Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii ya leo. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuwapongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Gwajima na Naibu Mawaziri Mheshimiwa, Dkt. Mollel na Mheshimiwa Mwanahamisi. Kwa sababu leo ndiyo siku hii Wizara inayohusika na mambo ya wanawake, naomba kwa kweli nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Kwanza kabisa kwa kuwa Rais ambaye amekuwa akituwakilisha vyema, lakini nimpongeze pia kwa hotuba yake ambayo alikuja kuhutubia hapa Bungeni kuhusiana na mambo ya afya. Ametuhamasisha sana. Vile vile, nampongeza kwa kumteua Naibu Waziri ambaye anashughulika na masuala ya wanawake, wazee na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya masuala siku zote tulikuwa tunaona yanamezwa na masuala ya afya, kwa sababu katika Wizara hii kuna mambo mazito mengi ya wanawake, watoto na wazee ambapo tulikuwa tunaona hata sisi wenyewe tukichangia tunaenda moja kwa moja kwenye afya. Sasa tuna imani Naibu Waziri wetu atachangamsha kuhakikisha kwamba anasikiliza changamoto zinazohusu wanawake, wazee na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais. Amewateua wanawake kwenye nafasi nyeti sana. Kwa hiyo, nampongeza na nina imani kabisa tutawaunga wenzetu mkono na watafanya kazi vizuri akiwemo dada yetu Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na wote waliochaguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze hata Wabunge waliochaguliwa katika Majimbo wakiongozwa na wewe mwenyewe. Kwa kweli, tunaona kazi kubwa mnayoifanya na tunawatia moyo na tuna imani kwamba wananchi waone kazi ya mwanamke, wanawake tunaweza na tunasema kwamba mzigo mzito mpe mwanamke, atauweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja sasa kuna vitu viwili nataka kusema. Jamani wanaume mpo? Wanaume mpo? (Kicheko)
WABUNGE FULANI: Tupo.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wale waliosema jamani, hiki ni kipindi cha wanaume sasa kupima UKIMWI. Tulikuwa na Balozi wetu Waziri Mkuu ametuwakilisha vizuri sana kuhakikisha anawahamasisha wanaume kupima, lakini bado hawapimi, wanatupimisha sisi wanawake. Wanaume wengi wanaishi na virusi lakini wanatuficha na wakati mwingine wanameza dawa hawatuelezi, wanaweka sehemu nyingine. Kwa hiyo, niombe kwa kweli kupitia Bunge hili leo hii tuhamasishe wanaume wote wakapime na tuanze na Wabunge wote wanaume muwakilishe wanaume wenzenu kwenye majimbo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu maambuzi mapya ni asilimia 40, utakuta kwamba asilimia 80 ni watoto wa kike. Sasa niseme kwamba unaona kwa watoto wa kike wengi wanaambukizwa kwa sababu pia wanabakwa sana. Watoto wa Iringa, tuna kesi zaidi ya 400 wamebakwa, kuna mwanaume mmoja alibaka watoto saba amewabaka siku moja. Kwa hiyo, kwa kweli niombe kabisa pengine hata sheria ije. Naomba kwa kweli sasa hili liangaliwe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule China watu wakiiba wanauawa, lakini sasa hawa sijui tuangalie adhabu gani maana kitu kinachosababisha watoto wetu wabakwe kiangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema kwamba nyumba ni choo. Sasa kulikuwa kuna kampeni ile ya kuhamasisha vyoo bora vijengwe kwenye vijiji vyetu. kunapokuwa na vyoo bora inasaidia kupunguza hata maambukizi yale ya katika maji, kwa sababu bado kwenye vijiji wananchi wanatumia maji ya kwenye mabonde na mito, kwa hiyo unakuta maambukizi yanakuwa mengi sana. Nimwombe Waziri mwenye dhamana ahakikishe kwamba ile kampeni inaendelea kwa sababu bado kuna kaya hazina vyoo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kuhusu Bima ya Afya. Niombe, naona leo wengi wameongelea kuhusu Bima ya Afya, lakini niombe Bima ya Afya iongeze wigo wa matibabu. Kuna magonjwa ambayo yanawatesa sana wananchi hasa magonjwa ya figo na magonjwa ya saratani. Unaona wananchi wanatumia pesa nyingi sana, wengine ni watumishi tu wa kawaida, wengine hata sio watumishi unaona bima zile bado hazimwezeshi huyu mgonjwa kwenda kutibiwa kwenye hospitali zetu. Wamekuwa wakipata shida, wanakuwa wakienda kule kwenye matibabu inatakiwa watafute nyumba za kupanga. Niombe Serikali yetu hii iangalie wanyonge hawa ambao kwa kweli mara nyingi wamekuwa wakipata mateso makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite kwenye changamoto za Mkoa wangu wa Iringa. Jambo la kwanza ni Hospitali yetu ya Mkoa ina shortage kubwa sana ya Madaktari Bingwa kwa magonjwa mbalimbali. Karibu Madaktari saba wanahitajika katika hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa. Pia, hii CT scan machine nilishawahi kuleta hata swali ni tatizo kubwa sana kwa wagonjwa wetu pale Mkoani Iringa. Nishukuru kwamba Serikali imesema kwamba itaanza kuleta hizi mashine katika hospitali za rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nielezee changamoto nyingine, ambayo ni upungufu mkubwa sana wa watumishi wa Sekta ya Afya. Unaona karibu asilimia 62 ya mkoani kwetu bado tuna upungufu mkubwa na katika hata baadhi ya Wilaya kwa mfano Kilolo hospitali imeshakuwa tayari kabisa lakini tatizo ni watumishi wa afya. Niiombe Wizara sasa iende sambamba na hizi hospitali zinazojengwa, iweke watumishi ili kuondoa changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hawa watumishi wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Unaona wanafanya kazi kwenye maeneo hatarishi, hata wakati wa covid vifaa havikuwepo vya kutosha. Kuna wengine walipoteza maisha. Naomba pia Serikali iangalie pia na suala la vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusiana na dawa MSD. Kuna malalamiko kwamba watu hawapati dawa wanalazwa lakini dawa hawapati. Inabidi tena waende wakatafute sehemu nyingine. Mimi niombe kwamba MSD ijitahidi kwa sababu ilibidi nifanye ziara kwenye hii Hospitali ya Mkoa na wakasema kwamba wanapeleka asilimia 50 ya yale makusanyo lakini dawa wanazohitaji kule hakuna. Sasa iwe kama zamani kwamba kama hakuna dawa basi waangalie labda kwa wale washitiri, kwa maana waruhusiwe kwenda kununua hizo dawa, kwa sababu limekuwa ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nitoe pongezi kubwa sana. Tumekuwa na watu ambao wanachangia Wizara yetu ya Afya lakini bado sijajua kama Serikali inawatambuaje. Kwa mfano, kwenye Mkoa wetu wa Iringa tunayo majengo ambayo yamejengwa na wadau wa maendeleo. Kwa mfano, nimpongeze Mheshimiwa ASAS, labda nitaje tu baadhi ya majengo ambayo amejenga. Kuna jengo la Benki ya Damu, Wodi ya Watoto Njiti na vifaa vyake, ICU unit, Jengo la Kiwanda cha Viungo Bandia, jingo la Kituo cha Ustawi wa Jamii na mengine mengi. Kwa kweli, naomba tutambue michango ya wadau ambao wamekuwa wakisaidia hata bajeti yetu ya Wizara ya Afya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga.
MHE. DKT. RITTA E. KAKABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.