Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa tena nafasi hii. Naitwa Riziki Said Lulida, Mama Tembo, Mama Mjusi, Mama Selous na ni Balozi wa Utalii. Nataka niwapongeze kwa dhati katika Wizara ya Maliasili ikiongozwa na Waziri na Naibu Waziri. Pia kuna watu wamefanya kazi kubwa ya kusimamia utalii na maendeleo ya wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitawataja kwa majina; kwanza inaongozwa na Mheshimiwa Ndugu Allan Kijazi. Kwa kweli amefanya kazi kubwa. Mheshimiwa Fred Manongi wa Ngorongoro, mpaka wanazeekea ndani ya utalii na kuweka heshima kubwa ya nchi hii. Wamefanya kazi kubwa. Bwana Silayo Dosantos katika TFS, mmeona hata mapato ya misitu yamekuwa makubwa na bila kusahau na wahifadhi wengine ambao wana upendo, ikiwemo sisi Wabunge ambao ni Ma- champion wa kupenda maendeleo ya utalii ndani ya nchi hii. Tanzania ili tuendelee tunahitaji mapato ambayo yataisaidia nchi hii.
Katika upande wa maliasili ya Tanzania watalii wanakuja kwa ajili ya masuala ya wanyama watano tu, big five ambao ni Simba, Tembo, Nyati, Chui na Faru. Bila hivyo, kuwahifadhi hawa wanyama, basi hatutaweza kufanikiwa, tutarudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie wenzetu Kenya, Masai Mara ni eneo dogo sana, lakini wamefanya kazi kubwa sana ya kutangaza utalii kwa kupitia Masai Mara. Sasa nataka nami niwasaidie vile vile tuweze kufanya kazi ili tuweze kupata pato kubwa, kumsaidia Mheshimiwa Mama Samia Suluhu katika eneo hili la utalii, kama alivyokuwa champion kuhakikisha kuwa Tanzania yenye mapato ya ndani kupitia Hifadhi zetu pamoja na maliasili yetu inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo hayo ni kama ifuatayo: kama alivyozungumza ndugu yangu Kanyasu, kwa kupitia International Conferences na Global Summit kule ndiyo watu wanakwenda. Niulize TANAPA imewahi kwenda katika mikutano kama hiyo? Hawana Fund. Ujiulize Ngorongoro wanatangaza maeneo kama hayo? Hakuna. Hivyo lazima tutarudi nyuma na wenzetu wanatupita kwa ajili ya kutangaza na kuhakikisha matangazo yao/promotion zao na marketing zinakuwa kubwa na ndiyo maana unaona tunapitwa mpaka na Masai Mara ndogo kama ni wilaya tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kupitia airlines; leo ingia katika KLM unaiona Kenya inatangaza, come to Kenya and visit Serengeti, Ngorongoro and Zanzibar. Sasa unajiuliza, tunakwenda wapi? Kwa nini wamefikia pale? Ni kwa sababu wanatangaza matangazo makubwa sana ya kidunia na ndiyo maana mapato yanapatikana. Kwa kupitia ma-tour operators, wengi wanakwenda, mimi nimewahi kutembea nao, lakini ni wachache. Wengi hawafanyi kazi ya kutosha. Kama wangefanya kazi ya kutosha, Tanzania hii ambayo tuna mbuga nyingi, tumeambiwa sasa hivi TANAPA wana 22. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tungekuwa tumezipita nchi za Afrika zote kwa mapato, lakini kwa vile bado hatujajitangaza inabidi tufanye kazi kubwa ya utalii wa ndani. Tufanye kazi kubwa; na Watanzania hata Wabunge humu ndani; kuna Mbunge mwingine ukimwita unakujua Serengeti? Atakwambia mimi sikujui. Tulete mafunzo ya kutosha, tutembee nao Wabunge hawa wakaone haya yanayozungumzwa. Mimi ni Mwenyekiti wa kupambana na ujangili ndani ya Bunge; nimetembelea mbuga, ndiyo maana nimeiokoa Mbuga ya Burigi, imerudi katika Hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanyamapori inabidi walindwe, lakini na wafugaji wanaingia ndani ya mapori wakiwa na ma-rifles na mabunduki makubwa sana. Wengi wao wanakwenda kibiashara na katika uindaji haramu. Kupitia mimi, nimekwenda pale kwa kuwa nimenyanyaswa kwa vile ni mfugaji, haikubaliki. Mimi naikataa hiyo. Naomba mafunzo yaje kila mara ili Wabunge waelimishwe. Wakielimishwa Wabunge kazi hii itakuwa rahisi. Tulikuwa na Mheshimiwa Keissy, alikuwa champion wa kupambana kuona wafugaji wanaonewa. Nikamwambia utaingia Kamati ya Selous. Aliyoyaona, mwenyewe amekuwa mpenzi mkubwa wa wanyamapori na tukamaliza migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la mjusi. Najua muda wangu ni mdogo sana. Nimelizungumzia suala la mjusi toka mwaka 2005. Hii maana yake, nami nahisi hata uchaguzi wangu nimekuja ili kuhakikisha suala la mjusi tunalimaliza. Nawe Mbunge, kama Naibu Spika ni champion naomba uwe mmojawapo katika ma-champion wa kupambana na kuhakikisha pato la mjusi linarudi katika nchi hii. Kwa maslahi mapana ya nchi yangu, nasema karibu sana. Tuko Wajumbe 20, lakini naona na wewe hutalikataa hili, unakaribishwa sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, mjusi, fossils ambazo zimetoka Lindi, sasa hivi ziko sita Ujerumani. Vile vile tumeambiwa duniani kuna ndege wakubwa sita wametoka Tanzania, wako Ujerumani. Wengine wakaniambia, mama bado, ongeza harakati. Kuna vyura wa Kihansi, wako Marekani. Tunataka tujue sisi tunafaidika nini na vyura wa Kihansi ambao wako Marekani? Tumeambiwa tena kuna chameleon wako Australia. Tunataka kujua kule Australia tunapata faida gani na wale chameleon wetu wale, hawa naniiā¦ (Makofi)
NAIBU SPIKA: Chameleon kwa maana ya kinyonga au?
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, eeh, ni vinyonga. Nisamehe sana, nimesahau Kiswahili kidogo, lakini nitazidi kujitahidi. Chameleon wako Australia kule, lakini tunataka kujua tu wamefikia vipi? Bado ni maliasili, inabidi tuisimamie na tupambane nayo. Kuna vichwa vya watemi viko Ujerumani, vilichukuliwa miaka mingi sana. Tunaomba tusimamie nayo. Hivi tunachozungumza, suala la hakimiliki, hata kama walichukua wakati wa Ukoloni, lakini Tanzania it is the sovereign state na tunajua kabisa Balozi wa Ujerumani amemleta mwakilishi wake. Tunataka tukitoka hapa mwezi wa Saba tunakwenda kufanya event kubwa Tendeguru na tunataka tutengeneze MoU, Tanzania ipate tozo kutokana na mapato ya mjusi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haki ya mtu hailiki, ni lazima tupambane nayo na tukipata pato lile, nina imani kwamba nitakapoondoka hapa Bunge nitakuwa nimeacha legacy kubwa sana na kuhakikisha Wabunge wenzangu wanapotoka hapa, watakuwa champion wa kusimamia maliasili yetu ya Tanzania ambayo inatoweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia suala la NIASA Selous Corridor; ni kama la Serengeti, Masai Mara. Wanyama wanatoka Tanzania Serengeti wakielekea Kenya na imetangazwa sana, lakini hii ya Tanzania ya Selous NIASA haijatangazwa. Hii ni Mbuga rasmi ya tembo. Nataka nikuambieni tu angalizi, hii mbuga imevurugwa sana na kutoa vitalu pembeni kabisa anapopita tembo. Hivyo, ina maana tembo akipita pale anavurugwa.
Nilihudhuria katika Mkutano wa WTO wakasema Tanzania it is a lost Eden. Mmeiacha Eden nzuri ya tembo inavurugwa na matokeo yake kwa vile Wabunge hawajui wanachokizungumza, wanaona wanaonewa, kumbe wao wanawaonea wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, corridor zote za wanyamapori zimekuwa intervened. Sasa unajiuliza, tembo inabidi apite katika Miombo Forest, atapita wapi na ninyi mmeshaiharibu? Misitu mmeshakata, mmefanya fujo kubwa ya kukata misitu. Je, hawa wanyama watakwenda wapi? Simba wamemalizika mpaka hadi mwisho Serengeti unauliza, sharubu yuko wapi? Hii yote ni fujo ya binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mikoa ambayo hata umwambieje, yeye kila siku anataka kula kimolo. Wanajijua wenyewe! Sasa ukiona watu wale wanapenda nyamapori maana yake wao ni majangili, ni watu ambao wanafanya uharibifu mkubwa kwa wanyama. Tulikuwa na tembo kuanzia 2,000,000, wakaisha wakafika mpaka 300,000, wakafika mpaka 100,000, wakaisha mpaka 10,000. Tushukuru katika Serikali ya Awamu ya Tano tumewarudisha mpaka 47,000. Bado hatujafikia kundi la tembo tunalohitaji. Sasa kinachofanyika ni majangili wanafuata tembo. Wakiwafuata tembo, ni lazima na tembo naye atakuwa hakubali, atawaua. Sasa hapa lazima tukae chini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana. Napenda wanyamapori, napenda uhifadhi na utalii. Ahsante sana.