee wanapofikia umri huo magonjwa na maradhi yanakuwa ni mengi mno; tunaomba Wizara ilitilie mkazo suala hilo la wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti wanayopata hii Wizara ya Afya ni ndogo sana na haitoki kwa wakati. Unakuta kwamba wamepewa asilimia chache sana kwa maendeleo….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha, ahsante sana.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)