Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nianze na dodoso tulilopewa. Kila Mbunge amepewa dodoso hapa la kujaza skimu za umwagiliaji kwenye eneo lake, hekari lakini mwisho wa siku hili dodoso tunalipeleka wapi maana bajeti imeshapita. Kama ni skimu za umwagiliaji wanazo humo ndani, hii tunapewa kwa faida gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, skimu ambazo ninazo, ninazo Skimu za Utuja, Simbo, Nyandekwa, Ndembezi, Mwashiku, Choma na Buhekela zote Wizara wanazo. Leo wananiambia niandike zingine nazitolea wapi? Hata hizo walizonazo hawajatupa hela hata shilingi moja; siyo ya kutengeneza, kuboresha wala kujenga, hata bwawa hakuna. Dodoso hili ni kwa ajili ya mwaka ujao? Dodoso hili tulipaswa tupewe mwezi wa tatu, mwezi wa nne…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na mchangiaji anayeendelea kuzungumza Mbunge wa Manonga, Mheshimiwa Seif Gulamali kwamba huo ni ushahidi wa namna ambavyo kilimo chetu kinachezewa. Huwezi kuleta dodoso katikati ya bajeti unategemea watu watoe input uende ukafanye kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa Seif?

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, ni sahihi kabisa. Mimi nilitarajia humu tungeambiwa sehemu fulani angalia tunarekebisha labda tumekosea kwenye bajeti hebu hakikisha, hamna kuhakikisha, hili nilitakiwa nipewe mwezi wa tatu nijaze ili wakathibitishe. Sasa leo hakuna fedha na hapa kwenye bajeti hii sijaona ujenzi wa skimu yoyote na mimi nina mabonde makubwa na tunalima mpunga kwa wingi. Hapa sikubaliani na dodoso hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine, ninayo mawili tu, nina kiwanda kile kinachotengeneza mbolea cha Minjingu. Mheshimiwa Waziri Mkuu tumemuona akienda Minjingu akituambia tutumie mbolea ya Minjingu. Waziri aliyepita na wa sasa hivi Minjingu lakini mbolea zinaagizwa nje ya nchi. Sasa tunaboreshaje viwanda vyetu vya ndani wakati nyie mnaagiza mbolea nje ya nchi? Hapa hatuelewani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Minjingu mbolea yao wananunua Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi sisi Tanzania tunafanya tafiti ya mbolea miaka mitano sasa. Tuna upungufu wa mbolea mahitaji tani laki tano Minjingu wanazalisha labda tani laki moja Wizara mmeshindwa kuchukua Minjingu tani zote laki moja halafu tani zingine laki nne mkawaambia wakaagiza nje ya nchi, mnaagiza zote nje ya nchi tani laki tano? Hapo hatuwezi kuelewana. Kama tunahitaji kulinda viwanda vya ndani, mnasema wenyewe watu wawekeze viwanda vya ndani anawekezaje wakati soko hana, soko lake nje ya nchi, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri akija ku-wind up hapa atuambie ni jinsi gani watalinda viwanda vya ndani kwa maana ya wote wanaozalisha lakini pia ….

T A A R I F A

SPIKA: Mwenye taarifa endelea nimekuruhusu.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza mchangiaji kwamba ile mbolea ya Minjingu ikiwekwa katika ardhi ya Tanzania itageuka kuwa sumu? Ahsante. (Kicheko)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea kwamba tunataka mbolea ile itumike hapa ndani, haiwezekani nchi nyingine watumie sisi kwetu tunaendelea kufanya tafiti. Hivi tukichukua hii Minjingu …

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Soko kubwa la Minjingu liko kwenye nchi zinazotuzunguka kama Kenya, Burundi na Uganda. Nampa tu taarifa kwamba baada ya kuona mbolea ya Minjingu inafanya vizuri sana kule Burundi kwa wale wateja aliokuwa anawapelekea, sasa ameamua kuja kuwekeza hapa Dodoma ili aendelee kuiua vizuri hii Minjingu, ni vizuri Waziri ajipange kwa majibu. (Makofi)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Seif.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, taarifa naipokea. tunazungumza hivi kwa kulinda viwanda vyetu vya ndani, tunalindaje viwanda wakati hatulindi viwanda vinavyozalisha mbolea ambayo tunaweza tukatumia sisi wenyewe? Niwaombe Wizara wakati wanakuja kujibu watuhakikishie soko la viwanda vya mbolea vilivyoko ndani halafu inapopungua ile gap ndiyo vitolewe vibali vya kununua nje ya Tanzania siyo unatoa vibali kwa ajili ya kununua mbolea yote nje ya nchi halafu iliyopo hapa ndani iende wapi?

Mheshimiwa Spika, kiti chako pia kitoe mwongozo kwenye suala hili kwani hatuwezi kwenda kwa stahili hii otherwise viwanda vingi vitakufa kwa utaratibu huu. Kama Kiwanda cha Minjingu kinaweza kutendewa hivi, je, viwanda vingapi vinaweza vikafanyiwa hivi? Kwa hiyo, tuombe kama kuna Wizara nyingine tofauti na Wizara hii inafanya utaratibu kama huu wa Wizara ya Kilimo tuuangalie tubadilishe. Ni lazima tulinde viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)