Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara na Watendaji wake wote katika Wizara hii. Pia nawapongeza sana Kamati kwa taarifa yao nzuri na uchambuzi wao mzuri sana ambao wameufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa miongozo yake ambayo ameitoa na hasa katika eneo la kumaliza migogoro ambayo imewagharimu sana wananchi, wafugaji na wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kwenda kwenye Randama ya Waziri ukurasa sita na wa saba. Kwenye ukurasa wa sita kwenye item namba nne kwenye malengo mahsusi ya Wizara, Mheshimiwa Waziri amezungumza namna ambavyo maelekezo ya Serikali ya kumaliza migogoro ya ardhi ambayo inahusisha wananchi wanaokaa karibu na hifadhi na pia migogoro inayohusisha wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa saba wa randama ya Mheshimiwa Waziri na nikikariri hotuba ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. Magufuli, ambayo imeeleza vizuri namna ambavyo lengo la Serikali ni kufikia watalii bilioni tano na kuongeza mapato kutoka bilioni 2.6 za sasa za mwaka 2016 kwenda mpaka shilingi bilioni tano ndiyo malengo ya Wizara katika miaka mitano ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuangalia katika maeneo hayo mawili, naomba nianze kwa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba Mheshimiwa Rais, mwaka 2019, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua uwepo wa migogoro mingi sana nchini, mwezi wa Tatu, tarehe 15 aliagiza kuundwa kwa kikosi kazi cha Wizara saba kikiongozwa na Wizara ya Ardhi kushughulikia na kushauri namna gani Serikali inaweza kumaliza migogoro katika maeneo mengi ambayo yamekuwa yakiwakabili wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu, kazi kubwa katika eneo hili ilifanyika. Tulikuwa tunazungumzia maeneo yenye migogoro, vijiji 366, ikaja ikagundulika ni zaidi ya 1,000, lakini katika uchambuzi uliofanywa katika hiyo joint committee ilionekana karibu vijiji 975 vitaendelea kuwepo kutokana na mazingira na baadhi vilionekana vitashughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu hapa ni ya msingi kwamba nataka kufahamu maamuzi haya ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyatolea tangazo la Serikali na kuahidi utekelezaji; utekelezaji wake unafanyika lini? Kuchelewa kufanyika kwa utekelezaji huu kunawagharimu sana wananchi. Nataka nitoe mfano; katika Jimbo langu la Geita Mjini, msitu wa Hifadhi wa Usindwake na msitu wa Geita Kata ya Mgusu asilimia 80 wapo ndani ya eneo ambalo zamani na mpaka sasa linahesabika kwamba ni hifadhi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha asilimia 80 kuwa katika hifadhi maana yake ni kwamba makazi yamo ndani ya hifadhi, wakulima wamo ndani ya hifadhi na mifugo waliyo nayo inachungwa ndani ya hifadhi. Sasa wananchi hawa wanakamatwa kila siku na wanapokamatwa hawakamatwi kwa sababu ni makosa yao ni kwa sababu tayari kuna shule, tayari kuna zahanati, tayari kuna barabara, tayari kuna shughuli za kiuchumi zinaendelea maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali kumaliza tatizo hili. Tayari lilishatolewa maelekezo, sasa sielewi anatekeleza nani? Wizara yako Mheshimiwa Waziri Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi au Wizara gani? Ninachojua ni jukumu la Serikali kumaliza mgogoro huu ambao unawagharimu wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, faini katika maeneo haya ni kubwa sana. Anapokamatwa mfugaji ameingiza mifugo kwenye hifadhi, faini zake ni kubwa. Tuliona kwenye hotuba ya Wizara ya Kilimo na Mifugo, karibu ng’ombe milioni sita zimekamatwa, zimetaifishwa; na ni kwa mujibu wa sheria. Sasa lazima tumalize migogoro hii kwa maelekezo ya Serikali. Nataka kujua kwa nini utekelezaji wa maagizo haya unaendelea kuchukua muda mrefu? (Makofi)
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Olelekaita.
T A A R I F A
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe tu mzungumzaji taarifa, kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii tarehe 1 Januari, 2021 alitoa tangazo lifuatalo: “Ninyi ni Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu, fanyeni kazi zenu za kulinda maeneo mliyokabidhiwa kama kawaida. Mkikuta kuna ng’ombe wanamilikiwa na Dkt. Damas Ndumbaro, ninyi kamateni, msije mkasema ng’ombe hawa ni wa Waziri, tuwaache, ninyi mkamate na mwapige mnada kama kawaida. Ng’ombe watakaokutwa ndani ya Hifadhi ni shilingi 100,000.” Nataka tu nimpe taarifa kwamba hili tangazo siyo kwa mujibu kwa sheria. Hakuna sheria inayosema ng’ombe atozwe kwa kichwa shilingi 100,000. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa John Constantine Kanyasu, unaipokea taarifa hii?
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo na ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, pengine na Mheshimiwa Waziri wa Sheria watoe ufafanuzi kwenye hiyo sheria. Kwa sababu, hiyo sheria ukiitazama haimpi absolute right anayekukamata kupiga hiyo fine. Ina vipengele vyake ambavyo vinakuwa attested kufika kwenye fine hiyo. Kutokana na ignorance ya wananchi wetu huku, it is direct, ukikamatwa mara shilingi 100,000/=, sasa utatengeneza masikini wangapi katika nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja yangu ya pili ambayo lengo letu ni kufikisha watalii milioni tano. Kwanza niendelee kuwapa pole wahifadhi wetu Tanzania kwa sababu, kuja kwa COVID kumewarudisha nyuma. Walikuwa wanakwenda vizuri sana, nilikuwa ninaamini baada ya muda mfupi tungelikuwa ni nchi ambayo inaongoza kwa utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili katika Afrika, nchi ambazo zinafanya vizuri sana katika utalii, Morocco wanapata watalii milioni 12.3 ambao maeneo mengi sana wanachokwenda kuangalia kule ni cultural, pamoja na utalii ambao unahusisha sana mambo ya vyakula na maeneo mengine ambayo yamekuwa ni ya asili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Egypt milioni 11.3; huko nako ni cultural na maeneo makubwa hapa ni pyramids pamoja na kuangalia Pharaoh Tombs na kadhalika. Eneo la tatu, ni South Africa, hawa wanapata watalii milioni 10; most popular ni kwa sababu ya safari na kitu kinaitwa MICE, mikutano ambayo inafanyika South Africa. Katika Afrika kwa mujibu wa International Convention and Conference Association, South Africa wanaongoza kwa Afrika nzima kwa ku-host mikutano mingi sana ambayo inapeleka watu wengi kule nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya nne ni Tunisia ambayo inapata watalii milioni 8.3 na nchi ya tano ni Zimbabwe. Nini kinawapeleka watu Zimbabwe? Ni kwenda kuangalia Victoria Falls. Sasa hapa nataka kuzungumza nini? Katika orodha yote hii ya nchi tano, kimsingi nchi ambayo kidogo watalii wanakwenda kwa ajili ya kuangalia wanyama ni South Africa. South Africa ni kwa sababu ya improvement yake katika miundombinu na namna ambavyo wametengeneza mazingira ya kufanya watalii waweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi nyingi ambazo zinaongoza katika utalii, kinachowapeleka kule ni cultural pamoja na heritage centers ambazo ziko katika maeneo yale. Sasa ukiitazama vizuri Tanzania, ukaacha zile traditional products zetu zinazoleta watalii kwa maana ya safari, beach, labda kwa maana ya hunting na vitu vingine. Bado tuna- lack product ambayo inaweza kutuletea watalii wengi kwa mara moja na kufikisha watalii milioni tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka ni-emphasize jambo moja, katika Afrika Mashariki, Rwanda sasa hivi wamekuwa waki-host mikutano mikubwa sana kidunia. Kwa nini? Kwa sababu ya ile Kigali Convention Center. Wametengeneza Kigali Convention Center ambapo inafanyika mikutano mikubwa sana ya dunia. Nataka tu nitoe mfano; wamekuwa na Mkutano wa Force Agenda Summit, ambao ulikusanya maelfu ya watu; Mikutano ya Mo-Ibrahim, wamefanya mikutano ya GMSA ya Mobile 360, wamekuwa na mikutano mingi ambayo imeleta watu kutoka maeneo mbalimbali. Why Rwanda?
Moja, kwa sababu kwanza ni free VISA. ukiingia Rwanda unatoka dunia nzima, ukifika Kigali unakutana na VISA baada ya kufika, VISA on arrival. Hii imeondoa sana usumbufu, kwa hiyo, unaweza kwenda maelfu na maelfu ya mikutano pale na ukafika ukafanya mkutano wako lakini utapata VISA on arrival. Pia ni rahisi kupata VISA kwa masharti mepesi bila usumbufu wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, connectivity. Rwanda hana Shirika kubwa sana la Ndege, lakini anachokifanya ana ndege ndogo ambazo zinaweza kukupeleka kwenye activity nyingine. Kwenye eneo hili la mikutano anayeongoza ni South Africa, wa pili ni Rwanda; tatu hapa tuna Ethiopia, tuna Kenya, tuna Uganda. Why Kenya na Uganda na wenyewe hivyo ni connectivity. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa, tunayo haja kubwa; watu wanaokuja kuangalia Wanyama, anaweza akaja mara moja na asirudi tena, lakini anayekuja kuangalia cultural, anaweza kuja mara ya kwanza, akarudi mara ya pili. Kwa hiyo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimalizie eneo moja kwamba kutoa ushauri wangu. Tunaomba kuishauri Serikali kutafuta uwekezaji mahususi kwa ajili ya kuhamasisha…
NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: …utalii wa mikutano katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.(Makofi)