Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kwa jioni ya leo na kuwa mchangiaji wa kwanza. Nampongeza Waziri wa Ardhi na Naibu wake dada yangu Mheshimiwa Angelina kwa kazi nzuri wanazozidi kuzifanya pamoja na watendaji wote wa Wizara na Katibu Mkuu dada yangu Mary Makondo. Nawapongeza sana kwa ajili ya kazi zote wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika changamoto zilizopo katika ardhi. Migogoro ya ardhi imekuwepo mingi na haiishi. Sababu mojawapo ni hawa wazee wa Mabaraza ya Ardhi. Wananchi wanyonge wamekuwa ndiyo victim wakubwa. Hawa wazee wa Baraza la Ardhi hawapati posho yao kwa wakati. Unaweza ukakuta wamepata posho baada ya miezi mitatu, minne au mitano. Sasa hapo tunawawekea wananchi ambao ni wa hali ya chini kupata shida. Kwa sababu, ambao wanapata haki katika haya Mabaraza ya Ardhi ni wale ambao wana kitu ambao ni matajiri lakini wanyonge wanapata shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mtu anaenda pale ana kesi yake, lakini yule Mzee wa Baraza la Ardhi atazungusha nenda rudi, atakayepata haki ni huyu ambaye amempa kitu kidogo na hiyo inatokana na wale wazee kutokupata posho yao kwa wakati. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu, kaka yangu Lukuvi naomba awaangalie kwa umakini hawa wazee wa Baraza la Ardhi, awalipe posho yao kwa wakati, ili hii migogoro ya kupata rushwa iweze kutoka. Rushwa haiwezi kukoma kwa style hiyo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aweze kuliangalia hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia vijana. Vijana wengi hawana ajira. Wanazunguka na karatasi na vyeti vyao kila kukicha. Ningeshauri ardhi ya akiba inayotengwa na vijiji wangepewa hawa vijana wakalima, wangepewa hawa vijana wakapata hati, hatimiliki itakayowawezesha kupata mkopo wa pembejeo. Wakishapata ile mikopo watalima, watapata mazao. Mfano mzuri ni mimi mwenyewe nalima mpunga, nina heka na heka, naweza kupata tofauti na hii hapa ambayo ajira yangu niliyonayo ya wananchi, naweza nikapata hela kutoka huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukiwaangalia hawa vijana au nikimtolea pia mfano Mariam Ditopile. Naye ni mkulima na anapata hela kutokana na huo ukulima. Kwa hiyo wakiwapa vijana hatimiliki wakamiliki kutoka katika hizi ardhi za vijiji vya akiba, wakafanya hata biashara ya kilimo. Wanaweza wakapata hela wakaondokana na hali duni ya maisha. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri aangalie hali za vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ardhi ya akiba inayotengwa mara nyingi hupewa wawekezaji wenye hela zao na matajiri. Hawa watu ambao hawana uwezo wanakosa. Naomba Serikali iangalie kama kuna mwekezaji ambaye sio tajiri sana, wasiangalie wawekezaji wanaotoka nje, waweze kuwasaidia hawa wawekezaji wa ndani ya nchi ambao wanaweza wakalima vitu na wakasaidia ndugu zetu wakatoka katika hali duni ya Maisha na kuwaondolea umaskini. Kwa hiyo, naomba huu upande wa wawekezaji wasiangaliwe sana matajiri, waangaliwe pia wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ardhi naomba ijikite sana kusafisha Maafisa Ardhi na Wapima ambao wamekuwa ni chanzo cha migogoro. Unaweza ukaenda ukakuta mpima anakuja mpima sijui binafsi, anakuja mpima wa Serikali, anakuja sijui mpima gani. Sasa inakuja kutokea unakuta kila mtu ana hati, shida inayokuja kutokea huyu ana hati na huyu ana hati. Mwingine anasema Serikali ilikuja ikapima, huyu mwingine anasema nilileta mtu binafsi alikuja kupima, huyu ana Sekta Binafsi ya kupima. Kwa hiyo, naomba Serikali ijikite kuangalia mpima ambaye anatambulika na Serikali kuliko kuzidi kuchanganya wananchi katika ule upimaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya uwepo wa Mabaraza ya Ardhi ya Kijiji, Kata na Wilaya bado lipo ongezeko la migogoro ya ardhi. Migogoro ya mipaka kati ya kijiji na kijiji kingine, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, hapa ndiyo balaa kabisa. Mkulima analima mazao yake, mfugaji anaenda anapeleka ng’ombe au mbuzi au whatever, wale wanyama anaowafuga wanaenda wanaharibu mazao ya yule mkulima. Ukiangalia, mfugaji ndiyo ana hela kuliko mkulima. Kwa hiyo anaweza kufanya chochote kile. Kwa hiyo naomba Serikali yangu iangalie haki ya hawa watu. Huu mgogoro wa mkulima na mfugaji wauangalie kwa undani sana. Waache kunyanyasa, hakuna mtu anayependa kutokuwa na kitu. Kila mtu anapenda awe na kitu lakini ukimnyanyasa yule ambaye hana kwa kweli inatia huzuni na simanzi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna migogoro kati ya vijiji na taasisi za Serikali, wenzangu wameshaongea. Unakuta kuna beacon, huyu anakuja anasema beacon yangu iko hapa, beacon yangu iko pale, lakini hiyo yote inatokana na wale Wapima. Ndiyo maana nilianza kumwambia Waziri wangu wa Ardhi angalia hawa Wapima kwa umakini. Sio kuangalia tu mtu huyu anapewa, wewe nenda ukapime, mara sijui nina taasisi fulani napima, wawe ni watu wanaoeleweka ili kuondoa hiyo migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia migogoro hii msingi wake inasababishwa na tamaa. Rushwa kwa baadhi ya watendaji katika Mabaraza, waliopewa kusimamia migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi. Narudi kule kule kwa wale wazee wa Mabaraza. Hawa hawa ndiyo wanakuwa chanzo cha migogoro lakini migogoro yao ni kutokulipwa posho. Unakuta huyu mzee wa Baraza anadai posho yake miezi mitano, miezi minne na kuendelea. Sasa kweli, akutane na pedeshee amwambie sasa huyu hapa, lazima ummalize mimi nakupa hela. Atashindwa kweli kama mwanadamu? Ili kumaliza rushwa, naomba tuwalipe hawa wazee kila anapodai posho yake mwezi au siku ikiisha, nafikiri wanalipwa kwa siku, wawalipe posho yao kuondoa huo mkanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua Wizara ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha inasimamia na kuwajibisha watendaji hawa. Endapo mtu amejulikana kabisa huyu mtu ametoa rushwa, je, Serikali inamchukulia hatua gani. Naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Wake waangalie kuanzia kwenye Kata, wasiangalie wilayani wala mkoani. Huku chini ndiyo chanzo cha yote, huku vijijini. Kwa hiyo, wakitaka kupata information iliyo sahihi, waanziae huku chini ndiyo kuna shida. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi afuatilie kwa undani sana. Tusipofuatilia, hii rushwa haitakaa iishe katika mambo ya ardhi kutokana na huo mpango unaoendelea kuwepo, ambapo hatuwasaidii hawa ambao wanatakiwa kusuluhisha ili kila mtu apate haki yake, zaidi tunazidi kuwaumiza hawa wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna hawa ma-secretary ambao wanawasaidia hawa Wazee wa Mabaraza, unaweza kukuta wamelipwa miezi mitatu na miezi mingine hawalipi. Au wanalipwa kwa miezi mitatu mitatu. Hawana ajira, namwomba Mheshimiwa Waziri Lukuvi awasiliane na Waziri wa Utumishi ili tuweze kujua hawa watu watalipwa kwa wakati au…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)