Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu vile vile kunipatia nafasi hii. Niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam kwa bajeti nzuri waliyoiwasilisha leo.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme mambo machache katika bajeti hii. Bajeti ya Uvuvi inaonekana kwenye utekelezaji, hela ya Serikali iliyokwenda mwaka 2020 ni asilimia 30 tu. Kwa hiyo, naishauri Serikali iongeze kupeleka pesa kwa ajili ya utengenezaji wa bajeti hii kwa sababu inawagusa sana wananchi wetu. Vile vile kwenye bajeti hii upande wa mifugo bado pesa iliyokwenda ni kidogo. Kila unapoangalia kwenye bajeti hizi utagundua mchango wa Serikali kwenye mchango ule ambao Serikali inatakiwa itoe, kwenye bajeti nzima ya nchi ni kama 0.08. Kwa hiyo, ni ndogo, haifiki hata asilimia 1 na hasa hizi za uvuvi na mifugo ni kama 0.03. Ni ndogo sana. Kwa hiyo, kama tunatarajia maendeleo makubwa na uchangiaji mkubwa wa pato la Taifa, tunategemea bajeti hizi ziongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri, kwenye uvuvi safari hii development budget ameiongeza mara saba; seven point something ambayo inaonesha kabisa kwamba kuna vitu vikubwa kwenye uvuvi vitakwenda kutokea japokuwa kwenye mifugo bado development budget ni ndogo kwa hiyo, naamini hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Mifugo.
Mheshimiwa Spika, niungane na wewe ulivyosema NARCO ni kama imeshindwa hivi. Pamoja na kushindwa nitoe ushauri kwamba tunatakiwa tuunde sasa kitu kinaitwa Livestock Development Authority. Katika hilo, tukishakuwa na authority hii wao maeneo yao sasa kama wataya-surrender wayaache kwenye Halmashauri na Halmashauri iwape watu binafsi na vikundi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba uzalishaji huu unaweza ukaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunda hiyo Livestock Development Authority, tufanye kama Waganda. Tuwe na Dairy Development Authority ambayo itashughulika na maziwa na nyama. Kwa sababu, mpaka sasa hivi haya maziwa tunayosema yamezalishwa hapa yameshindwa kuuzwa nje kwa sababu hatuna chombo kinachoshughulika na haya. Kwa hiyo, tuunde chombo hicho, Dairy Development Authority ambayo itakuwa inashughulika na hii. Tutakapokuja kwenye bajeti nyingine, watatupa taarifa sahihi ya nini wameanzisha katika kuingia kwenye Soko la Kimataifa kuuza maziwa.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nataka nikizungumzie kwenye mifugo ni nyanda za malisho. Tunataka kufuga na sisi tupo atika tatu bora Afrika kama wafugaji wa ng’ombe. Mifugo hii tusipokuwa na malisho ya kutosha imekuwa ikisababisha mifarakano mikubwa katika jamii, wananchi wanagomba kati ya wakulima na wafugaji. Ugomvi huu unaotokea kati ya wakulima na wafugaji ni kwa sababu hakuna nyanda za malisho na hatujapanga matumizi bora ya ardhi kwa utaratibu mzuri ambao unaweza kutufikia nyanda za malisho wasigusane wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai hapa kwamba tunazo sheria za kutosha. Tunayo Sheria Na.5 ya Mwaka 1999 ambayo inavikabidhi vijiji ardhi, inakuwa ni mali ya vijiji. Pia tunayo Sheria Na.7 ya Mwaka 2007 inayoshughulikia matumizi bora ya ardhi. Tunayo Sheria Na. 13 ya Mwaka 2010 inayozungumzia habari ya nyanda za malisho. Tuone ni namna gani bora tunaweza kufanya wakulima na wafugaji wasigombane kwa sababu hii ni kama Wizara moja. Kila mmoja azalishe lakini kwenye ardhi hii tuliyonayo.
Mheshimiwa Spika, nitoe ushauri tu kwamba tunapokwenda kwenye utekelezaji wa haya ambayo tunayafanya mwaka huu tuangalie namna gani tutaenda kushughulikia nyanda za malisho maana matumizi bora ya ardhi tuliyonayo yafanyike kwa wingi ndani ya maeneo tuliyonayo. Bahati mbaya sana jana ilikuwa Wizara ya Ardhi. Kwa hiyo, najua hili wao wanahusika na Wizara ya Mifugo nayo wanahusika kuhakikisha kwamba nyanda za malisho zinakuwepo ili ugomvi huu tunaousikia kila siku upungue. Migogoro ya ardhi inafifisha sana ukuaji wa Sekta hizi.
T A A R I F A
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa unapewa.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tatizo la Nyanda za Malisho halitokani na kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa sababu vijiji vingi tayari vimeshapimwa. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Longido kati ya viji 49, 30 vimeshapimwa na vina mpango wa matumizi bora ya ardhi, lakini kuna mashindano kati ya Wizara na Wizara. Wakati Wizara ya Mifugo haihangaiki ku-secure na kuhifadhi nyanda zake za malisho, maliasili wao wako kazini kutafuta nyanda za malisho za kuchukua na kuongezea kwenye hifadhi.
SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa Magessa.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, naipokea. Inaonekana tena kwamba kuna habari tena ya wanyamapori na siyo ya wakulima na wafugaji. Naipokea Taarifa hiyo. Najua kabisa Mkungunero pale kuna shida hiyo na kwa ndugu yangu Ngorongoro kuna shida hiyo. Hizi Wizara zifanye kazi kwa pamoja kwa sababu ni Wizara ya Serikali. Kwanini zinashindana? Shida yetu kubwa ni kumtumikia mwananchi, hatuna haja ya kushindana. Nafikiri hili limeshazungumzwa sana kwamba Wizata zikutane kwa pamoja kujua nani anafanya nini na wakati gani ili wananchi waweze kupata maendeleo? Naomba niipokee Taarifa hiyo. Naikubali Taarifa yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme pamoja na ufinyu wa malisho kuna upungufu wa majisafi na salama kwa ajili ya mifugo hii. Kuna upungufu mno wa maji na mabwawa. Ningeomba sana mabwawa yaweze kuongezwa. Vile vile kumekuwepo na shida katika Sekta hii, kuna uwepo wa soko holela na bidhaa za madawa na vifaatiba vya mifugo. Sasa watu wanaleta tu dawa, badala ya kutusaidia ng’ombe wetu wakati fulani ng’ombe wanakufa. Pia kuna mwamko mdogo wa ufugaji wa kitaalam kwa kuzingatia idadi sahihi ya mifugo katika maeneo ya malisho. Hili nalo, tuna ng’ombe wengi lakini je, elimu imetolewa ya kutosha kuhakikisha kwamba wananchi wetu sasa wanaweza kufuga kitaalam badala ya hii ambayo inafanyika sasa hivi, inafikia mahali fulani watu wanagongana. Naamini kabisa hili likitolewa elimu, changamoto hizi zitapungua.
Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye uvuvi sasa. Mimi kwenye maeneo ninayotoka…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, hii kengele ya kwanza?
SPIKA: Ndiyo?
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo ninayotoka nina mialo yapata karibu saba. Nina mwalo sehemu moja inaitwa Butunde, Kasamwa, Kageye, Bukondo, Busaka, Chankorongo na Kabugozo. Maeneo yote haya ni sehemu ambayo nategemea wavuvi waweze kufanya kazi na kupata maisha. Bahati mbaya sana katika haya mazingira ya uvuvi, hawa wamekuwa wanafanya uvuvi huria tu. Akichukua mtumbwi wake asubuhi, anakwenda anakuja na samaki watatu au watano usiku mzima. Tunahitaji kuwawezesha hawa watu kwa kuwapa elimu na kuwafundisha.
Mheshimiwa Spika, kwenye kilimo tuna mashamba darasa, sijui kwenye uvuvi tutaita nini? Sijui tutaita uvuvi darasa, sielewi tutaita kitu gani? Ila tuwe na namna ambavyo hawa wavuvi wanaweza wakafundishwa. Sasa hivi dunia imehamia kwenye uvuvi wa vizimba. Nilimwona ndugu yangu mmoja alisimama hapa, ni mtaalam kwenye cage hizi (vizimba). Nimejaribu kuangalia kwenye maeneo yote hayo niliyoyataja, hakuna kizimba hata kimoja.
Mheshimiwa Spika, niseme tu, kwa sababu tuna kituo kikubwa kilichoko pale Chato, naamini kwamba kituo hicho sasa Wizara inaweza kukitumia kutusaidia sisi maeneo hayo kupata vizimba; kwanza vije vizimba vya mfano watu waone kinachofanyika; na wapatikane hao Maafisa Ugani wa kufundisha hiyo kazi kwa sababu hatunao sasa, lakini tuoneshe mfano halafu baadaye watu waingine kwenye vizimba. Watu wanasema kuna maeneo mengine yamechukuliwa kama breeding area, eneo tu la kufanya watu wazalie, lakini nafikiri tukifuga samaki maana yake hatuzuii breeding hiyo ambayo inafanyika sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naombe sana Wizara watusaidie kwa sababu tuna changamoto kubwa ambayo inaonesha ili uweze kuingia kwenye vizimba hivyo, inabidi ufanyiwe environmental impact assessment. Hii ni gharama kubwa. Inatakiwa TAFIRI waingie hapo, nao wana tozo yao; halafu Kata, Kijiji na Wilaya nayo ina tozo yake. Napendekeza sana, TAFIRI ambao wanashughulika na mambo ya samaki hawa ndio wachukue tozo moja tu. Wakishachukua wao ndio watai-distribute huko kwenye environmental impact assessment.
Mheshimiwa Spika, badala ya kuonekana huyu mtu mmoja mvuvi masikini anakwenda kulipa hizi na gharama yake ni kubwa, zinakwenda karibu milioni 10, ni nani mvuvi wa kawaida ana uwezo wa kuzilipa? Maana yake lazima Serikali iingie kuhakikisha kwamba tozo hizi zinapungua ili wananchi wa kawaida waingie kwenye hivyo vizimba na mwisho wa siku tutaona maendeleo yamekuja. Tumepata umeme sasa. Umeme huu utatumika wapi kama uvuvi wenyewe utaendelea kuwa wa mtu mmoja mmoja. Umeme huu utumike vizuri kuona viwanda vidogo vidogo vya samaki ili mapato haya yaweze kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa Waziri na Naibu Waziri na Naibu Waziri wanajua, Kituo chao cha Nyamirembe kina uwezo wa kufanya kazi kubwa kwenye maeneo hayo na tukaona matokeo makubwa. Wananchi wetu tunategemea mifugo iliyoko. Kwa mfano, mifugo iliyoko Jimboni Busanda, mingi inabidi ipelekwe Misenyi. Sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)