Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi. Mimi nina msemo wangu mmoja huwa nasema, mtu ukiwa mnafiki ukiwa kijana, ukizeeka lazima utakuwa mchawi, na mimi kwa sababu sina mpango wa kuwa mchawi kwenye uzee wangu, napenda nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, William Lukuvi; Naibu wake Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Makamishna wote kwa kazi kubwa wanayofanya kwenye Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa changamoto za Wizara hii ukiona wachangiaji wachache maana yake changamoto nyingi zimefanyiwa kazi, tumebaki na sisi wachache ambao tunadhani pia watatusikiliza, watakwenda kuzimaliza ili huko mbeleni changamoto zisiwepo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kwenye masuala mahsusi kwa sababu yale maswala ya kijumla jumla sijui kuna mgogoro mpaka kati ya mtaa na mtaa, sijui kata na kata hayo siwezi kuzungumza kwa sababu ule ni mipaka ya kiutawala tu, haikuzuii kununua ardhi mahali popote, haikuzuii kufanya shughuli zako. Kwa hiyo ni masuala ambayo yatamalizwa huko kwenye ngazi ya mitaa, ngazi ya kata, wilaya na mikoa, hapa tunazungumzia masuala mahsusi ambayo tunadhani yanahitaji attention ya Wizara ili mambo yaweze kuwa rahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la kwanza; Arusha tuna mgogoro mkubwa sana wa ardhi ni mgogoro kati ya Jeshi letu la Wananchi na Kata za Mushono, Mlangalini na Nduruma. Ni mgogoro wa miaka mingi sana, lakini mgogoro ambao umeshika kasi mwaka 2012. Tunaishukuru sana Serikali, baada ya changamoto kuwa kubwa, Mheshimiwa Waziri Mkuu kipindi hicho alikuwa ni Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda, aliitisha kikao tarehe 20 Machi, 2012 kwa ajili ya kujadili mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kikao hicho maelekezo yaliyotoka. Katika maelekezo hayo pamoja na kuwa na maagizo kumi, lakini maelekezo ya msingi yalikuwa ni mawili. La kwanza, Jeshi irekebishe mipaka yake upya na kuacha eneo lenye mgogoro kwa wananchi; na la pili, Jeshi wapewe eneo la mlima ambapo wananchi hawana mgogoro nalo eneo hilo wapo tayari kulitoa. Maelezo haya ya Serikali yaliwasilishwa na Naibu Waziri Mheshimiwa Goodluck Ole-Medeye kipindi hicho, aliyafanya kwa wananchi tarehe 28 Machi, 2012.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyojitokeza pale Serikali ilikwenda mwaka 2012, ikabainisha baadhi ya maeneo ambayo wanadhani wanatakiwa waondoe watu wakaenda wakafanya uthamini mwaka 2012, wakaondoka zao. Mwaka 2012, 2013, 2014, 2015 mpaka 2019 na tunafahamu kwa mujibu wa sheria uthamini ukishafanyika ikipita miezi sita kuna interest kidogo inalipwa, ikifika miaka miwili inabidi ule uthamini ufanywe upya, lakini uthamini wa mwaka 2012, Serikali imekuja kurudi mwaka 2019 na kuwalipa watu kwa uthamini wa siku za nyuma ambao hautambuliki kwa mujibu wa sheria kwa sababu miaka miwili tayari ilishapita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kibaya zaidi mwaka 2015 Serikali ilikwenda pale na Mkuu wa Wilaya wa kipindi hicho na viongozi wengine wakawahakikishia wananchi kwamba, eneo hili Serikali haina interest nalo tena kwa hiyo, wananchi wenye maeneo yao wanao uhuru wa kufanya shughuli zozote. Wale wananchi wakaamua kuyauza yale, maeneo wakawauzia wadau wengine na wakati huo Serikali hiyo hiyo, ilishakwenda kutengeneza mchoro, kuna approved plan pale No. CAO/65/01/6 na wananchi ambao wanataka kujenga walienda kuomba vibali vya ujenzi wakapewa na halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walikwenda kwenye mitaa na vijiji wakapitishiwa, wamejenga mpaka magorofa, leo Serikali inakuja, inataka kutumia mabavu na kutaka kwenda kuwaondoa wale wananchi. Kosa lililofanyika hapo mara baada ya Serikali kurudi mwaka 2019, ikaja na orodha yao ile ile ya mwaka 2012, wakaanza kutumia nguvu na mabavu wanawarushia watu hela kwenye Mpesa na kwa njia nyingine ili mradi tu zile hela zilizokuja ziweze kwenda.
Mheshimwia Naibu Spika, badala ya kumlipa mwananchi ambaye anaishi pale kwa wakati huo na ambaye amejenga, wamekwenda kumlipa mtu ambaye alishauza na alishaondoka siku nyingi. Nadhani hapa TAKUKURU wana kazi ya kufanya kuwatafuta wale watu waliolipwa, warudishe zile fedha na Serikali ifuate maelekezo haya ya Serikali ambayo yalisimamiwa na Waziri Mkuu wa nchi hii, ili wale wananchi wabaki pale wafanye shughuli zao na kama kuna maelekezo mengine yoyote basi ni vizuri Serikali ikakaa chini na wahanga wale tutafute solution ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwenye jambo hili, kwanza, nimepata taarifa kwamba Mheshimiwa Waziri huenda akawa Arusha kwenye ziara ya kikazi wiki ijayo, tulikuwa tunamwomba Mheshimiwa Waziri akutane na wahanga hawa ili apate picha pana ya jambo hili na mwisho wa siku Serikali ifanye maamuzi kwa maslahi mapana ya wananchi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu la pili kwa Mheshimiwa Waziri, namwomba kwamba kama kuna mchakato wowote wa kutoa hati kwa Jeshi la Wananchi usitishwe hadi hapo mgogoro huu utakapohitimishwa na Serikali itakaporidhika na hali halisi ya mchakato mzima kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili, shida ya hii nchi kuna double standard, kuna maeneo mengine maamuzi yanafanyika very fast, kuna maeneo mengine maamuzi yanafanyika kuangalia maslahi mapana ya nchi, kuna maeneo mengine kuna ku-delay. Yako mashamba ambayo hayajaendelezwa kwenye nchi hii ambayo Serikali imeyachukua, lakini kwa upande wa Jiji la Arusha kuna kigugumizi kikubwa sana, liko shamba la Bondeni City ambalo kwanza halijaendelezwa na mimi nina ushahidi na Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba halijaendelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na yeye tuliwahi kuhudhuria kikao kikubwa kabisa kilichoongozwa na Kiongozi Mkuu wa Nchi hii yeye akiwepo, Mheshimiwa Mhagama, Waziri wa TAMISEMI na Makatibu wao Wakuu na mimi nilikuwepo, maelekezo yalishatoka pale lakini kuna kwenda mbele, kuna kurudi nyuma. Ziko baadhi ya hatua zimechukuliwa, kwanza, lilitakiwa lipatikane eneo mahususi kwa ajili ya kujenga stendi, kwenye hili Waziri nampongeza sana kwa sababu, eneo limeshapatikana na Wizara ya TAMISEMI kupitia TACTIC imeji-commit kutoa fedha, pale tutajenga stendi ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu kwa Mheshimiwa Waziri, hili jambo alipe uzito unaostahili, tunaomba hili jambo sasa aende akalihitimishe, tunaomba hili jambo ajiridhishe kwa sababu kwanza taarifa ziko kwamba mmiliki mwenyewe kwanza sio raia wa Tanzania, taarifa zipo pia mmiliki mwenyewe ameshakufa, taarifa zipo kwamba halmashauri waliingia makubaliano ya kiujanjaujanja na yule mwekezaji ya hiyo asilimia tano, eti Jiji asilimia tano yule mhusika asilimia 95.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupigwa mkwara wakabadilisha, ikawa Jiji asilimia 10 yule asilimia 90. Sasa hivi tena wamepigwa mkwara mwingine tena wanasema Jiji asilimia 50 yule mwingine asilimia 50, huu ni utani, kwa sababu, Jiji la Arusha tuna changamoto kubwa ya ardhi, tumetenga fedha kujenga vituo vya afya, kujenga shule na maeneo mengine ya maendeleo. Tulikuwa tunaomba Serikali ikasimamie jambo hili kwa haki na kwa mujibu wa sheria na ikiwezekana hiyo ardhi irudi Serikalini ili maeneo ambayo hakuna shule tukajenge. Maeneo hakuna vituo vya afya tukajenge na mambo mengine yaweze kuwa mazuri zaidi. Tunamwomba Waziri mwenye dhamana ya ardhi aingilie kati ili mgogoro huu uhitimishwe kwa mujibu wa sheria na tufanye masuala ya maendeleo badala ya kuanza kunung’unika na kuzua masuala mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwangu la tatu ni kuhusu urasimishaji. Tuna dhamira nzuri sana, lakini kama kuna zoezi ni kichefuchefu ni urasimishaji. Tuna Kata pale kama ya Sekei, kuna Kata ya Balaa, Kata ya Lemala na Kata nyingi za Jiji la Arusha ambazo watu wamekwenda kufanya zoezi la kurasimisha, wamechukua fedha za watu na zoezi halijakamilika, zaidi ya mwaka umeshakwenda. mambo haya hayatoi sura nzuri kwa Serikali, Mheshimiwa Waziri Lukuvi ni mtu anayefanya kazi kwa weledi sana, watendaji wake wanaendana na kasi yake vizuri sana, heshima aliyoijenga kwenye nchi hii ni kubwa sana, lakini hili la urasimishaji litampunguzia umaarufu kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu atakapokuja Arusha tukutane pia na viongozi wanaotoka kwenye Kata zote zinazofanyiwa urasimishaji, ili tumweleze changamoto halisi na yeye kama Waziri mwenye dhamana na timu yake waende wakatutafutie majawabu ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kwa heshima na taadhima naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)