Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza, nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri, Katibu wake na watumishi wote wa Wizara hii. Wizara hii imepata mtu ambaye tunamtegemea sana Waziri pamoja kijana wetu Naibu Waziri, kwa kweli tunawapongeza kwa kazi nzuri ambayo mmekuwa mkiifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi, naunga mkono ushauri wa Kamati ya Kilimo na nadhani muifanyie kazi. Kamati ya Kilimo wameshauri vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie changamoto ambazo zipo nchi nzima au kwenye Mkoa wetu wa Njombe na hususani Jimbo langu la Makambako. Tuna changamoto kwenye zao la mahindi, mahindi katika Mkoa wetu inawezekana na Mikoa mingine ni tatizo kubwa. Mpaka sasa mahindi hayajapata soko, mahindi ya mwaka jana mpaka sasa yapo. Nashauri Wizara ijipange kutafuta masoko ili wananchi wetu waweze kuuza mahindi haya. Wamekuwa wakitupigia simu sana, mahindi yapo kwenye maghala yao mpaka sasa hayajauzwa na hivi sasa kwetu Njombe wameanza kuvuna tena ya msimu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda Njombe kule mahindi yanauzwa debe Sh.3,000 au Sh.3,500, plastiki ya lita kumi na tisa au ishirini. Kwa hiyo, unakuta sasa uuzaji wa mahindi wa debe hili au gunia hauendani na ununuzi wa pembejeo. Kwa mfano, mbolea ya DAP ndiyo tunatumia sana sisi na mbolea hii ya Urea, mfuko mmoja unauzwa kati ya Sh. 55,000 hadi Sh.60,000, ukijumlisha mifuko miwili unapata Sh.110,000. Katika Sh.110,000 mpaka uuze gunia karibu nne ndiyo ununue mifuko miwili. Kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ione namna ya kukomboa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri ili mbolea hii iwe bei chini, Mheshimiwa Waziri tunaimani sana na wewe, Serikali tafuteni wawekezaji ili vijengwe viwanda vya mbolea ya kuzalisha DAP na Urea katika nchi hii hii. Tukipata wawekezaji wa kujenga viwanda vya mbolea, tunaimani mbolea itashuka itaendana angalau na bei ya soko la mazao ambayo wananchi wetu wamekuwa wakiuza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine tuna maghala ambayo mlianza kujenga Dodoma, Makambako na mahala pengine, maghala haya hayajaisha. Ombi letu muhakikishe maghala haya maghala haya yanaisha.
Mheshimiwa Spika, tuna Benki ya Kilimo (TADB), benki hii ipo Dar es Salaam na wakulima wetu kutoka mikoani kule kwenda Dar es Salaam ni mbali. Kwa hiyo, haiwasaidii kabisa vinginevyo inawasaidia watu wenye uwezo mkubwa. Ombi langu ni kwamba benki hii iende katika maeneo husika angalau muitoe Dar es Salaam muweke Dodoma hapa ndiyo katikati. Vilevile mshushe huko kwenye mikoa yetu hasa kwenye mikoa ile ambayo ndiyo inayozalisha mazao ya kimkakati na mazao mengi zaidi ikiwepo Mkoa wa Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile ipo changamoto ya wakulima wetu wa chai, amezungumza sana ndugu yangu hapa Mheshimiwa Swalle ambapo kule Njombe kuna majimbo matatu yanayozalisha chai kwa wingi likiwepo Jimbo la Mheshimiwa Mwanyika, Jimbo la Mheshimiwa Swale la Lupembe na Jimbo la Ludewa. Tatizo kubwa wakulima hawa wameanza kukata tamaa kwa sababu wanacheleweshewa kulipwa fedha zao wanapouza chai, inachukua mpaka miezi minne/mitano hawajalipwa. Kwa hiyo, ombi langu Wizara msimamie kuhakikisha wananchi wanalipwa chai yao wanapouza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Njombe tuna zao kubwa vilevile la parachichi. Parachichi soko lake ni kubwa lakini parachichi hizi zinapozalishwa kule Njombe vifungashio, sitaki nionyeshe vinaonyesha vinatoka nchi gani, vifungashio vile wakifunga inaonekana maparachichi haya hayatoki Tanzania yanatoka nchi jirani. Ombi langu kwa Wizara hebu mfuatilie nchi ambazo zinanunua sana maparachichi na ninyi mjipange kuona moja kwa moja parachichi zinavyotoka Tanzania zinaandikwa parachichi za Tanzania, hii itatusaidia sana katika suala zima la masoko. Sasa hivi watu wanalima kwa wingi sana parachichi, itapendeza kujua soko hili litadumu kwa miaka mingapi na ni nchi gani ambazo zitanunua? (Makofi)
T A A R I F A
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa, ndiyo nimekuona Mheshimiwa.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba nchi ya Mexico wanatumia ekari 260,000 kuzalisha zao la parachichi sawa na asilimia 5 ya eneo zima la Mkoa wa Njombe na wanauza parachichi duniani wanapata trilioni 5. Hii maana yake sisi hatujakifanya kilimo hiki cha parachichi kama kilimo biashara. Ahsante.
SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Deo Sanga kwamba bado msisitizo kwenye parachichi unatakiwa.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, mimi nadhani anasisitiza kwenye suala la kilimo cha parachichi. Kwa hiyo, Waziri amesikia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante na kengele tayari.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, dakika amenimalizia huyo. (Kicheko)
SPIKA: Hapana, hayajatumia dakika zako, ahsante sana Mheshimiwa Deo Sanga.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.