Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja. Naomba Serikali itengeneze mnyororo wa huduma na kuhudumiana (chain supply) ili uzalishaji wa viwanda vyetu ulenge kwanza kuhudumia mahitaji ya ndani (soko la ndani). Yapo mahusiano kati ya viwanda, masoko na ubora wa miundombinu ya umeme, maji, barabara, mawasiliano na uzalishaji wenye tija. Hivyo namwomba Mheshimiwa Waziri awasiliane kwa karibu na Wizara nyingine ili kuwe na matokeo chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri elimu itolewe ili wananchi na wataalamu, viongozi waliopo vijijini waelewe viwanda vinaanza na viwanda vyenye kuajiri watu 1, 2, 3, 4 - 9 hadi viwanda vikubwa. Wananchi hawaelewi kama shughuli wanazofanya kama usindikaji wa vyakula ni viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa data, naishauri Wizara iwe na utaratibu wa kuweka kumbukumbu (data) ili kuweza kuchambua maendeleo ya uendeshaji viwanda na matokeo yake kama vile idadi ya walioajiriwa Kiwilaya hadi Kivijiji. Hii itasaidia kufanya maboresho ya mara kwa mara. We need to have proper and useful information.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nashauri utafiti ufanyike mara kwa mara ili Wizara iweze kutoa ushauri, maagizo na maelezo ya namna Sera ya Uchumi wa Viwanda uweze kutekelezeka. Utafiti ufanyike pia ili tujue changamoto za uendeshaji wa viwanda na utatuzi wa changamoto kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la ufafanuzi kwa Waziri: Je, Mheshimiwa Waziri, Wizara ina mpango gani wa kuhimiza ushirika na wenye viwanda hususan viwanda vidogo vidogo ili iwe rahisi kuwafundisha kupima maendeleo yao na kuona kwa kiasi gani viwanda vimepunguza hali ya umasikini na kuongeza ajira?
Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango gani kuhimiza mafunzo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi hususan Jimboni Ushetu?
Je, tutawatumiaje vijana waliohitimu mafunzo ambao hawana ajira kushiriki na kutumika katika ukuzaji wa viwanda?
Je, Sekta ya Viwanda inapunguza kwa kiasi gani mfumuko wa bei kwa kusogeza huduma ya masoko karibu na wananchi?
Je, hadi sasa kuna changamoto zipi za kiteknolojia kifedha, kisera na kiutawala ambazo bado hazijatatuliwa na zinazokwamisha maendeleo ya haraka katika viwanda vyetu na kwa namna gani changamoto hizi zitatatuliwa?