Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii maalum sana, Wizara ya nguvu, Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa na hoja tatu tu za kusema leo; hoja mbili naomba nizungumze hoja za Kitaifa, na hoja moja kubwa nizungumze Jimbo langu la Same Mashariki.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tunaishi na Serikali humu ndani. Wakati Serikali inafanya jambo zuri, ni vyema Wabunge tujifunze kuisifu Serikali. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na mama Samia Suluhu Hassan, mpaka sasa tuliposimama hapa, inakwenda vizuri sana upande wa Mradi wa Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu Mradi wa Rufiji Serikali ilipoanza kulikuwa na maneno mengi sana. ukweli naomba niipongeze Serikali kwa kuthubutu. Serikali imefanya kitu ambacho wengi tulikuwa hatukijui vizuri, lakini mpaka sasa hivi Serikali imefanya mradi ambao ni mkubwa kweli katika Afrika Mashariki. Na Mradi huu wa Umeme wa Rufiji katika Afrika Mashariki ni wa kwanza wa kipekee.

Mheshimiwa Spika, ukija katika Afrika nzima, mradi wenye hadhi hii nikiri wa kwanza uko Ethiopia, tukubali; wa pili uko Nigeria; wa tatu uko angola; wa nne uko Tanzania. Tumepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, na ninakumbuka nilikuwepo humuhumu ndani, kulikuwa na migongano mingi nje ya nchi, huko ulimwenguni walisema maneno mengi. Nimpongeze Rais wa Awamu ya Tano, alisimama imara sana, tena alitumia nguvu nyingi sana; Mungu amuweke mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Megawatt 2,113 siyo ndogo. Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla tutaona mafanikio makubwa mradi huu utakapokwisha. Mradi huu umefikia asilimia 52. Nimpongeze na Waziri wa Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, Waziri wa Nishati mwaka 2017 ndio alianza hii Wizara hapa, zilikuwa zipo mbili; Nishati na Madini. Zikatenganishwa 2017, huyu kijana akachukua hii Wizara.

Mheshimiwa Spika, nikiri kabisa na niseme ukweli Mheshimiwa Waziri, ukitembea mtu hasikii hata hatua zako zinavyokwenda, lakini unakwenda mbio sana, unajitahidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niseme; sina kawaida ya kusifu Mawaziri, lakini huyu kijana nimeona leo nimwambie ukweli, jitahidi sana, tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine kikubwa; huu mradi tunaujenga kwa pesa zetu wenyewe Watanzania jamani. Huu mradi ni mradi wa trilioni 6.5; hatukukopa mahali, hatukupewa msaada, zote ni pesa za Watanzania. Hivi kwa nini tusijivune? Trilioni 6.5 siyo pesa ndogo, ni hela zinazotaka uthubutu mkubwa. Nawapongeza sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, na ninaomba niwaambie ukweli; leo nimeamka vizuri sana.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa mama Kilango; ni kwamba kitu kinachofurahisha mkandarasi hadai hata senti tano kwa kazi alizofanya. Kwa hiyo, Serikali imefanya vizuri na Mheshimiwa mama Samia, Rais wetu, anaendeleza gurudumu lilelile. (Makofi/Vigelegele)

SPIKA: Mheshimiwa Kilango, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, tena naipokea kwa unyenyekevu. Mheshimiwa mama Manyanya, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, naomba niseme ukweli; tusipoisemea Serikali yetu vizuri, nani ataisemea? Ni sisi tumeiweka madarakani. Tumepambana tukashinda; Chama Cha Mapinduzi, Serikali inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo nimempenda sana; huu mradi wa kupeleka umeme vijijini. Nilikuwepo tangu mwaka 2000 humu ndani, niliona umeme ulivyokuwa unasuasua, niliona. Nilikata tamaa. Lakini katika vijiji 12,268 vya nchi yetu sisi, leo hii kuna vijiji 10,312 vimepelekewa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kama umeme umefika kijijini haujaenda vitongojini, lakini ni mwanzo mzuri kwamba umefika vijijini next utakwenda kwenye vitongoji vyetu. Serikali mmenifurahisha sana katika hilo pia, haswa sisi mnaotuona tulio simama hapa wengi wetu tunatoka vijijini, tumezaliwa vijijini, tumekulia vijijini bado tupo vijijini huku tumekuja kutembea sisi ni watu wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia 86 ya vijiji vyetu tayari wameona umeme, tuishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na ile mikakati Wabunge mlioiweka hapa kwamba chukueni pesa hapa kwenye mafuta pelekeni huku mkakati ule ulikuwa mzuri sana. Ulikuwa mkakati mzuri sana, lakini niseme ukweli mnakumbuka mwaka 2015 ambao mpo sawa tulikuwa namba 39 katika nchi 54 za Afrika tulikuwa namba 39, nikisema hivyo sijui mnanielewa, kwamba katika nchi 54 za Afrika tulikuwa namba 39 kwa kupeleka umeme vijijini. Leo tukizungumza hapa katika Afrika sisi ni namba moja katika kupeleka umeme vijijini, hivi hapa mtasema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inacheza? Inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Naomba niipongeze Serikali sana, sasa naomba niachane na Serikali naomba tugombane kidogo na Serikali. Naomba nigombane na nyie kidogo ili mfanye kazi. Nimezungumza kitaifa sasa naenda kwa walionichagua jamani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri naomba uniangalie vizuri, nimeingia Jimbo la Same Mashariki mwaka 2005 nikawa nasema humu ndani nagombana na Ngeleja, nagombana na Muhongo kuhusu umeme wa Tarafa ya Mambavunda, wananchi wangu wanaishi mlimani sana na wanapoishi kule wanaishi na migomba, na miti, mitangawizi kuna giza sana, nilisema kwa miaka tisa, 2014/2015 Serikali ndiyo ilipoona ikanipa pesa za kupeleka umeme katika Tarafa ya Mambavunda, nikashukuru, nikafurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha kwanza nilichokiona kinaitwa Mwala kilipata umeme mwaka 2015 nikafurahi nikaona umeme. Mradi ule Serikali ilisema utakwenda 2015, 2018 utakwisha, wananchi wakafurahi, wakashangilia, leo ni 2021mradi ule 2015 ulikwenda kidogo ulisimama, 2015 ukasimama, 2016, 2017, 2018, 2019 waziri juzi ndiyo umeanza kidogo.

Mheshimiwa Spika, nasimama vizuri kukwambia waziri huu mradi wale wananchi walitegemea sana nao waingie kwenye taa, waingie kwenye mwanga, mliwaacha tangu 2015 mkaenda vijiji viwili,vitatu tu mradi huu mpaka leo nimeanza kwa kuwasifu Serikali narudi kuwaomba tafadhalini huu mradi umalizeni, hawa watu mliwapelekea taa kidogo vijiji viwili, vitatu mradi huu ni wa tarafa nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu mradi ulikuwa uende Vunta, uende Papa, uende Miombo, Uende Mwala, uende Kidandini, uende Mwateni, Njagu, Kirangare, Makasa, Mshewa, Pangani, Vugwamakati, Hedaru, Mweteni, Tambwe, Tintin na cha Nguruwe. Mlikwenda sehemu kama tatu tu, sasa mimi ni Mbunge Same Mashariki kama mlilala hapo katikati sababu siijui, leo nakwambia Mheshimiwa Waziri utoe majibu kwa wale wananchi kwanini ulisimama tangu 2015. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,umerudi kuanzia 2020 hapa mwishoni niliuona nimekwenda mwenyewe naona una wakandarasi kule, lakini wananchi wangu wana wasiwasi kwamba huenda utasimama tena, naomba Mheshimiwa Waziri sitakamata shilingi, lakini uniambie kwanini ulisimama, na utamaliza lini huu mradi.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, sitaunga mkono hoja kwanza. (Makofi)