Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa nafasi ambayo umenipatia.

Mheshimiwa Spika, nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wanafanya na wanaendelea kufanya.

Mheshimiwa Spika, pale Geita Mjini miaka miwili iliyopita tulizindua ujenzi wa substation katika Kata ya Mtakuja ambapo mimi pia nilikuwepo na Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake aliahidi baada ya miezi nane watu wa GGM wataanza kutumia umeme kutoka kwenye ile substation. Substation ile inatoa megawatts 98 na imekwishakamilika nadhani sasa karibu mwaka. Pia katika ahadi zake Mheshimiwa Waziri alisema kwamba Kata hiyo ambayo substation hiyo ipo ya Mtakuja ambayo ipo kilometa mbili tu kutoka makao makuu ya mji itapata umeme kutoka kwenye mradi huo.

Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza leo mradi ule umekamilika, Kata ile ina vijiji 11 hakuna kijiji hata kimoja kimepata umeme. Sasa nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri sijui ilikuwa sio sehemu ya package ya mradi huo, sijui kama mradi huo unaendelea, kwa sababu mpaka leo navyozungumza nashindwa kwenda kuzungumzia ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Mtakuja kwa sababu mkandarasi keshandoka site na wananchi hawajapata umeme mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, kata katika Jimbo la Geita Mjini zimechelewa sana kupata umeme katika awamu zote tatu. Nimeingia kwenye Bunge hili nikakuta nchi nzima vijiji 2,000 ndiyo vina umeme leo tunazungumzia vijiji 10,000 lakini katika Jimbo la Geita Mjini kata sita hazijapata umeme mpaka leo. Ukiwafuata TANESCO wanakuambia huko ni REA, ukiwafuata REA wanakuambia huko ni Peri-Urban ukienda Peri-Urban wanakuambia hawana pesa, amekuja mkandarasi wa kwanza, wa pili sasa wa tatu. Wananchi wa Jimbo la Geita Mjini wanakusikiliza Mheshimiwa Waziri, Geita Mjini siyo Mjini pale tuna kata 14 na kata zingine zote ziko nje ya Geita Mjini wanataka kujua wanapata lini umeme; Kata za Shiloleli, Bulela, Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Mtakuja ambako kule kote watu wako wa kufanya survey wamefanya zaidi ya mwaka mmoja lakini umeme haujaenda.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi sijui inakuwaje Mheshimiwa Waziri alikuja siku moja akazindua umeme kwenye kijiji kimoja alipoondoka hakuna tena kwenye kata hiyo kijiji kingine kilichopata umeme leo mwaka mmoja na nusu. Sasa sielewi anapoondoka anasimamisha zoezi la usambazaji wa umeme mpaka arudi tena au inakuwaje?

Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa kampeni tumefanya zoezi zuri sana la kutoa umeme mjini kuupeleka Nyanguku na Nyanamilo, mwezi wa saba mpaka leo nguzo zimesimama hakuna kinachoendelea. Ukiwauliza TANESCO wanakuambia subiri Peri-urban inakuja. Kwa sababu ya muda Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha naomba awahakikishie wananchi wa Geita Mjini kata hizo nilizozitaja wanapata lini umeme.

Mheshimiwa Spika, nilizungumzia hapa wakati nachangia kwenye Mpango inawezekana shida iko sehemu moja, leo hii pale pale mjini watu wamelipia umeme wana miezi saba hawajapata umeme. Wanalipia umeme palepale mjini wanasubiri miezi sasa nikasema inawezekana centralization yenu ya supply inachelewesha watu kupata umeme. Kwa nini msitafute mfumo mwingine wewe unazalisha umeme running cost zako ziko constant unahitaji wateja wengi uweze kupata faida inachukuaje miezi saba unafanya biashara hujamuungia mtu umeme na mteja yupo?

Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri angalie vizuri watu wake wa planning na biashara kwa nini hawawezi kutafuta mbinu mbadala, unakaa na wateja 400 wamekulipa hauwaunganishii umeme kila siku unawaambia vifaa hakuna, vifaa hakuna wapi? Kama haiwezekani wewe ku-centralize supply tafuta watu ambao utakuwa na uhakika na quality za vifaa vyako ili mtu anapolipia leo kesho apate umeme. Haiwezekani wewe unazalisha umeme lakini wateja wapo halafu mtu amekulipa miezi sita yupo anasubiri, akienda hapa anaambiwa vifaa hakuna au hiki hakuna, kwa nini wakati source zipo? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tazama vizuri hawa watu wako inawezekana kupata source za vifaa sehemu zingine kwa quality unayoitaka kama wanavyofanya watu wa idara zingine ukaweza ku-supply umeme bila kumchelewesha mteja kwa miezi mingi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nakushukuru sana. (Makofi)