Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniamsha salama asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwanza sina budi kutoka pongezi za dhati kwa Wizara hii Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa juhudi mbalimbali wanazofanya kuhakikisha sekta zetu mbili za uvuvi na mifugo zinapiga hatua na kumsaidia mwananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na maoni ya Kamati kwamba Bajeti ya Wizara hii ni ndogo, utoaji wa fedha hauendi kwa wakati, hivyo inachangia kurudisha nyuma mipango kabambe ambayo imepangwa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashauri Serikali itoe fedha kwa wakati na iongeze bajeti kwa ajili ya kutatua changamoto na kupiga hatua mbele mbalimbali za maendeleo, kwa sababu Wizara hii ina mchango mkubwa katika kuongeza pato la Taifa. Tutapata fedha za kigeni kupitia Wizara hii, tutaongeza ajira, lakini pia Wizara hii itatusaidia kwenye usalama wa chakula kwa maana tutapata vitoweo, maziwa na vitu vinginevyo ambavyo vitasaidia usalama wa chakula katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakubaliana na mawazo ya Kamati kwamba sheria za uvuvi na mifugo na kanuni zake zifanyiwe haraka zikamilike ili kutatua changamoto za wavuvi na wawekezaji wa uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea ninakuja kwenye sekta hii ya uvuvi, kwenye uvuvi wa bahari kuu nawapongeza sana Serikali kwamba sasa tunaingia kwenye uchumi wa blue kwa vitendo na imesema hapa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 itanunua meli mbili za uvuvi kwa kuanzia. Sasa mimi ninataka niiambie Wizara kwakuwa chombo hichi DSFN cha Kitaifa meli mbili za uvuvi za Zanzibar zitanunuliwa kwa awamu gani ya bajeti? Naomba hapo nayo ituweke sawa ili tujue tunafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye uwekezaji wa viumbe kwenye maji, hapa pana soko kubwa sana la ajira kwa vijana na wanawake. Eneo hili litakwenda kutatua changamoto za ajira kwa vijana na wanawake, lakini pia itaongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja, kitaongeza kipato kwa vikundi, lakini pia kipato kikubwa kwa Taifa, kwa sababu tutawekeza kwenye hii sekta, tutauza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uingizaji mkubwa wa samaki kutoka nje hivi kweli hata saladini tunaagizia kutoka nje, vibua vile ambavyo vimejaa nchini mwetu, lakini tunaagiza kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema hapa kuna vyuo ambavyo vinatoa mafunzo ya ufugaji wa samaki vyuo vile ninawashauri serikali iwe na programu tofauti, programu ya muda mrefu na ya muda mfupi, zile za muda mrefu ziendelee kwa wale wanaotaka utaalamu zaidi, lakini zile za muda mfupi ziwe kwa vijana wetu hawa wa kati na kati ambao watatoka kupata ajira wakaanzie miradi yao. Ninashauri ili kuvutia uwekezaji katika sekta hii kwa wananchi mbalimbali wale wataalam ambao wamepata mafunzo kwenye vile vyuo vyetu vya mafunzo Wizara iwe inawatangaza, waweke kumbukumbu zao na wajulikane wako wapi ili mwananchi anapotaka kuanzisha huu mradi ajue mtaalam nitampata wapi wa kunisaidia kutengeneza huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wale vijana ambao tunawapatia mafunzo kwa program ndogo ndogo zile zitakazoundwa na Wizara ninashauri kuna mifuko ile ya vijana ya uzalishaji mali ya wanawake sasa badala ya kuwapa cash watengeneze ile miundombinu, hawa vijana wameshapata mafunzo, watengenezewe miundombinu, wajengewe mabwawa, vifaa na vifaranga waanzishe, hii itakuwa chachu kwa vijana wengine watakapoona wenzao wanafaidika na wao kutaka kujifunza utaalamu huo wa ufugaji samaki na wa viumbe kwenye maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye ufugaji wa samaki na viumbe kwenye maji sio samaki tu, pweza, na nini, lakini kuna madini pale yanapatikana madini ya lulu. Madini ya lulu yanahitajika sana duniani, yana soko kubwa, tunayapata kwa kupitia ukuzaji wa viumbe kwenye maji, kuna lulu zinapatikana baharini, lakini lulu tunaweza tukazitengeneza wenyewe kwenye vizimba vyetu, lulu ni madini makubwa duniani yanahitajika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwa dakika zangu chache zilizobaki labda nijikite kidogo kwenye suala la ufugaji. Wizara ijitahidi sana ufugaji wenye kuhifadhi mazingira ya nchi kwa maana zile Ranchi za Taifa, Kamati imeshauri vizuri, zile Ranchi za Taifa na nyongeza yangu hii iwe kama shamba darasa sasa kwa wafugaji ili kuwepo na mabwawa, kuwepo na malisho, halafu kuwe na program kuwachukua wale wenye ng’ombe wengi wafugaji wakubwa waliopo kwenye Mikoa yetu waje pale wajifunze namna ya kuhifadhi mazingira, yaani wafuge kitaalamu, wavutike na ile ranchi kwamba hapa tukifanya hivi na sisi tunaweza tukafanya kwa sababu wakirudi kule kwenye maeneo yao waanzishe hiyo miradi kwa sababu uwezo wa kuanzisha wanao kwa sababu wana ng’ombe wengi wanaweza wakauza wakaanzisha hayo malambo na vitu vingine vya kulishia wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaweza tukawekeza mabwawa kwenye maeneo, lakini bado wafugaji hawahamasiki kukaa pale pale wanaendelea bado kuendelea kuhama hama lakini tukifanya programu maalum…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Khadija muda wako umekwisha.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)