Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii ambayo ni muhimu sana. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuifanya kwa muda mrefu tangu nchi hii ipate uhuru.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza litakuwa ni eneo A, hili litakuwa linahusu Mkoa wa Pwani na eneo la pili tutakuwa tunazungumzia suala zima la Kitaifa na imani yangu ni kwamba dakika tano zitatosha sana.

Mheshimiwa Spika, nina masikitiko makubwa sana katika bajeti ambayo imetoka kuzungumzwa katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri kwamba bajeti hii haikuugusa Mkoa wa Pwani kama vile ipasavyo. Ni masikitiko yangu makubwa sana kuona kwamba pale Pwani katika Wilaya ya Rufiji watu wa Kibiti sisi ni wahusika, watu wa Mkuranga ni wahusika. Kuna mradi mzuri sana pale katika Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini bajeti/hotuba hii haikuzungumza chochote kuhusiana na suala zima la kilimo cha umwagiliaji sijui, sisi watu wa Kibiti, Pwani, Rufiji tumekosa nini kwa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama hivyo haitoshi masikitiko yangu mengine makubwa ni kwamba watu wa Pwani hasa watu wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Bagamoyo, Mafia sisi ndiyo wakulima kule wa zao la korosho wakizingatia kwamba pale Kibiti ndiyo barabara yao. Tunazalisha korosho kwa wingi sana. Tuna shida sana sisi pale Pwani kuhusiana na ubora wa korosho zetu na suala hili tumekuwa tukilijadili mara kwa mara. Waheshimiwa Wabunge tukiwa tunakutana na Mheshimiwa Ulega, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Mheshimiwa Jaffo tulikuwa tunakaa tunajadili suala hili, jinsi gani tutakavyoweza kusaidia sasa Serikali ili iweze kutusaidia. Zao hili la korosho liwe na ubora wa kutosha kwa sababu kila mwaka zao hili pale Pwani bei yake iko chini zaidi.

Mheshimiwa Spika, grade A, inayokuwa inauzwa kule kwa watoto wetu Kusini, pale Pwani inauzwa mpaka shilingi 400, hiki kitu hakieleweki. Nasikitika sana Profesa katika hotuba yako hujaeleza mkakati gani mlionao ili kuweza kutusaidia sisi watu wa Pwani, ili ubora wa korosho zetu uwe mzuri na vilevile tuweze kupata bei ile ambayo inastahiki kama vile watoto wetu wa Kusini na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nataka nichangie ni la kitaifa zaidi. Hotuba hii haijajibu maswali ya msingi ya mkulima; leo mkulima anahitaji soko na sustainability ya price. Mheshimiwa Waziri amekuja hapa hakutuambia mikakati gani Wizara au Serikali inayo katika kuhakikisha kwamba wakulima wa korosho, ufuta, pamba na wakulima wa mazao mengine na kwa ndugu zangu hapa Wagogo, wana mkakati gani kuhakikisha tunapata soko. Tulikuwa tunategemea Serikali mnavyokuja hapa na hii bajeti, mnakuja kusema mipango kwamba tuna mpango moja, mbili, tatu wa kuweza kupata masoko. Mkulima huyu anakwenda kulima soko hamna mnategemea kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili la kusikitisha ambalo hili ni majonzi makubwa vilevile, Serikali haijaja na mpango wa kuweza kutuambia ni jinsi gani sasa wanaanza kufikiria jinsi ya ku-control price ya mazao haya. Wakulima wanapata shida kubwa sana, wanalima na kuuza katika mazingira magumu sana na wanavyouza vilevile price inayopatikana siyo ya kufurahisha, lakini malipo yenyewe vilevile hayapatikani kwa wakati. Tulikuwa tunategemea Serikijali ikija hapa mnakuja na mpango wa kutuambia kwamba katika bajeti hii mmejipanga kuweza kuona price inakwenda juu na vilevile wakulima wanakwenda kulipwa kwa wakati, lakini hilo halikuweza kuzungumzwa katika hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine cha kusikitisha zaidi hotuba hii haijagusa hata kidogo suala zima la matatizo ya ushirika. Sisi tulikuwa tunategemea kwamba Waziri akiwa anakuja hapa anakuja kutueleza kwamba jamani ushirika kule tunajua kuna matatizo kwa hiyo sisi kama Serikali tumejipanga sasa kwenda kufanya 1, 2, 3 ili kumkomboa mkulima huyu.

Mheshimiwa Spika, nataka nikwambie sisi katika Mkoa wa Pwani tuna kitu kinaitwa CORECU, ni shida. Tulikuwa tumekaa Wabunge sisi tukajadili, Mheshimiwa Ulega akiwepo, Mheshimiwa Mchengerwa na Wabunge wengine ambao tuko katika Mkoa wa Pwani, tumekwenda mpaka tukafikia hatua kwamba tumebadilisha uongozi katika CORECU ili kuweza kuona jinsi gani tunakwenda kumsaidia mkulima. Cha kusikitisha zaidi Serikali hamjaja na mpango halisia wa kutuambia ni jinsi gani mnakwenda kutatua kero ya mkulima wa pamba, kahawa, korosho, ufuta, katika suala zima la ushirika. Wabunge wengi wamesimama wamezungumza suala hili.

Mheshimiwa Spika, lakini lingine kubwa zaidi la kusikitisha, Serikali hamjaweza kutuambia mnafanyaje kuhusiana na ile interference katika suala zima la agriculture. Interference ina shida, mturuhusu sisi tulime.

Mheshimiwa Spika, without prejudice na kwa heshima na taadhima ya hali ya juu, sisi wakulima hatutegemei leo eti uende ukampe kishkwambi hicho Afisa Ugani aende kule chini Mchukwi, Ruaruke, Kipugila, Mkuranga kumsimamia mkulima, hiki kitu kinatoka wapi? Tuna data base ambayo tumeshaiandaa sisi kama Serikali, hakuna. Leo Mheshimiwa Waziri nikikuuliza kwamba tuna wakulima wangapi Tanzania you haven’t got a clue.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Ally Mpembenwe dakika zako zimekwisha, lakini kwa dakika moja tu kabla hujakaa chini ulianza kwa kuwalaumu kidogo kwamba hawakuwa na mpango wowote kuhusu umwagiliaji kuhusiana na Bwawa la Mwalimu Nyerere, sikukuelewa hapo unataka kusema nini?

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mradi ule wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unakwenda sambamba na mradi mzima wa umwagiliaji. Sisi watu wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, kuna ardhi nzuri kule tunategemea masuala ya hot culture yaweze ku-take place. Serikali hawajaja na mpango wa kueleza kwamba Bwawa hili la Mwalimu Nyerere mbali ya kwamba linakwenda kutoa umeme lakini vilevile linakwenda kuwasaidia wananchi kule katika zile ekari 150,000 kuweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji. Hii ilikuwa ni concern yangu kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.