Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Juma Usonge Hamad

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu leo hii kutujaalia tuko wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa leo tunaendelea na Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi mimi nitajikita zaidi kwenye suala la uvuvi. Kwenye suala la uvuvi kuna watu ambao wanajishughulisha na suala la Mwani, ingawa wachangiaji wengi hawajalizungumzia suala hili, lakini ni suala ambalo ni muhimu sana na suala ambalo ni nyeti. Ukiangalia kuna baadhi ya Mikoa Tanzania Bara na kule Zanzibar kuna Mikoa Tanzania Bara isioyopungua mitano upo Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Tanga ndiyo mikoa ambayo imeshamiri sana katika kujikita kushughulika na suala la uvuvi huu wa mwani.

Mheshimiwa Spika, lakini bado sijaona mipango mikakati kupitia Wizara hii mbali na ripoti ambayo imewasilishwa hapa mezani, bado sijaona fungu la fedha au mikakati yoyote ambayo Wizara imejikita kwa ajili ya kunusuru hili zao la mwani. Miaka ya nyuma mnamo mwaka 1980 zao hili la mwani lilishamiri sana lilipoletwa Zanzibar na tukafanikiwa kwa muda wa miaka 10 na ikaonekana Zanzibar ambayo kiujumla ndiyo Tanzania ikaonekana kama nchi ya Tatu katika kufanikiwa katika kulipanda zao hili la mwani.

Mheshimiwa Spika, lakini mnamo mwaka 1990 na kuendelea zao la mwani hili likaendelea kulimwa huku Tanzania Bara, na wengi wao walikuwa wanapanda huu mwani ni wakinamama. Ukiangalia asilimia 90 ya kinamama ndiyo washughulikaji wakubwa sana wa zao hili la mwani, miaka hiyo ya nyuma mwani ilikuwa ina value kubwa sana na ulikuwa una faida kubwa sana, lakini cha kushangaza baada ya mwaka 2010 na kuendelea zao hili la mwani halina thamani hata kidogo, mbali na gharama kubwa sana za wavuvi hawa wa mwani waliotumia kwa ajili ya kulikuza hili zao la mwani na matokeo yake kupata faida gharama kubwa sana ambazo wanazitumia, sijaona mpango mkakati wa kunusuru zao hili mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa Tanzania inatajwa ni nchi ya tatu baada ya Uphilipino na Indonensia katika kuongoza zao hili la mwani. Kwa hiyo naiomba sana Wizara, naiomba sana kupitia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi iende ikaangalie na kunusuru zao hili la mwani, tukiangalia Zanzibar wamejaribu kutumia mbinu tofauti tofauti kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani, wameanzisha makongamano mbalimbali, kutafuta wawekezaji bado changamoto kwenye soko, lakini bado kwa Tanzania Bara inaonekana kwamba zao hili halijapewa mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana ndugu yangu Naibu Waziri ingawa ni mmoja ambaye unafuatilia sana suala hili la mwani na kufuatilia sana, lakini bado sijaona mikakati ingawa mwaka jana mlitenga zaidi ya shilingi milioni 41, lakini fedha mlizozitowa ni shilingi milioni 14 kwa ajili ya kununua kamba, lakini mwaka huu sijaona kabisa, sijaona kabisa fungu la fedha ambalo limetengwa kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara hii mtenge fedha kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia la pili tutafute wawekezaji kutoka nje, tusing’ang’anie wawekezaji hawa tuliokuwa nao sasa hivi, lazima tufungue forum ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kunusuru zao hili; asilimia 90 ya kinamama ndiyo wanajishughulisha na zao hili la mwani. Najua tukisema tunaendelea pia tunawadharau na bei ndogo ya soko tunaenda kulididimiza zao hili la mwani.

Mheshimiwa Spika, nadhani tukiweka mpango mikakati mizuri zao hili linaweza likainuka na tukarejea kwenye top one ile ambayo tayari kidunia zao ili la mwani Tanzania miaka hiyo, basi tukaweza kuirejesha ndani ya miaka hii. Mimi ninaamini ndugu yangu Abdallah Ulega bado ujachelewa na ninaamini maarifa mengi na unauwezo mkubwa sana kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tusiishie hapa tu tunao ndugu zetu wa Zanzibar, kwa nini tusishirikiane kwa pamoja kwa sababu ni suala la kutafuta soko nje ya nchi ni suala la Muungano, Katiba imezungumzia ibara ya kwanza na ya pili kwamba tunapokwenda nje kule tunakuwa kitu kimoja tukaazisha angalau japo makongamano kwa mfano kama tukianzisha masuala ya Seaweed Vast Value Tanzania tunaweza tukanusuru zao hili la mwani na mwisho wa siku tukavutia wawekezaji na zao hili likaleta tija …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Juma Usonge Hamad.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)