Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo kwenye Wizara hii ya Kilimo. Napongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri na nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii; Waziri na Naibu Waziri. Nadhani katika Wizara ambazo combination yake imekaa vizuri ni Wizara hii. Mawaziri wake ni wasikivu, lakini wana werevu mzuri, nami nina matumaini kwamba sekta ya kilimo itakwenda vizuri. Hongera sana Waziri na Naibu wako pamoja na Katibu Mkuu. Watu wapole na wasikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nataka nizungumze jambo mahususi kwenye korosho. Mwaka 2018 tulibadilisha sheria hapa ya tasnia ya korosho. Tulipofanya yale mabadiliko yalisababisha kufutwa kwa mfuko wa kuendeleza zao la korosho ambao ulikuwa unaitwa Mfuko wa Pembejeo, ambapo chanzo chake cha fedha ilikuwa ni tozo ya mauzo ya nje (Export Levy). Uamuzi ule ulipofanyika, wale waliokuwepo wanakumbuka, Serikali ilitoa ahadi hapa Bungeni kwamba inachukua zile fedha ambazo zilikuwa zikipatikana; na kwa sababu kile chanzo bado kipo, fedha zinapelekwa kwenye mfuko mkuu ili zikasimamiwe vizuri kwa hoja kwamba zilipokuwa kwenye huu mfuko zilikuwa hazisimamiwi vizuri.

Mheshimiwa Spika, makubaliano ilikuwa ni kwamba hizi fedha zikishaenda Mfuko Mkuu, zitarudi kuja kuendeleza zao la korosho kama ambavyo zilikuwa zikifanyika kwenye mfuko wa pembejeo. Kwa hiyo, kilichofanyika ilikuwa ni kubadili msimamizi. Sasa huu ni msimu wa tatu toka makubaliano hayo yafanyike na sheria hii ibadilishwe, bahati mbaya sana hii fedha haijarudi kwenye zao la korosho, haiendi kabisa. Hili ni la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, baada ya hii fedha kuchukuliwa, uzalishaji wa korosho ukashuka kutoka tani 320,000 ukaenda mpaka tani 200,000 na kitu, kwa maamuzi tu haya ya kuchukua huu mfuko. Baya kuliko yote, badala ya kurudisha hii fedha kwa wakulima, kilichofanyika, msimu uliofuata moja ya kazi iliyokuwa inafanywa na hii fedha ilikuwa ni kugharamia utafiti na kuendesha Bodi ya Korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ikaleta mapendekezo, ikaweka tozo kwa wakulima shilingi 25/= ya utafiti na shilingi 25/= ya kuendesha Bodi ya Korosho, badala ya kutumia ile fedha waliyoichukua, ile fedha haikurudi na ule mzigo akarudishiwa mkulima. Kwa hiyo, mkulima anakatwa shilingi 50/= kwa ajili ya utafiti na kwa ajili ya kuendesha Bodi ya Korosho. Huu ni udanganyifu. Tulipoahidiwa hapa Bungeni tuliambiwa hii fedha ingeenda, lakini sasa huu mzigo amebebeshwa mkulima.

Mheshimiwa Spika, baya zaidi, sasa hivi yako mapendekezo mengine ya kugharamia pembejeo kwa kumkata mkulima shilingi 110/= kwa kilo. Ahadi iliyotolewa hapa ni kwamba hii fedha ya Export Levy ndiyo ambayo ingerudi kuja kugharamia. Sasa kwa mahesabu ya kawaida, mwaka 2018 iliingizwa shilingi bilioni 37, wakati huo mfuko haukufanya kazi kwenda kugharamia pembejeo. Serikali ilipata mapato shilingi trilioni moja na zaidi, kwa kuingiza shilingi bilioni 37 tu. Mwaka huu makisio ya uzalishaji ni tani 280,000 mpaka 350,000, tunahitaji shilingi bilioni 55 tu. Sasa kwa nini tunataka kwenda kumbebesha huu mzigo mkulima badala ya kuchukua ile fedha ambayo mlituahidi hapa kwamba itakwenda kutumika vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi bilioni 55, tunazalisha zaidi ya trilioni moja plus! Ni maombi yangu kwa Serikali, naomba sana; na bahati nzuri Naibu Waziri wakati ule tuna mgogoro huo wa Export Levy hapa, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na alituunga mkono. Ni matumaini yangu kwamba kwenda kwake Serikalini hakujambadilisha kuliona hili jambo kwa mtazamo sahihi, tuchukue fedha ya Export Levy turudishe iende kugharamia korosho ili Serikali mpate.

Mheshimiwa Spika, kushuka kwa uzalishaji kumemuumiza mkulima kwa sababu uzalishaji umeshuka, lakini kumeiumiza Serikali. Sasa siyo vibaya kurekebisha. Ni ombi langu kwamba Serikali ifanye marekebisho badala ya kwenda kumkata mkulima, chukueni fedha, shilingi bilioni 55 kati ya shilingi bilioni 200 au shilingi bilioni 300, rejesheni huku tukomboe zao la korosho lisife. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mfuko huu ulipoondolewa na Bodi ya Korosho ilivunjwa, huu mwaka wa tatu. Zao ambalo ndiyo linaloongoza kwa kuiingizia fedha nyingi za kigeni nchi hii kuliko zao lolote, mwaka wa tatu hakuna bodi. Mkurugenzi wa Bodi, yuko anakaimu.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya mimi nadhani Mkurugenzi amepewa kazi kubwa kuliko uwezo wake. Hii kazi imemshinda, mtafutieni kazi nyingine, tuleteeni Mkurugenzi mwingine. Kwa sababu huyu Mkurugenzi anakwenda kule, anafika mahali akibanwa na wakulima anaanza kutoa majibu ya kiburi kabisa. Sasa zao ambalo ndiyo linawaingizieni fedha; mwaka wa tatu huu kuunda bodi tu inashindikana; tuna lengo gani na zao hili? Hili zao likifa tunapata nini? Tuundieni bodi, tutafutieni Mkurugenzi mwenye uwezo, tutengenezeeni mambo.

Mheshimiwa Spika, la tatu, mwaka ule wakati tunaanza kuhamasisha kulipeleka hili zao mikoani, wako wananchi waliohamasishwa kutengeneza miche ya korosho; na kati yao kwanza wengi hawajalipwa, lakini kati yao walikuwepo Watumishi wa Umma. Mkoa wa Lindi wako saba, nchi nzima wako 24. Wameingia mkataba na Bodi ya Korosho.

Mheshimiwa Spika, maajabu kabisa, wameshazalisha miche imechukuliwa imesambazwa, wanaambiwa wao hawakutakiwa kuzalisha. Kwa nini mliingia nao mkataba? Kwa nini mmechukua miche yao? Why don’t you pay them today? Uharamu unapatikana baada ya kuchukua miche na kusambaza. Eti ni Watumishi wa Umma! Kwani Mtumishi wa Umma akizalisha akapata hela ya ziada, dhambi iko wapi? Mimi nadhani hii ni roho mbaya tu ambayo haina sababu. Tengeni fedha, walipeni hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mapendekezo yangu, msimu huu ambao pengine muda wa kurekebisha sheria unaweza ukawa haujafikia na bahati nzuri Kamati imependekeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Malizia kwa sentensi moja.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, naipongeza Kamati kwa kupendekeza jambo hili, mfuko wa kuendeleza zao la korosho urudishwe. Kabla haujarudishwa, tupeni shilingi bilioni 55 mkalipie pembejeo, ile iliyobaki rekebisheni.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)