Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na pia namshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunifikisha siku ya leo niweze kuchangia WIizara muhimu si kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa peke yake bali Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, toka nimeingia kwenye Bunge hili, Wizara ya Kilimo kila ilipowasilisha bajeti yake nimechangia toka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuzungumza niwashukuru sana kwa sababu hotuba zao zote wanapowasilisha huwa zinakuwa nzuri ila shida inakuwa kwenye utekelezaji wa hizo hotuba zao ambazo wanazileta ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaanza na Mkoa wangu wa Rukwa, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikao inayozalisha zao la mahindi kwa kiasi kikubwa sana lakini leo Mkoa wa Rukwa tunaliona zao la mahindi ni kama zao la laana kwenye Mkoa wetu wa Rukwa. Pamoja na kwamba ni Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini na mikoa mingine Tanzania inayozalisha mahindi ningependa kujua hapa kwenye hotuba yako umezungumza kidogo sana Mheshimiwa Waziri. Kama zao la mahindi ni zao ambalo kwa sasa mmekosa ufumbuzi wa soko njooni na zao mbadala wananchi waachane na mahindi; wanatumia gharama kubwa kununua pembejeo na haiendani na bei halisi ya mahindi tunayolima sisi watu wa nyanda za juu kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo mwananchi anakwenda tena kuvuna mahindi ya mwaka huu wakati msimu uliopita mahindi yapo ndani. Natambua kwamba Serikali haiwezi kuwapangia bei lakini ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha wananchi wake wanapata masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo ningependa Wizara mnapokuja mtuambie ile mbegu ya mahindi inayotoka Zambia kama mmeiona ndiyo mbegu bora waambieni Watanzania na wakulima wa zao la mahindi wajue kwamba mbegu ile ndiyo inayostahili kwa sababu leo kama kweli wanafanya tafiti Wizara ya Kilimo, mbegu inayotumika na inayopendwa Zaidi ya wakulima wa nyanda za juu kusini ni mbegu inayotoka Zambia. Leo wakiamua kufanya jambo lolote mkumbuke kwamba tupo kwenye ushindani wa masoko, mnategemea wakulima wa Tanzania watakuwa kwenye hali gani. Ni vizuri mkafanya tafiti na mje na mkakati wa ziada kwenye jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi mbegu hizo zinapitishwa kwenye njia za panya. Serikali pamoja na kwamba Wizara ya Kilimo mnashirikiana na Wizara mbalimbali hapa kwenye majukumu yenu ni pamoja na kulinda hali ya wakulima pamoja na mbegu.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida kuna maazimio mbalimbali ambayo kama Watanzania tumeshiriki, Azimio la Maputo ya Nchi za Afrika la mwaka 2014 pamoja na nchi yetu ilishiriki ambapo maazimio yalifanyika kwenye kwa nchi zote za Bara la Afrika. Katika maazimio hayo ilikuwa ni pamoja na kuweka mahususi Sera za Kilimo ambazo zitaenda kuondoa umaskini kwenye Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia kwenye utekelezaji wa bajeti zetu na hayo maazimio ilikuwa ni kufikia mwaka 2025, leo tupo 2021. Nitatoa mfano tu kwenye utekelezaji wa bajeti, miaka mitano mfululizo bajeti ya mwaka 2016/2017 ilitekelezwa kwa asilimia 2.22, 2017/2018 asilimia 11, 2019/2020 asilimia 15 na 2020/2021 asilimia 26.46. Kwa maana hiyo miaka mitano imetekelezwa kwa wastani wa asilimia 19.3. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maana nyingine miaka mitano Wizara ya Kilimo utekelezaji wa bajeti pamoja na kwamba tunatenga lakini imeweza ina maana kwamba asilimia 80.7 bajeti hii utekelezaji wake imeshindikana kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kutenga bajeti lakini ni wajibu wa Serikali kupeleka fedha kama Bunge lilivyotenga. Na hapa kumekuwa na changamoto, kutenga bajeti ni jambo moja na utekelezaji wa bajeti hiyo ni jambo linginge. Tumekuwa na kauli mbiu nyingi Kilimo ni Uti wa Mgongo, kilimo sijui ni kitu gani sisi hatuna shida na slogan, tuna shida na utekelezaji wa kilimo. Na kama kweli lengo ni kuwasaidia vijana wa nchi hii, tunawezaje kutekeleza suala hilo kwa kupeleka fedha kama hizi kwenye maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine, mbegu hiyo ambayo leo kaka yangu Mheshimiwa Mhagama alisema katika vipaumbele vyenu vya Wizara kwamba ni vizuri mngeanza na masoko. Narudia tena katika michango yangu yote ya miaka yote pamoja na kutafuta masoko, lazima tuwekeze kwenye utafiti kwenye suala la kilimo. Hauwezi kutafuta masoko kama mbegu zako asilimia 60 ya Taifa hili ya mbegu tunaagiza kutoka nje, haiwezekani. Tunaingiaje kwenye ushindani wa masoko kama mbegu ndo hizi asilimia 60 unategemea kutoka nje, tunaaminije wale watu wa nje watafanya sisi tuongoze kwenye biashara kwenye mazao tunayolima wakati wao ndio wanatuletea sisi mbegu kwa asilimia 60. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba mnajitahidi, Waziri na Naibu wako lakini mtajitahidi kama mnapewa fedha kama tunavyokuwa tumetenga ndani ya Bunge. Haitawezekana kwa maneno matupu kufikia malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kupitia Ripoti ya CAG kuna mambo kadhaa ambayo yamezungumzwa pale na katika mambo hayo ni pamoja na udhibiti mbovu wa mbegu na pembejeo kutoka kwenye Wizara yako. Sasa kama malengo ni kusaidia Taifa letu, hatuwezi kushindwa kudhibiti tukategemea malengo/matokeo chanya kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, ni vizuri kama kweli tunaamini kipaumbele kitakwenda kukomoa umaskini wa Taifa letu, tuweke kilimo kama kipaumbele kwa kuwapatia fedha, pembejeo lakini tukawekeze kwenye tafiti kwa kupima udongo kama nyanda za juu kusini imeshindikana mahindi, tujue ni zao gani ambalo tutapeleka iwe mbadala wa mahindi lengo tu ni kuondoa umaskini na kuwasaidia wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia pamoja na hayo, wakulima hawa wana hali ngumu sana. Tunapozungumzia mikopo ya kilimo, hiyo Benki ya Kilimo hebu mje siku moja mtuambie hapa mikoa hii ambayo inazalisha sana ni wakulima wangapi wamenufaika na mikopo inayotokana na Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna danadana nyingi lakini ukiangalia maneno kwenye hotuba mbalimbali inaonesha kabisa fedha zinatoka, zinakwenda, zinakwenda kwa nani mbona hatuyaoni matokeo kwa wakulima wetu kama kweli wanapewa hiyo mikopo? Kuna mazingira ambayo lazima tubadilishe pamoja na kwamba vipaumbele vinakuwa vingi, tuje na kipaumbele kimoja ambacho lengo ni kumkomboa mkulima na Mtanzania, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)