Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza sina budi kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa alivyowasilisha vizuri taarifa yake, vilevile kuwapongeza walinzi wetu wote waliokuwepo hapa jinsi walivyokuja na tulivyowaona na jinsi wanavyohamasisha wanapokuwepo kwenye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kidogo nilikuwa nataka kuzungumza makazi ya wanajeshi wetu waliokuwepo pale Mererani wanaolinda Tanzanite. Kwa kweli Kamati ilipokwenda hali tuliyoikuta pale ilikuwa siyo nzuri, maana kwa maneno ya mjini utasema hali ya full suit, makazi yao juu bati, kuta bati, sasa kwenye joto, kwenye baridi wanapata shida. (Makofi)

Sasa tungeomba wawaboreshewe yale makazi kwa sababu askari wetu wasikivu wakakamavu wanatufanyia kazi nzuri basi na makazi yao japo nyumba mbili, tatu pale zijengwe za za kudumu waweze kufanya kazi zao kwa uweledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia tena JKT; kuhusu ujuzi, kazi ya JKT kumfanya kijana awe mkakamavu, kijana awe mzalendo, lakini vilevile kuwafanya vijana wetu wakiondoka wawe na ujuzi, mnaweza kumfanya fundi cherehani, fundi makenika, fundi ujenzi, fundi mchundo, lakini akiondoka pale tayari anakwenda mitaani ana ufundi wake mwenyewe wa kwenda kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa kuwaongezea lingine, mngekuwa mnatoa elimu ya Muungano, vijana wetu akitoka pale tayari anakuwa anajua nini chimbuko la Muungano. Akifika pale anatoka anajua nini faida ya Muungano, sasa hilo mkilifundisha ninyi kule na vijana wetu wengi mnawachukua litasaidia. Hii kuzungumza nitaienzi, nitaitukuza itakuwa rahisi kule ameshapata elimu ya kutosha. Sasa ningewaomba katika masomo yenu mnayotoa chimbuko la Muungano lazima liwemo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie lingine kuhusu Ofisi ya Wizara ya Ulinzi - Zanzibar. Ofisi za Muungano ipo ni moja tu, Ofisi ya Makamu wa Rais na ipo nyingine Mambo ya Nje, lakini zote haziridhishi, kwa sababu ya Makamu wa Rais imo ndani ya makazi yake, kule haipendezi kuwekwa ofisi. Kule kuna makazi ya Makamu, ofisi lingejengwa jengo moja kama la ghorofa au jengo la chini, ikawepo Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Ndani, Muungano, Mambo ya Nje na taasisi zote za Muungano zikawepo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu kama anashida ya jambo la Muungano anajua nakwenda sehemu fulani nitaikuta ofisi na nitamaliza mambo yangu. Mtu anastaafu aende Bara, mtu ana matatizo yake katika Wizara ya Muungano aende Bara, kwa kweli haipendezi, na hata ninyi mkija Zanzibar mtafikia rest house, hotelini au kambini, pia haipendezi. (Makofi)

Sasa ningeomba mkashirikiana na mkajenga jengo moja tukasema hili jengo la Muungano, mtu anashida anakwenda pale Wizara zote atazikuta pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka sehemu nyingine stahili za likizo za wanajeshi. Toka mwaka 2011 mpaka 2020 wanajeshi hawajapata stahili zao za likizo na hasa wale wanyonge, wanadai shilingi bilioni 114 kama sikosei. (Makofi)

Sasa na hili mliangalie, mwanajeshi hawezi kusema hana wa kumsemea, atanung’unika pembeni na hastahiki kunung’unika. Sasa kama hatukuwasemea mtu haki yake apewe. Hata mama mwenyewe analipigia kelele hili watu wenye stahili zao walipwe, sasa ningekuona na hili ukaliangalia kwa jicho la huruma na kwa jicho la imani vipi mtawasaidia wanajeshi wetu waendelee kufanya vizuri ingawa wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja la mwisho, Hospitali ya Jeshi iliyokuwepo Zanzibar Bububu, hospitali nzuri inafanyakazi vizuri, lakini tungeomba kizuri lazima na kingine uongeze. Mngetuongezea nyingine kama Mkoa wa Kusini mkatufanyia kama ile iliyokuwepo Bububu au moja mkapeleka Pemba kama iliyokuwepo ili tunajua kwa sababu unapotaka upate matibabu mazuri ukikimbilia jeshini, jeshini hambagui, hambagui kitu, yoyote atakayekuja mnamtibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hasa ningeona hili mliangalie kwa sababu pale pana vifaa vya kileo, pana madaktari wazuri, kuna kila sifa mnayo, mtu uzuri wake aambiwe, lakini tunataka kama itakupendeza au itawezekana mtutafutie na nyingine ikiwa mtaweka Mkoa wa Kaskazini maana hii ipo Mkoa wa Mjini Magharibi. Kama mtatuwekea Kaskazini au Kusini na nyingine Pemba kama mtaweka Kaskazini au Kusini ili kila zikiwa zipo nyingi na mambo yetu yanakuwa mazuri na ninyi kama mnapata thawabu kwa Allah. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kwa haya machache naunga mkono hoja. (Makofi)