Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii muhimu iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, wote tunakubaliana hapa kwamba kilimo ndiyo kimebeba uchumi wa nchi yetu. Asilimia 80 ya Watanzania wanafanya kilimo na kumekuwa na juhudi mbalimbali zinafanyika, naipongeza Serikali na katika hili juhudi inatakiwa kuongezeka na tumeendelea kushauri mara nyingi, nataka nishauri kwenye eneo moja kubwa sana la mbegu.
Mheshimiwa Spika, tusipokuwa na mbegu zenye tija hatuwezi kubadilisha kilimo chetu. Wananchi wataweka juhudi zao, muda wao, rasilimali zao lakini bado tutajikuta tunarudi nyuma, hatuwezi kwenda mbele. Kama hivi tunavyoambiwa wenzetu nchi nyingine wanalima eneo dogo lakini wanapata uzalishaji mkubwa ni kwa sababu ya utafiti mkubwa walioufanya kwenye mbegu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi kumekuwa na ruzuku inayotolewa kwa ajili ya mbegu. Nitajitika kwenye eneo la zao la alizeti. Leo hii tunalia wote hapa kwamba tuna tatizo kubwa la mafuta ya kula, Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula wakati tuna ardhi ya kutosha na mazao mengi yanayoweza kutoa mbegu za mafuta. Mfano zao la alizeti, tumekuwa na mawazo mengi ya kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji, kuna baadhi ya mbegu zile za kienyeji unatoa magunia matatu kwenye heka, unapoteza muda mrefu sana kufanya kazi ambayo haina tija.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na mawazo ya mbegu mbalimbali ambao zimeendelea kufanyiwa utafiti kwenye maeneo yetu. Kwenye eneo hili nimeona kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kuongeza utafiti. Nimuombe Waziri tuongeze nguvu kwenye eneo hili, watafiti wetu wapo, vituo vyetu vipo viongezewe fedha za kutosha kwa ajili ya kuja na mbegu zenye uzalishaji wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano mdogo kumekuwa na mawazo ya kuwa na GMO, tunatakiwa kuwa makini sana kwenye kuingiza mbegu hizi. Kuna baadhi ya nchi ambazo ni ushahidi leo wanapata mbegu hizo za GMO asilimia 100 hawana mbegu zao za asili katika nchi yao. Niombe sana Serikali inapoamua kufanya haya iwe na uhakika na tunachoenda kukifanya.
Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi kilimo cha umwagiliaji kipewe nafasi kubwa. Hekta hizi ambazo zinatengwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hazitoshi, hatuwezi kujitegemea kwa chakula. Katika eneo hili pia tuongeze wataalam wa kutosha kwenye Halmashauri zetu. Leo hii unaweza kusema unaweka skimu ya umwagiliaji unawakabidhi wakulima ambao wao wenyewe hawana uwezo wa kuendesha mradi ule, tunapoteza fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumesikia Tume ya Umwagiliaji inaboreshwa, niombe sana nguvu ziongezeke tuwaweke wataalam wale mpaka kwenye Halmashauri zetu ili waweze kusimamia kweli kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji tukikifanya vizuri, maeneo mengine wamefanya vizuri kwenye eneo dogo tunapata uzalishaji mkubwa. Leo nchi yetu inapata mvua nyingi sana kila mwaka, tuna baadhi ya maeneo mpaka zinaharibu miundombinu, tumekuwa tunalalamika hapa barabara zetu zinaharibika ni kwa sababu ya mvua nyingi. Yale maji yanapotea yanakwenda baharini. Naombe sana Serikali iweke nguvu kwenye kuvuna maji ya mvua na tuwe na mabwawa ya kutosha kwenye maeneo yetu ambayo yatatumika kwenda kuwasaidia wakulima wetu wawe na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni masoko ya mazao yanayopatikana, lazima tuwe na uwezo wa kuhakikisha kwamba mkulima anapolima ana uhakika anakwenda kuuza wapi. Mfano mdogo kwenye eneo la kilimo cha alizeti kuna baadhi ya maeneo kama Singida kule imeshuka kwa sababu kuna baadhi ya maeneo wakulima wanakopwa bado wapo shambani, watu wanakwenda kununua shambani bado mtu hajavuna. Maana yake ni kwamba anauza kwa bei ya kutupa, mkulima huyu mwakani hawezi kurudi kulima. Naomba Maafisa Biashara, Maafisa Mipango na Maafisa Kilimo kwenye Halmashauri zetu wasimamie vizuri suala la masoko ili kumfanya mkulima huyu afaidike na kilimo chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Maafisa Biashara, Maafisa Mipango kwenye Halmashauri zetu na Maafisa Kilimo wasimamie vizuri suala la masoko ili kumfanya mkulima huyu afaidike na kilimo chake. Tunaposema tuwe na usalama wa chakula kweli chakula, tutaendelea kuwa na uwezo wa kuhifadhi, lakini kuna mazao ya biashara tumesema hapa tuwe na kilimo biashara. Eneo dogo, tuweze kuwa na uzalishaji wa kutosha na mwisho wa siku mwananchi huyu tuweze kumkomboa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili nilikuwa nataka niongee kidogo sana kwenye eneo la Benki yetu ya Kilimo. Leo tunaipigia chapuo, ni benki imepewa fedha isimamie, lakini masharti yale siyo rafiki kwa wakulima walioko vijijini. Mfano, mimi ninayo AMCOS moja pale kwangu Misughaa pale Ikungi, leo hii ile AMCOS wamekopeshwa shilingi milioni 85 tu. Leo ninavyoongea mimi na wewe, wale AMCOS kwa sababu tu msimu uliopita haukuwa na mvua ya kutosha, wamepelekwa TAKUKURU, wamepelekwa Mahakamani, ni kama vile ambavyo hapakuwa na mkataba. Usitegemee wakulima hao mwakani wakaenda tena kwenye Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana, nitakukabidhi document hiyo Mheshimiwa Waziri ili uweze kufuatilia. Haiwezekani watu waliokuwa na mkataba wa makubaliano ya mkopo na walikubaliana kwamba watu wa bima wapo, wameshachukua ile nafasi ya bima halafu mwisho wa siku kwenye msimu wasipovuna vizuri wanapelekwa TAKUKURU, wanapelekwa Mahakamani, hakuna sababu. Huyu mkulima unamfanya aogope hata kwenda kukopa kwenye hiyo Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi zinazofanyika za kuongeza fedha, lakini kuna treatment siyo nzuri inafanywa na baadhi ya maeneo kwenye Benki yetu ya Kilimo, kwa sababu haimsaidii mkulima, inaenda kumnyonya zaidi na kumwondoa kwenye mawazo mazuri ya kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo tunaposema kwamba kuna baadhi ya benki hazina urafiki na wananchi wa kawaida. Basi hata hii Benki ya Kilimo ambayo Serikali imeweka fedha, tuwawekee mazingira mazuri wakulima wetu waweze kuwa na uwezo mkubwa wa kulima eneo kubwa, wawe na pembejeo za kutosha, wawe na vifaa ikiwemo matrekta ili kubadilisha kilimo chao kutoka kwenye kilimo kile cha kawaida. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Miraji.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, nawatakia kila la heri Wizara hii. (Makofi)