Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini naomba nimshukuru Waziri, Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Bashe na Watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, nina hoja mbili kubwa, hoja ya kwanza ni kuhusu Mfuko wa Umwagiliaji na hoja ya pili ni kuhusu kilimo cha korosho Manyoni. Kwanza, niishukuru sana Serikali tulianzisha Tume ya Umwagiliaji, kuna Kanuni za Umwagiliaji za 2015, lakini kuna Sheria ya Umwagiliaji na vilevile kuna Mwongozo wa Tozo na Ada za Umwagiliaji, hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba hatuwezi kuendeleza kilimo cha Tanzania iwapo Profesa hutaweka mkazo na uwekezaji kwenye umwagiliaji. Hiyo itabaki kuwa ndoto, naomba tuige nchi za wenzetu Egypt, Somalia, Sudan na nchi zingine ambazo zimeendelea.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni nini? Katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki nina skimu zaidi ya 8, nina skimu za Udimaa, Ngait, Mawen, Chikuyu, Saranda, Msemembo, Kintinku na Mtiwe. Hata hivyo, nikipitia bajeti hii, sijaona sehemu ambako Profesa unaenda kuwekeza kuhakikisha kwamba ule uharibifu ambao ulisababishwa na mvua kubwa tunaenda kuwakomboa wakulima.
Mheshimiwa Spika, nina masikitiko makubwa kwa sababu kama hatutawekeza kwenye umwagiliaji…
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chaya sekunde moja tu, Waheshimiwa Wabunge sasa tumpe nafasi Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mbunge yeyote asiende pale ili apate kusikiliza masuala ya kilimo kwa sababu ni muhimu sana. Anayemhitaji Waziri Mkuu tuna ofisi hapa Administration kuanzia saa 7.00 mchana mpaka saa 11.00 jioni mnaweza mkaenda kumuona. Sasa hivi muacheni ili asikilize hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu matatizo halisi ya wananchi maana yeye ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mheshimiwa Dkt. Chaya, endelea. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni nini? Mwaka jana katika hizi skimu nyingi za umwagiliaji ambazo ziko katika Jimbo la Manyoni Mashariki zilipata adha kubwa sana ya mvua. Niliwasiliana sana na wenzetu wa Tume ya Umwagiliaji nawashukuru, waliahidi kuja kuturekebishia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mfuko wa Umwagiliaji, nina hoja kadhaa ambazo napenda kulishauri Bunge. Kwanza huu mfuko ambao tumeuanzisha na umeanza kufanya kazi mwaka jana unategemea ada na tozo za wanachama. Sasa tunategemea huu mfuko uje ujenge skimu kubwa hapa Tanzania lakini unategemea skimu ambazo hazijaendelezwa. Profesa naomba uliangalie hili, tunahitaji kwanza kuwekeza kwenye skimu hizi, kuzirekebisha ili huo mfuko wako utune. Bila kuwekeza kwenye hizi skimu Profesa hizi skimu zitabakia kuwa ndoto na mfuko utabakia kuwa ndoto na umwagiliaji Tanzania utabakia kuwa ndoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine hivi vyama vya wamwagiliaji vimeanzishwa lakini havijapewa mafunzo na utendaji wake wa kazi upo chini sana. Napenda kujua Profesa umejipangaje kwenye bajeti yako kuhakikisha kwamba, kwa mfano kwenye zile skimu zangu 8, umeweka bajeti ya kuja kuviwezesha vile vyama vya umwagiliaji, uwape mafunzo, wajue jinsi ya kusimamia mifuko hiyo, jinsi ya kuchanga na hata jinsi ya kuchukua hizo tozo na kurudisha kwenye mfuko wa Serikali. Kwa hiyo, naona hii ni hoja ya muhimu na ningemshauri Waziri aweze kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la kilimo cha korosho. Mimi naishukuru sana Serikali tumeanzisha kilimo cha korosho na baadhi ya Wabunge wetu humu wengi mna mashamba ya korosho kule Manyoni. Tunatumia block farming system ambapo wakulima wengi wameungana na nimshukuru sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha kwamba kilimo cha korosho kinaenda kuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeanza uvunaji wa awamu ya kwanza wa korosho kule Manyoni. Hoja yangu hapa, nitatamani kusikia kutoka kwa Profesa kwenye bajeti hii, amejipangaje sasa kuhakikisha kwamba Manyoni kilimo cha korosho kinakuwa chenye tija? Je, mnawasaidia vipi watu wa Manyoni kwa kuja na mfumo rafiki sasa kwenye masuala ya masoko, maghala na kuwa na mfumo rafiki kuhakikisha kwamba wale wakulima wawe sasa na matumaini ya zao la korosho?
Mheshimiwa Spika, kuna sintofahamu kubwa sana kuhusu suala la korosho. Nimesikia ndugu zangu wa Mtwara na Lindi wakilalamika, hatutaki hayo makosa yatokee Manyoni na ningetamani kuona sasa Waziri anakuja kwenye bajeti yake na bajeti ambayo Manyoni itakuwa ni sehemu ya kipaumbele kwenye suala la korosho na hasa kipindi hiki ambapo tumeshaanza kuvuna ili wananchi na wakulima wetu wapate matumaini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la miundombinu. Tutatamani kuona Waziri unakuja na bajeti ambayo kwa Manyoni ambapo Bodi ya Korosho inafanya kazi ni jinsi gani mnaenda kuwasaidia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chaya, dakika tano ni ndogo.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)