Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimepata hii nafasi kuweza kuchangia wizara hii muhimu na ninaomba niendelee alipoishia mchangiaji kwamba, pamoja na kwamba tunatambua kwamba wafugaji nao wanahaki na tunatambua kwa kwenda kuchukua ushuru kutoka kwao, lakini bado wafugaji hawajatendewa haki kama inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi zote zipo kwenye Serikali, leo ukiangalia namna wanavyotendewa wafugaji wa nchi hii, wakati tayari wizara inawajibu hamuwezi kuwa na haki ya kuchukua ushuru halafu mnashindwa kutimiza wajibu wenu kwa wafugaji, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo jambo kwamba, pamoja na hizo wizara mbili ambazo nimezungumza, lakini bado kuna wafugaji ambao ng’ombe zao zilikamatwa bila utaratibu wakaenda mahakamani na mahakama ikaamua kwamba hao wafugaji warudishiwe ng’ombe zao, mpaka leo hawajapewa ng’ombe zao. Ni wajibu wenu wizara kwa sababu mnachukua ushuru na tozo mbalimbali kuhakikisha wafugaji wa nchi hii ambao mahakama imeshaamua wanapewa haki zao za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba wanatakiwa kurudishiwa mifugo bado mnawajibu kama wizara kuhakikisha kwamba hawa watu, minada pale panapostahili, nitazungumzia eneo moja tu, wafugaji wangu ambao wapo ziwani, Ziwa Tanganyika ili wafikishe mifugo yao mnadani lazima wapite kwenye hifadhi na wakipita kwenye msitu ule wanakamatwa sasa ni wajibu wa nani, lazima muwapelekee huduma jirani na kule waliko kwa sababu ni haki yao na ni wajibu wenu Wizara kufanya hivyo. Kwa hiyo tunaomba minada kwenye maeneo ambayo yana wafugaji kwa sababu ni haki yao kupata huduma za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuzungumzia uchache tu kwa hao wafugaji, naomba niende kwa wavuvi, miongoni mwa changamoto ambao zinawakumba wavuvi wetu ni pamoja na kanuni zilitungwa 2019/2020, kuna changamoto kubwa kwenye eneo hilo, Mheshimiwa Ulega ulikuwepo kwenye utungaji wa hizo kanuni na wakati Mheshimiwa Rais anasema anakurudisha hapo alitamka maneno fulani. Hata hivyo, wakati naangalia CV zako nikagundua kwamba eneo hilo linakuhusu sana la uvuvi na akasema amekuleta urekebishe na sisi tunaimani kwamba Mama hakuja tu kwamba kukurudisha alikuwa amepitia na akagundua kwamba kuna shida. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hicho alichokifanya tuna mategemeo makubwa kwa kuwa waziri ndio ameingia wewe ulikuwepo utamsaidia zaidi kuweza kuboresha yale makosa ambayo yalifanyika kipindi kilichopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuzungumzia habari ya uvuvi haramu. Mimi Aida siyo muumini wa kuwasaidia wanaofanya uvuvi haramu, lakini kumekuwa na makatazo kadhaa kutoka kwa wizara na Serikalini, lakini makatazo hayo hayaendani na njia mbadala namna ya kuwasaidia wavuvi wetu kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la nyavu, wakati waziri anawasilisha hapa amesema uvuvi haramu umepungua kwa asilimia 80 tunashukuru kwa sababu umepungua, lakini umepungua umewaacha wavuvi wetu kwenye hali gani kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ilikuja na utaratibu wa kwamba wanahitaji kutumia nyavu ya milimita nane na kumekuwa na mkanganyiko kwenye hiyo taarifa, wengine milimita kumi, wengine milimita nane. Pamoja na milimita nane hiyo nyavu wanapokwenda kutumia hao wavuvi kuna maeneo ambayo haizuii hiyo nyavu Samaki ambao wizara haitaki waingie kwenye ile nyavu, kinachotokea ni nini? Huyu mvuvi ambaye ni mtu wa mwisho kabisa ikitokea wale Samaki ambao inaonekana ni halali wapo robo tatu labda pale wamepenyeza Samaki kumi au watano hawa watendaji wanapofika kule wanawatoza faini, faini ambazo hazina uwiano, milioni mbili, milioni tano, milioni kumi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wavuvi pamoja na kuchangia pato la Taifa hizi nyavu zinapoingia nchini Serikali mpo, nyinyi ni wajibu wenu kuhakikisha mnafuatilia nyavu hizo zinazalishwa wapi. Kinachofanyika sasa hivi kwenye nchi yetu ni sawa na msafara wa ng’ombe, ng’ombe wa mbele akisimama anayepigwa ni ng’ombe wa nyuma ndiye anaye adhibiwa. Hawa wanao adhibiwa leo wavuvi wetu ni watu wa chini kabisa hizi nyavu zimepita sehemu ngapi mpaka kumfikia mvuvi wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri nikuombe sana, niwaombe sana na Mheshimiwa Waziri kuna haja ya kufanya utafiti wa kutosha juu ya jambo hili na kwa sababu tumekuwa na utaratibu tukiamini ndiyo njia halali, au ndiyo suluhisho la kuchoma nyavu ni vizuri tukajifunza. Nitatolea mfano wa Ziwa Tanganyika, Ziwa Tanganyika tuna-share zaidi ya nchi tatu, hivi mmejiuliza nchi nyingine ikiwemo Kongo, Burundi na Zambia wamefanya nini na wanatumia nyavu gani badala ya kuja kuwaadhibu hawa wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumza kwenye Bunge lililopita na leo narudia kusema hawa Samaki wanavyokuwa mle ndani kwenye ziwa hawajui kwamba wapo Tanzania, wapo Kongo au wapo Burundi kwa hiyo kuna wakati mwingine tunatunga kanuni ambazo zinakwenda kuwanyonga wavuvi wetu bila kuangalia kwamba wenzetu wanafaidikaje na hilo jambo.(Makofi)

T A A R I F A

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Spika, taarifa nakuruhusu.

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza kuhusu nyavu hizi ambazo zinatakazwa na wizara ni nyavu aina ya Makira, hizi nyavu aina ya Makira neno lenyewe limetoka Kongo ni neno la kifaransa kwa hiyo linakatazwa huku kwetu Ziwa Tanganyika, lakini kule Kongo wanavua kwa kupitia nyavu hiyo, kwa hiyo, tunahifadhi samaki huku kwetu kule tunawaachia waweze kuwavua hao Samaki. Ahsante sana.

SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Aida?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, kwa maslahi ya wavuvi wetu ninapokea kabisa, kabisa hiyo taarifa na kuna haja ya wizara kujitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye jambo hili twendeni tukafanye utafiti wa kutosha kwenye nchi ambazo tuna-share kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, kuangalia wenzetu wanafanya nini kabla ya kuja na kanuni ambazo hazitusaidii. Lakini tuboreshe pia sera zetu na sheria ambazo tunaamini zitaleta manufaa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uvuvi ring net, kulingana na umaskini wa wavuvi wetu wanatumia ring net utakuta mle ndani kwenye hicho kifaa kuna wavuvi kumi, kumi na moja mpaka kumi na tano. Sheria zetu zinataka kila mvuvi aliyopo kwenye kile chombo awe na leseni, hili jambo Mheshimiwa Waziri nataka tu kwamba, kama tuliweza kuangalia zile sheria au kanuni za wafanyabiashara wadogo ambazo zilikuwa ni kero twendeni tukaangalie na kwa wavuvi wetu jambo hili ni kero bado kwa wavuvi wetu, naamini inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye jambo lingine kuhusu mikopo, mikopo kwa wavuvi. Pamoja na kuwachomea nyavu hawa watu wamekuwa maskini ni wajibu wa Serikali sasa tuende tukawapatie mikopo ambayo itawasaidia kuwa na nyavu halali ambazo zimeidhinishwa na wizara ziweze kuwasaidia watokane na uvuvi walionao leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba hili jambo ipo kwenye sera, nashukuru nimeona wizara mmeanza juzi Mwanza nilikuwa na Naibu Waziri yupo kule, tunataka kuwaona na wavuvi wa Ziwa Tanganyika wanapewa mikopo, mikopo ambayo itawawezesha waondokane na umaskini ambao mwingine ulitokana na maamizio na mambo yenu ambayo mlikwenda kuyafanya ambayo hayatatusaidia kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niende kwenye suala la mipaka ndani ya ziwa. Kama kuna sehemu kinatumika kama kichaka leo hii cha kukusanya kodi kwa wavuvi ni hicho kitu kinaitwa mipaka, hifadhi ndani ya ziwa. Hawa wavuvi wetu wanapoingia ziwani kuvua hakuna alama yoyote inayoonyesha kwamba hapa niihifadhi, matokeo yake wale watendaji badala ya kutoa elimu wamekaa pale kama mtego wanasubiri mvuvi aingie kisha wampe adhabu kwamba hapa umeingia kwenye hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili halikubaliki, ni vizuri tukajikita kutoa elimu na kutimiza wajibu wetu wa kuweka mipaka, alama zinazoonyesha hii ndiyo mipaka hapa ni hifadhi, badala ya kwenda kuwapa nanii adhabu wavuvi wetu. Na hili jambo wapo watendaji wenu ambao siyo waaminifu, inawezekana zile fedha hazifiki kwa sababu hata wanapotoza hawatoi risiti, naamini Serikali hainufaiki na chochote kwenye jambo hili. Kuna kila sababu pamoja na sheria zenu ziwe wazi na mjikite zaidi kutoa elimu kwa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi ni suala ambalo watu wanataka kujikimu kimaisha yale maji yalivyo yasigeuke leo kuwa laana kwa wananchi wetu lazima maji yale kuwa karibu leo na Ziwa Tanganyika wananchi wanataka kunufaika iwe baraka, siyo leo inavyoonekana kuwa laana kuwa karibu na Ziwa Tanganyika, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, kuna wamama ambao wamejikita kuuza Samaki hawa Samaki ambao leo inaonekana ni haramu wanapita na mabeseni na sinia wanauza zile Samaki. Jambo ambalo linatokea leo Maafisa Uvuvi akikuta yule mama anauza Samaki, yule mama hajui kwamba huyu Samaki anaruhusiwa au haruhusiwi anakamatwa na sinia lake, anatozwa faini milioni moja, laki tano, laki nane, niwaombe wizara kuna kila sababu ya kuwaangalia...(Makofi)

SPIKA: Ahsante sana

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)