Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kumshukuru Mungu kunipatia nafasi ya pumzi na kuniwezesha kuchangia mchango kwenye Wizara hii ya Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze watumishi hawa kwenye Wizara ya Ardhi, nikianza na mwenyewe Waziri Mheshimiwa Lukuvi, Mheshimiwa Angelina Mabula dada yangu Mary, Stella, Nico na wengine kwa kweli kwenye Wizara hii. Napongeza kwa sababu moja kubwa sana, Wizara wamejitahidi sana katika eneo hili la ardhi wana eneo kubwa sana. Migogoro ilikuwa mingi sana na mimi nimeishuhudia katika maeneo yangu mengi na niwashukuru sana kwanza kwa kulinda, kwa sababu gani nasema hivi? Ni kwa sababu ardhi imebaki kama rasilimali pekee ya Mtanzania aliyobaki nayo na urithi mmojawapo ni ardhi katika eneo letu hasa la kule vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwapongeze sana watumishi hawa kwa huku juu kama Wizara yenyewe kwa sababu wamejitahidi sana. Yuko mtangulizi amezungumza habari ya haya makampuni, nimsihi Mheshimiwa Waziri, yako mengi ambayo ameyafanya na Wizara yake, lakini machache yanaleta shida. Kwanza niliweke wazi hili kabla sijamiminika vizuri, haya makampuni ambayo kwa kweli yanakwenda kurasimisha, mara nyingi hayatumii sheria kwa jinsi Wizara ilizoziweka na hayafuati taratibu na hayasubiri miongozo ambayo wameweka Wizara kama Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mifano michache, ukiangalia wanavyokwenda kwenye halmashauri zetu, wakifika kule, kwa mfano halmashauri kama ya kwangu ina watumishi wachache wa Idara ya Ardhi na pengine hakuna kabisa. Kwa hiyo, baadaye nitampa Waziri ombi lakini aangalie haya makampuni, ushauri wangu kwake na kwa Serikali waunde Kamati ya Kisekta ambayo itasaidia kusimamia hawa warasimishaji ili walau waweze kupanga maeneo yetu vizuri. Nasema hivyo kwa sababu gani? Tanzania kama nchi lazima sasa nchi ipimwe yote na ikipimwa yote migogoro hii itaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingi inasababishwa kutokana na kwamba maeneo mengi hayajapimwa, lakini siyo hiyo tu maeneo mengi yakipimwa na yakapimwa kwa uhakika, maana yake ni kwamba hata Serikali itajipatia pesa kwa kutoza kodi ya maeneo yote yaliyopimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sasa hivi kila kampuni ina-charge kadiri inavyoona, iko nyingine ina-charge 150,000, nyingine 200,000 nyingine 100,000, lakini sasa basi Serikali ione namna gani ya kufanya, iwawekee utaratibu haya makampuni yanayopima ili utaratibu ule uonekane na sisi wawakilishi tujue kabisa kwamba wanapima kwa kiasi hiki na iwe kama formality ili hata mwananchi anapotakiwa kupima eneo lake ajue kipande chake anapimiwa kwa namna gani na kama ni kiwanja au chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niwapongeze sasa Wizara kweli kweli, kwa sababu wametoa mikopo kwenye halmashauri kadhaa na Mheshimiwa Waziri amesema sita zimefanya vizuri na zimerejesha hela. Nimwombe Waziri waendelee kuzikopesha halmashauri ili maeneo mengi yaendelee kupimwa, wasije wakakata tamaa kwa sababu halmashauri zingine hazikulipa. Niombe Wakurugenzi wale anmbao wamekopeshwa hizi hela na maeneo yao yamepimwa na wamepata faida kutokana na kupimwa kwa ardhi hii, basi nao warudishe hizo fedha ili halmashauri zingine zipate mikopo ambayo haina riba, wakapime maeneo yao. Ikiwa hivi basi ni wazi Serikali itapata mapato, lakini siyo hiyo tu migogoro itakuwa imepungua na miji yetu mingi itakuwa imepimwa. Siyo hilo tu, unapopima miji hakuna tena sababu ya kwenda kufanya urasimishaji kwa sababu miji ile imekwishapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba nitoe mchango wangu katika Mabaraza ya Ardhi. Niishukuru kwanza Serikali imeanzisha baraza katika jimbo langu na Wilaya ya Mbulu. Bbaraza linafanya vizuri sana na linasaidia kutatua kero hii ya ardhi, lakini wana changamoto chache; ya kwanza baraza halina namna ya kwenda kutembea.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mheshimiwa Waziri ikimpendeza aone namna gani ya kuanzisha haya Mabaraza yatembee yawe mobile zile mahakama zao zitembee, zikaone, maana wakati mwingine hazina namna ya kwenda kwenye maeneo zikaona, ni kweli kwamba hii ardhi ni ya fulani, hii ardhi ikoje kabla ya kutoa hukumu? Niombe pia wasitumie technicality za kisheria kabisa kutoa haki, waangalie vizuri namna ya kuhukumu kwamba haki iko wapi zaidi kuliko kutumia technicality. Niishukuru sana Wizara imeanza kutoa hukumu Kiswahili, kesi inasikilizwa Kiswahili na hili niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana leo napongeza Wizara hii kwa sababu wananchi wetu kule wanapotoa hukumu wanasikiliza na wanakuwa wanajitetea bila kuwatumia hawa Wanasheria ambao mara nyingi walikuwa wakiwadanganya. Kubwa zaidi sasa katika maeneo haya, muwasaidie hao Wazee wa Baraza wawe na posho za kutosha…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei, Mawakili wanawadanganya wale wanaowawakilisha ama? Maana umesema walikuwa wanatumia Wanasheria ambao walikuwa wanawadanganya, kwani sasa hivi wakitumia Kiswahili wanajisimamia wao wenyewe unataka kumaanisha hivyo?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Ndiyo ukweli.
NAIBU SPIKA: Kwa hiyo Mawakili ni waongo?
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kusema Mawakili wote ni waongo hapana, kwenye mahakama hasa hizi za Baraza la Ardhi wako wengine wanajifanya ma-bush lawyer, hawana hata hizo taaluma.
NAIBU SPIKA: Sasa ngoja, tufafanue vizuri, kuna tofauti ya mtu ambaye ameamua kukupa wewe ushauri ambaye siyo Wakili, wala siyo Mwanasheria. Sasa ukisema walikuwa wanadanganywa na Wanasheria yaani hapo maana yake ni kwamba kimsingi sheria… (Kicheko)
Wanasheria humu ndani wataandamana isipokuwa mimi, sasa hiyo kauli hiyo iweke vizuri kidogo.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, basi niifute kabisa, najua wewe ni Mwanasheria na naelewa angle unayozungumzia.
NAIBU SPIKA: Ngoja ngoja unampa taarifa Mheshimiwa Flatei Massay au mimi?
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa anayezungumza.
NAIBU SPIKA: Basi ngoja tulimalize kwanza hili halafu nitakupa nafasi. Mheshimiwa Flatei ulikuwa unataka kusema point moja hivi sijakuelewa, hii ya pili uliyokuwa unasema kwa kuwa mimi ni Mwanasheria...
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, najua nini maana ya Mwanasheria, haya nilikuwa nataka kupongeza Wizara hii ielewe kwamba kwa sababu wananchi wetu kule hata kuweka hao Wanasheria zile gharama zinakuwa kazi kubwa sana, kwa hiyo kumtafuta mwanasheria proper kama wewe ni kazi sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Nadhani hoja imeeleweka, hoja ya gharama ni tofauti na hoja ya wale watumiaji wa hizo huduma za Wanasheria kudanganywa.
Mheshimiwa Olelekaita.
T A A R I F A
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nataka tu nimpe mzungumzaji taarifa kwamba, mawakili hatuendi kwenye Mabaraza hayo anayozungumza, kwa hivyo kama wananchi wamedanganywa huko basi watakuwa ni watu wengine lakini siyo Mawakili.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatei Massay.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipokea taarifa kwa sababu ni rafiki yangu na isitoshe ni Mbunge mwenzangu na tunatoka Manyara wote, naipokea sana taarifa hii wala asiwe na wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuipongeza Wizara hii naomba niendele na mchango wangu. Kwa hiyo, Wizara inajitahidi sana na kwa kuwa sasa nimeomba kwa Mheshimiwa Waziri, wale Wazee wa Mabaraza, Wenyeviti wa Mabaraza wawasaidie basi wawapatie ajira za kudumu, ili mtu awe na hakika na ajira yake. Mtu anapokwenda kufanya kazi ile kubwa ya kutoa haki mahali fulani pia anatakiwa awe na security ya kutosha. Wakati mwingine anajua kabisa ajira yake inakwisha baada ya muda fulani au kwa miaka mitatu, kwa hiyo haimpi ile hali ya kujiona yeye ni mfanyakazi katika eneo hili la kutoa haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali iwape hawa Wenyeviti ajira ya kudumu kwa sababu sasa hivi nadhani ajira zao siyo za kudumu. Pia niombe pia hawa Wazee wa Baraza, nao pia waangaliwe kwa namna Fulani, waletewe bajeti hapa na katika hiyo bajeti wapewe fedha ambazo zitaonyesha kabisa kwamba kweli fedha hii inaweza ikawa kama posho ya kawaida kabisa kulikoni sasa hivi ilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa, niwashukuru pia kwasababu wamefanya kazi nzuri, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Stella huyu ambaye kwa kweli amekuwa akisimamia Mabaraza haya ya Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kama ushauri tu niombe Mheshimiwa Waziri aangalie kanuni katika Mabaraza haya, pawepo na namna rahisi ya kusaidia, kesi zinapoanza pawe na utaratibu ikiwezekana kesi zianze kwenye Kijiji, iende kwenye kata, lakini baadaye iende kwenye Mabaraza ya Wilaya. Kwa nini ninasema hivyo? Mtu mwingine anaweza kuwa na uhuru, akaenda kufungua kesi kwenye Baraza la Wilaya ambako anajua kabisa yule Hakimu au Mwenyekiti hawezi kuja kwenye eneo ilipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utoaji wa haki ule mtiririko na kesi ilivyoendeshwa inakuwa hawezi kujua kwa sababu yule Mwenyekiti hawezi kwenda site kuona hali hii ilivyo. Kesi ikianzia kwenye kijiji ni rahisi kujua kwamba kijijini wameamuaje, Baraza la Kata limeamuaje. Kwa hiyo ni rahisi kwa Mwenyekiti kuamua namna gani ya kutatua mgogoro huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, niombe Mheshimiwa Lukuvi, iko migogoro ambayo Mheshimiwa Waziri anaweza kuitatua, migogoro iko Manyara mingi hasa ya Mkoa kwa Mkoa, Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa kengele ya pili imeshangonga.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)