Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. JENEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yake kwa kazi nzuri mnayoifanya kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Spika, nijikite kwenye block farm katika mazao ya kimkakati. Tunajua wana mazao ya kimkakati kila mkoa. Mathalani zao la kimkakati la Dodoma tunajua ni zabibu na alizeti, lakini kama tungetafuta block farm, tukawagawia wakulima, tukaweka miundombinu mizuri pale, itawasaidia sana hawa wakulima kuweza kuwakopesha hata mikopo ya kuendeleza kilimo na kuwapa wataalamu wa kuwasaidia katika kilimo kile. Kwa sababu watakuwa wako pamoja, wanahudumiwa kwa pamoja na wanaweza tukazalisha vya kutosha kwa kutumia block farm. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizo block farm zitatusaidia kupata masoko kwa sababu, patakuwa panafikika kwa wale wateja wanaohitaji kununua mazao yetu. Tuna imani tutakuwa tumeweka miundombinu ya kutosha ya barabara, tutakuwa tumeweka wataalamu wa kuweza kuwasaidia watu kwenye kuuza mazao, tutakuwa tumepafanya mahali ambapo ni pa soko la kuweza kuuza mazao yetu haya. Kama hatukufanya hivyo, kwa kweli tutakaa kwenye kilimo cha ndoto ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi wakati unasainiwa Mkataba wa Mafuta, Kiongozi Mkuu wa Nchi ametuambia, Tanzania tukitaka kuendelee tuwekeze kwenye kilimo cha biashara, kwenye nishati na kwenye miundombinu. Sasa ifike wakati basi, tuone hizi block farms ndiyo za kututoa mahali tulipo. Hii ya kumfuata mkulima mmoja mmoja, tutachelewa kwa sababu, kwanza wataalamu wa kutosha hatuna, miundombinu kuwafuata wakulima huko waliko, ni ngumu zaidi na uwekezaji wake utakuwa mkubwa zaidi, lakini tukiwaweka pamoja, tukawahudumia kwa pamoja tunaweza tukatoka hata kwenye sakata hili la ukosefu wa mafuta, ukosefu wa masoko na wakulima wetu wakapata thamani ya kile wanachokilima.

SPIKA: Mheshimiwa Jenejelly, mnaposema block farm mnamaanisha nini?

MHE. JENEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ninaposema block farm naamisha hivi, kwa mfano Dodoma kuna ardhi ya kutosha, kwa hiyo, Serikali iende pale impimie kila mkulima. Kwa mfano, kama ilivyo Singida, katika zao la korosho wamepimiwa na kila mkulima ana sehemu yake, ana eka zake za kulima, lakini wote wako kwenye sehemu moja ambayo ni rahisi wataalamu kuifikia, ni rahisi kupata pembejeo, ni rahisi kutengeneza miundombinu ya pale na ni rahisi kutafuta soko la mahali pale kwa sababu wako sehemu moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo ilikuwa maana yangu. Hilo ndilo litakalotutoa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tukienda kwenye kilimo cha umwagiliaji, nacho tuangalie ambapo tumeweka miundombinu ya umwagiliaji na hawa wakulima nao ziwe ni block farm, wawekwe kwa pamoja. Tumeona hapa Tume ya Umwagiliaji tunaambiwa imefikia wakulima 714, bado tuko mbali sana; kwa nchi nzima kufikia wakulima 714 wakati tunasema asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, bado tuko mbali sana. Najua Waziri na Naibu wake na timu yake mnajitahidi sana, lakini tuendelee kujitahidi.

Mheshimiwa Spika, haya yote yatafanyika wakipelekewa bajeti yao ya maendeleo kama tunavyoipitisha leo. Wanajitahidi sana, lakini wanakwama kwa rasilimali fedha, hatujawa serious kwenye kilimo kama tulivyokuwa kwenye miundombinu ya barabara. Ukiangalia bajeti ya miundombinu huwa inapelekwa asilimia 80 mpaka 70, lakini ukienda kwenye kilimo, tumeona wanapelekewa asilimia 18, 19, 20 au 26; hawawezi kufanya chochote. Kila siku tutamlaumu Waziri wa Kilimo, Naibu wake na wataalamu wake, lakini hatujawawezesha kwenye rasilimali fedha tukaweza kufanya kilimo kiweze kuwa uti wa mgongo kama kweli tunavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu. Tukijikita kwenye hilo tutakwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)