Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii angalau niwasemee wananchi wenzangu ambao kwa asilimia 95 ni wakulima katika Jimbo langu la Singida Kaskazini. Uhai wa wana Singida Kaskazini unategemea sana zao la alizeti, lakini kilimo hiki wamekuwa wakilima kwa jembe la mkono jambo ambalo limeshindwa kabisa kutuletea tija ya uzalishaji wa zao hili kama ambavyo ingeweza kuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa zao la alizeti kuanzia kupanda mpaka kuvuna ni miezi mitatu tu lakini mkulima anakosa kulima kiwango cha kutosha kwa sababu ya changamoto hasa hasa za vitendeakazi. Zana za kilimo, mbegu pamoja na mitaji. Nikuombe sana na niiombe Serikali, Wizara hii watuletee mbegu na mbegu hizi ziwe kwa bei ya chini ili wakulima waweze kumudu gharama. Haiwezekani kilo mbili ziuzwe shilingi 60,000 na zaidi halafu gunia moja lije liuzwe 50,000. Hii inamuumiza sana mkulima na inampotezea muda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi niombe sasa Serikali tuhakikishe kwamba tunaleta kilimo cha irrigation, cha umwagiliaji. Katika Jimbo la Singida Kaskazini mabwawa matatu yameungana imekuwa ziwa. Niombe sasa maji haya yatumike ipasavyo kwa kuleta miundombinu ya umwagiliaji ili vijana waliojitokeza waliohamasika kutumia maji haya walime hata wakati wa kiangazi. Bwawa la Masoqeda, Kisisi, yameungana yamekuwa ni ziwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana maji haya Serikali iyatumie ipasavyo kwa kuhakikisha vijana wanapelekewa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuongeza tija katika uzalishaji wa alizeti na hata viwanda vilivyopo pale viweze kupata raw materials ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasahivi viwanda vinakosa malighafi kwa sababu tunazalisha kwa kiwango kidogo sana na kwa mwaka huu alizeti haijalimwa kwa sababu ya kukosekana mbegu na bei kuwa ndogo. Kwa hiyo, watu wanaamua waende kwenye mazao mengine na kuachana na alizeti. Ndiyo maana mnaona mwaka huu mafuta yamepanda bei na yameadimika kabisa. Kwa hiyo, niombe sana eneo hili litazamwe kwa jicho tofauti sana. Nashukuru kwamba zao la alizeti limeingizwa kwenye yale mazao ya kimkakati, basi isiwe ni kwenye makarasha tu. Yaende kwenye utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongee kidogo kuhusu zao la kitunguu ambalo ndilo hasa sisi watu wa Singida tunalima kitunguu bila kutumia madawa. Ni kilimo cha asili kabisa, unapanda kitunguu, unavuna bila kutumia dawa. Kitunguu hiki hakijawekewa mkakati, ni mkulima mwenyewe anahangaika kwa nguvu zake binafsi, hakuna mkono wa Serikali hata kidogo. Sisi tunaishia tu kujivunia kwamba watu wanalima lakini hatuwasaidii. Tuhakikishe tunawapelekea hawa watu mbegu. Subsidies zipelekwe kwenye mbegu lakini pia tuwape vijana mitaji waweze kuongeza tija, waweze kuzalisha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa spika, lakini hapo hapo eneo la masoko, soko la kitunguu lipo lakini shida ni utaratibu mbovu unaopatikana pale sokoni. Mkulima anapopeleka zao lake sokoni utaratibu ni mbovu anaishia kuteseka madalali wajanja wajanja.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, sasa ni vyema utaratibu mzuri uwekwe ili watu hawa nao wanufaike na kilimo chao hiki wanachoteseka nacho muda mrefu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa haya machache. Naunga mkono hoja lakini niiombe Serikali itusikie haya tunayoyazungumza. (Makofi)