Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kufungua dimba katika uchangiaji wa hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Naomba kuchukua fursa hii kwanza kumpongeza Waziri, Mheshimiwa William Vangimembe Mwalukuvi. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt Angelina Mabula na wataalam wao wa Wizara. Nimpongeze pia Katibu Mkuu wa Wizara hii, dada yetu Mary Makondo, ambaye pamoja na sifa za kiutendaji lakini ana sifa ya unyenyekevu ambayo ni sifa muhimu sana kwa utendaji wa kazi za Serikali. Vile vile nimpongeze Naibu Katibu Mkuu Nico Mkapa na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwenye maeneo matatu, eneo la kwanza ardhi ni rasilimali ambayo kama itapangwa na kutumika vizuri ina uwezo mkubwa wa kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwenye Taifa letu. Utaona kwenye mwaka wa fedha uliopita Wizara ilikadiria kukusanya bilioni 200 na mpaka hivi tunavyozungumza zaidi ya shilingi bilioni 110 zimekusanywa kwenye halmashauri zote za nchi nzima, tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa hapa ni fedha hizi zinavyokusanywa, uwekezaji wake unaorudi kwenye Wizara kuwekeza katika upimaji wa ardhi ni mdogo sana. Ukisoma bajeti ya mwaka wa fedha uliopita pamoja na fedha za nje, kwenye fedha za ndani Wizara ilitengewa shilingi bilioni 16 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hata hivyo, mpaka Waziri anawasilisha hotuba yake ya bajeti ni shilingi bilioni tano tu ndiyo zimepelekwa kwenye Wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 30.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni Mwalimu na moja kati ya wanafunzi wako umemtambulisha hapa asubuhi asilimia 30.9 kule shuleni ukiipata kwenye mtihani nadhani tutakubaliana supplementary. Ninachoomba kusema, lazima Serikali itenge fedha za kutosha kwenye Wizara hii ili Wizara iweze kutekeleza wajibu wake wa kupanga matumizi ya ardhi na kupima ardhi. Mpango huu na upimaji huu utakuja baadaye kuwa mapato makubwa kwa Serikali kwa mapato ya land rent. Kwenye Jiji la Dar es Salaam mpaka hivi tunavyozungumza tayari bilioni 5.6 zimekusanywa kati ya malengo ya bilioni, 11 ni kazi kubwa, lakini zitakusanywa zaidi kama maeneo mengi zaidi yatapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, mimi nilikuwa Meya pale Ilala kabla halijawa Jiji la Dar es Salaam. Nilikaa miaka mitano nakaimu Mkuu wa Idara Mipango Miji. Nimeondoka miaka mitano kuna Kaimu Mkuu wa Idara hivi nimerudi kwenye Ubunge bado kuna Kaimu Mkuu wa Idara. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu am-confirm mtendaji yule aweze kufanya kazi hizi akiwa tayari amethibitishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ninalotaka kuchangia, ni eneo la urasimishaji. Kutokana na bajeti finyu na uwezo unaofanya Wizara iwe na uwezo mdogo wa kupima, Serikali mwaka 2015 ilianzisha zoezi la urasimishaji kwenye maeneo mengi ya mijini kwenye Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye Jiji la Dar es Salaam, kwenye Jimbo la Ukonga inafanyika kazi ya urasimishaji. Pale Jimbo la Ukonga yako makampuni 24 kwenye mitaa 64 kwenye Kata zote 13 za Jimbo la Ukonga, kuanzia Kitunda, Mzinga, Kivule, Kipunguni, Ukonga, Gongolamboto, Pugu, Pugu Station, Buyuni, Zingiziwa, Chanika na mpaka Kata ya Msongola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, zoezi hili linasuasua. Ukisikiliza hotuba ya Waziri ziko hatua wameanza kuzifanya. Nimpongeze Waziri, Waziri wetu wa Ardhi ni mtu mwepesi na anajituma sana katika kazi ya ardhi, maana kazi yenyewe hii haitaki sana kukaa ofisini. Tulipata tatizo pale Kata ya Kivule na upimaji wa kile Chuo cha Ardhi Morogoro nilimwambia Waziri na alifika kutatua tatizo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile juzi Naibu Waziri amekwenda Chanika kutatua matatizo haya ya urasimishaji. Nimeona kwenye hotuba ya Waziri wanachukua hatua, lakini tukumbuke kampuni hizi zimechukua pesa za watu, hatua za kuzisimamisha, hatua ya kuzifungia upimaji, hazitasaidia Mtanzania aliyechanga fedha zake kwenye Jimbo la Ukonga na maeneo mengine kupata upimaji wa eneo lake. Nimwombe Mheshimiwa Waziri katika kuhitimisha aje atueleze nini mpango sasa wa kusimamia kampuni hizi ili Watanzania waweze kupimiwa ardhi zao, wapate hati milki, waweze kumiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ninaloomba kuchangia ni migogoro ya ardhi; migogoro ya mipaka katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Naomba nijikite kwenye eneo moja tu la migogoro ya mipaka baina ya hifadhi mbalimbali na vijiji na maeneo yetu tunayotoka. Kule Ukonga uko mgogoro wa kudumu baina ya Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Jimbo la Ukonga wa Kata za Buyuni, Chanika na Zingiziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, maana leo nilikuwa nimeshapanga kabisa jioni hapa, siyo kwa kuwa jana alisikia wachangiaji wachache angedhani bajeti ingepita kirahisi. Nilipanga leo jioni niwaombe Wabunge tushike shilingi kwenye eneo hili, lakini nimpongeze Waziri kwenye hotuba yake ameelezea vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, The Land Survey Act, Sura ya 324, inampa Mkurugenzi wa upimaji na Ramani mamlaka ya kusimamia upimaji na kutatua migogoro yote ya mipaka. Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 68 ameeleza vizuri na kwenye ukurasa wa 69, naona amelimaliza tatizo hili na naomba nimnukuu Waziri anasema:
“Ni marufuku kwa Idara au Taasisi yenye migogoro kwenda yenyewe uwandani kutafsiri GN zao bila uwepo wa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani ambaye ndiye mhusika mkuu. Aidha Viongozi wa Mikoa, Wilaya lazima washirikishwe wakati wote mipaka inapohakikiwa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni marufuku kwa idara yoyote ama taasisi kwenda kunyanyasa wananchi na kujitafsiria GN zao wenyewe. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Ndumbaro marufuku, Mheshimiwa Naibu Waziri Mary Masanja marufuku, siyo maneno yangu, maneno ya Waziri mwenye dhamana ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maelezo yake Waziri ametoa wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, maana wengine ni mabingwa kuweka watu ndani, sasa hawa ndiyo wa kuwaweka ndani, hawa wanaokuja kutafsiri GN zao wenyewe na migogoro ya mipaka na kunyanyasa wananchi wetu.
T A A R I F A
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jerry Silaa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Charles Mwijage
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa mzungumzaji MCC mstaafu kwamba unapotoa taarifa, wale unaowapa taarifa hawapo, tatizo la maliasili hifadhi ndilo tatizo la mifugo ninalolipata kwangu kule, lakini unaowaambia hawapo hawawezi kuelewa unavyopata uchungu, hawapo hapa.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge nimeshasisitiza mara kadhaa, Serikali ipo Bungeni na ndiyo maana mnazungumza na mimi, yaani kama kuna mtu yeyote wa Serikali ambaye jambo linamhusu limezungumzwa hajaelewa vizuri hata kama yupo humu ndani ataelezwa vizuri, ni jambo gani limezungumzwa kuhusu yeye. Kwa hiyo msiwe na wasiwasi na michango yenu mnayoitoa, Serikali iko Bungeni.
Mheshimiwa Jerry Silaa, malizia mchango wako.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mwijage, kaka yangu, mtaalam wa propaganda, sisi wataalam wa sheria hapa tuna address the chair, tunaongea na kiti na ujumbe utafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ni eneo la uthamini. Niseme tu kwamba, Wizara ya Ardhi inafanya kazi yake ya uthamini vizuri sana chini ya Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, mama yetu Evelyn Mugasha. Nafasi hizi zenye mambo ya hela hela ama za uadilifu uadilifu, wanapokaa akinamama wanazifanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kitu kimoja, naiomba Wizara ambayo ndiyo wataalam wa masuala haya, waishauri vizuri Serikali. Kulikuwa kuna wakati tunatumia sport valuation kuweza kupata bajeti ili idara ama taasisi inayotaka kufanyiwa uthamini iweze kutenga fedha, lakini tumeona mara nyingi uthamini unafanyika lakini kumbe hata hiyo taasisi inayoagiza uthamini hata fedha kwenye bajeti haijatengewa. Matokeo yake uthamini unafanyika, fidia zinachelewa na wananchi wetu wanapata shida sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iweke utaratibu mzuri wa kufanya uthamini na kulipa wananchi kwa wakati. Ili hili lifanikiwe lazima wakati uthamini unafanyika tayari bajeti iwepo na fedha ziwe zimeshatengwa. Maeneo mengine wawe wanaaminiana, hawawezi wakafanya uthamini ukaidhinishwa, wakaanza uhakiki, ukakamilika, ukaja uhakiki mwingine wakati wananchi wanasubiri fidia zao, ile miezi sita ya kisheria inapita, hela za riba hazipo, tunaanza tena kurudi nyuma na wananchi wanapata shida kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nirudie tena kuipongeza Wizara, inafanya kazi nzuri hasa katika kujikita kuingia kwenye mifumo ya TEHAMA. Tukienda hivi nchi yetu itapata tija kubwa kwenye sekta ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)