Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende ku-declare interest yangu hapa, mimi nimezaliwa jeshini, ni mwanajeshi niliyefanya kazi jeshini miaka 33; kati ya hiyo miaka 13 nilikuwa nimewekwa attachment Wizara ya Mambo ya Nje, kwa hiyo….(Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pinda, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nakumbuka kumbukumbu zangu ukiwa umekalia kiti hapo ulitupa mwongozo tukisema una-declare interest au maslahi jambo unalozungumzia labda uwe unapata fedha direct. Sasa Mheshimiwa Pinda naomba nikupe taarifa kwamba kukaa kambini sio kwamba una maslahi, wengi tumekaa kambini.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, mtoa hoja hajaelewa ninachokisema, kwa hiyo naomba nimuhurumie tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema kwamba mimi ni uzao wa jeshi na nimetumika jeshini miaka 33 na hivyo basi ninaposimama kama Naibu Waziri wa Katiba na Sheria najisikia raha sana kwa sababu nimetokea kwenye chombo hiki ambacho leo kimewasilisha bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya kuchangia; kwanza niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna ya pekee jinsi ambavyo mmechangia, mmetoa mawazo makubwa sana, nadhani Wizara ya Ulinzi mwakani tutakaa mkao mzuri ili kuandaa bajeti inayolingana na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge kwa sababu mmegusa maisha ya wanajeshi kwa karibu sana na hili ni jambo muhimu sana kwa sababu wakati mwingine tungekuwa tunashuhudia tu nashika shilingi, lakini kumbe nimebaini kwamba mnajua umuhimu wa hiki chombo ambacho ni chombo muhimu sana hasa kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba katika kufikia uchumi wa kati, jeshi limechangia sana kwa sababu bila utulivu tumeshuhudia nchi nyingi zinakimbia kimbia, hakuna muda wa kuzalisha. Hivyo basi niwaombe mkawe mabalozi huko ambako vikosi vyetu vya jeshi vipo karibu na wananchi, mjaribu kutusaidia kuelimisha wananchi kuelewa umuhimu wa hivi vikosi vya jeshi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hakuna Kikosi cha Jeshi kinachowekwa bila mpango maalum wa umuhimu katika ulinzi wa nchi. Kwa hiyo utaona maeneo mengi ambayo vikosi hivi vipo vina malengo maalum katika kulinda mipaka ya nchi yetu na kuwalinda wananchi wake ambao tunalala na kuamka salama bila hata kuchomwa na sindano na maadui zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya jeshi; makambi na vikosi vya jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) vinaundwa kulingana na sheria ya ulinzi ya Taifa Na. 24 ya mwaka 1966 ambayo imefanyiwa marekebisho na kuwa Sura ya 192 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mwaka 1966 hadi 1979 Serikali imetenga maeneo mengi na makubwa mbalimbali mbali na miji na vijiji kwa matumizi ya jeshi. Miaka ya hivi karibuni kumezuka migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo kadhaa ya jeshi, kwa sababu mbalimbali zikiwemo maeneo ya jeshi kutopimwa kuchelewa kulipa fidia mapungufu ya sheria za ardhi kupanuka miji midogo kuwa miji mikubwa wananchi wasio wahaminifu kuvamia maeneo ya jeshi. Hata hivyo Wizara inachukuwa hatua mbalimbali kutatua migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na kupima maeneo yake kufanya uthamini na kufanya vikao vya usuluhishi na wadau wa migogoro husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo tayari upimaji umefanyika na ramani zake kusajiliwa. Wizara inafanya jitihada za kuandaa hati miliki, hadi sasa Wizara ya Ulinzi imeweza kupima maeneo yake yapatayo 121 kati ya 203; maeneo matatu tayari hati miliki zimepatikana na maeneo 62 yapo katika mipango ya kuomba kuandaliwa kwa hati.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021 imeweza kulipa fidia kwa maeneo kumi yakiwepo Kigongo Ferry na Ilemela shilingi 6,824,544,927; Nyagungulu na Burihahela shilingi 3,534,295,165.58; Mwanza Mlangalini na Mashono huko Arusha shilingi 1,548,490,247.88. Kwa upande wa Kilwa ni shilingi 624,236,405 Makoko ni shilingi 1,109,841,249 na Nyabange Musoma shilingi 203,646,661 na Airport Chato, Geita ni shilingi 972,218,036.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara inatarajia kulipa maeneo yafuatayo Nyamisangula Bugosi na Kanyambi - Tarime shilingi 1,631,984,692.76; Kaboya - Muleba shilingi 4,440,346,998.25; Kikombo - Dodoma shilingi 2,261,604,837.45; Mitwero - Lindi shilingi 187,888,88 na Duluti - Arusha shilingi 4,694,000,000 idadi ya maeneo yaliyotarajiwa kulipwa fidia kwa mwaka wa fedha 2021/2022 yataongezeza kutokana na timu ya wataalam walioko uwandani hivi sasa wakifanyia upimaji na uthamini kwa sababu timu hiyo ipo Mikoa ya Lindi na Mtwara wakiendelea kutekeleza majukumu ya upimaji na thamani yake. (Makofi)
Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo niombe tu kwenu mjaribu kuwapelekea wananchi wawe watulivu kwenye maeneo yale ambayo bado hatua za uthamini zinaendelea, lakini Serikali inaendelea kupunguza ulipwaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kilimo kwa upande wa JKT; katika kuhakikisha kwamba JKT inajitosheleza kwa chakula, umeandaliwa mpango mkakati 2019/2020 - 2024/2025 ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya mkakati huu ambayo yamefanyika ni pamoja na kuandaa andiko la mkakati, upimaji wa ukubwa wa mashamba na afya ya udongo katika maeneo ya vikosi, upatikanaji wa pembejeo na kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba. Aidha, kwa kuanzia JKT imeanza ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Shamba la Chita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutekeleza mkakati huu JKT imeingia makubaliano na Wizara ya Kilimo katika maeneo ya utaalam na teknolojia ya kilimo, mafunzo ya utaalam, mbinu za uzalishaji bora wa mazao, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, masoko ya mazao na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo makuu ya mkakati huu ni kuongeza uzalishaji wa mazao ili kujitosheleza kwa chakula na kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia sekta ya kilimo na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio ya Jeshi la Kujenga Taifa ifikapo mwaka 2024/2025 ni kuhakikisha linaongeza maeneo ya kilimo kutoka ekari 14,200 zinazolimwa sasa hadi kufikia ekari zaidi ya 28,000 sanjari na kuongeza eneo la umwagiliaji katika shamba la Chita kutoka ekari 2,500 zinazojengwa kwa sasa hadi kufikia ekari 12,000 ifikapo 2024/ 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo basi, mimi naamini wazi kwamba hata baada ya muda huu vijana watapata nafasi ya kujiajiri kwa sababu sasa hivi ni kweli vijana wetu wanapoambiwa wanakwenda JKT wazo la pili walilonalo ambalo wanaondoka nalo ni kupata ajira. Lakini ukweli ni kwamba JKT inakwenda kuwajengea uwezo wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa naamini wazi kabisa kwamba tukihamasika hata sisi Wabunge kuwatumia wale vijana waliomaliza JKT kuwaweka katika makundi ya uzalishaji kwenye maeneo yetu, watakuwa na tija ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, nipende tu kusema hayo, lakini naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)