Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa nianze na kuipongeza Wizara iliyoko chini ya Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Ndumbaro pamoja na Naibu Waziri kwa namna wanavyoweza kufanya kazi vizuri; na kwa ushahidi tu wa pekee kwa sababu pia hata tarehe 22 aliweza kutembelea kwenye Jimbo langu hasa kwenye Kata tatu. Kata ya Kalulu, Jakika na Matemanga. Amejionea mwenyewe namna tulivyokuwa na kero kubwa ya tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, nianze tu moja kwa moja na kueleza kwenye jimbo langu halafu baadaye nifuate Taifa. Jimbo la Tunduru Kaskazini kwa maana ya Wilaya ya Tunduru, tuna hifadhi za Taifa tatu na pia tuna hifadhi ya misitu ya asilia moja kwa maana ya Mwambesi na vile vile tuna hifadhi za wanyamapori za jamii mbili, yaani Nalika na Chinguli. Vile vile tuna hifadhi za misitu asilia ya vijiji, saba. Kwa hiyo, utaona ni namna gani wilaya hii ilivyozungukwa na hifadhi za wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, yako maeneo mahususi kwa ajili ya ufugaji, lakini pia yako maeneo mahsusi kwa ajili ya ukulima na sisi wilaya yetu ni mahsusi kwa ajili ya kilimo. Tunalima korosho, mpunga, ufuta mbaazi na kadhalika, lakini kero kubwa ambayo tunaipata kutokana na kilimo ni kutokana na wanyama wakali na waharibifu, yaani tembo. Nikizungumzia athari kubwa ambazo tunazipata kutokana na wanyama hawa waharibifu na wakali, kwa miaka mitano tumepoteza maisha ya watu 24 kutokana na tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015/2016 waliuawa watu wawili na tembo; mwaka 2016/2017 waliuawa watu wawili; 2017/2018 waliuawa watu saba na tembo; 2018/2019 waliuawa watu wanne; na 2019/2020 waliuawa watu tisa. Kwa hiyo, utaona takwimu ni namna gani watu hawa wanavyozidi kuongezeka kuuawa. Kwa hiyo, kero hii isipotatuliwa kwa umakini maana yake tunakwenda kupoteza nguvu kazi kubwa kweli kweli. Vile vile wanyama hao hao waharibifu kwa maana ya tembo, wameacha vilema vya kudumu kwa watu 20 kwa miaka mitano tu. Vile vile, ekari zilizoharibiwa na tembo zinazidi 4,679. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii nakueleza uone ni kwa sababu gani tuna kero hii kubwa ya tembo katika wilaya yetu ya Tunduru. Sababu kubwa moja ni wafugaji kwenda kufuga katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Pili, wakulima kuvamia maeneo ya misitu na pia kwenda kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya mapito ya wanyama (shoroba).
Vilevile tuna changamoto kubwa sana ambayo inasababisha kutokupunguza tatizo hili kubwa ambalo linatupata sisi kutokana na kwamba tunao Askari wa Wanyamapori ambao wako chini ya Halmashauri. Sasa tunaweza kuona kabisa Halmashauri zetu hazina bajeti kubwa ambayo inaweza kutatua changamoto kubwa ama ika-facilitate kwa asilimia 100 Askari hawa wa Wanyamapori kwenda kutatua hizi changamoto kubwa za watu kuvamiwa na mashamba yao. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Askari wasiozidi tisa katika wilaya yenye kata 39 na vijiji 57, lakini askari hawa tisa wanaokwenda field ni saba tu. Kwa hiyo, utagundua tuna vijiji 157 lakini tuna askari saba; na kwa siku kuna kero ambayo wanatoa taarifa vijiji 15 mpaka 20 ambayo vinahitaji msaada wa kwenda kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Askari wa Wanyamapori naona kuna tatizo la kimfumo kwamba Askari wa Wanyamapori wako chini ya Halmashauri; na tunajua kabisa Halmashauri zetu hazina uwezo wa kutosha.
Kwa hiyo, nashauri Askari wa Wanyamapori hawa wawe chini ya Wizara kwa sababu tunakumbuka na tunafahamu mwanzo walipokuwa wako chini ya Wizara, maana yake ni kwamba walikuwa wanapata magari ya kutosha, walikuwa wana silaha za kutosha, lakini pia tulikuwa na askari wa kutosha. Kwa sasa, kwa sababu wako chini ya Halmashauri, maana yake bajeti yao ni ndogo. Hakuna Halmashauri inaweza kutenga fedha kwa ajili ya Askari hao wa Wanyamapori. Tuna tatizo kubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwa mfano kwenye Wilaya yetu ya Tunduru, kitengo hiki cha Askari wa Wanyamapori wana silaha tisa, lakini silaha hizi ni za kizamani kweli kweli, maana yake zina zaidi ya miaka 40. Kwa hiyo, utakuta mara nyingine wakienda nazo porini zinakataa hata kufanya kazi.
Kwa hiyo, ndiyo maana nashauri hawa Askari wa Wanyamapori wawe chini ya Wizara kwa sababu, Wizara ina Askari ambao wana silaha za kisasa kama vile TAWA na Ngorongoro pamoja na TANAPA. Pia utaona, pamoja na silaha hizi ambazo ni kuukuu, zina zaidi ya miaka 40 bado pia hata risasi zake pia zina bei ghali. Kwa maana ya risasi moja inanunuliwa kwa shilingi 23,000 mpaka shilingi 25,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wale wa TAWA wao wana silaha za kisasa, lakini pia risasi moja inauzwa kwa bei rahisi sana, shilingi 3,000. Kwa hiyo, Askari wa Wanyamapori wakiunganishwa na TAWA tunakwenda kuondoa hili tatizo kubwa ambalo linatukabili kwenye wilaya yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kushauri, kama wilaya yetu ni mahususi kwa kilimo, naomba sana, hawa wafugaji ambao wanaingia, basi wafuate utaratibu ambao unawekwa na Serikali. Kwa mfano, Halmashauri yetu imetenga vitalu vinavyozidi 200, lakini cha ajabu hawa wafugaji wakiingia na ng’ombe hawaendi kufuga kwenye vile vitalu na badala yake wanakwenda kufuga kwenye hifadhi za wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ndiyo tatizo ambalo linasababisha kupata shida kubwa ya tembo kuwasumbua wananchi pamoja na kuwaua kwa sababu, wanapokwenda kufuga kwenye hifadhi zetu wale ng’ombe wanakuwa na harufu za dawa ambazo zinawakinga wao wasishambuliwe na wadudu. Kwa hiyo, ile harufu inawafanya wanyama hawa wakali kutoka nje ya hifadhi na badala yake kwenda kwenye maeneo ya binadamu. Sasa hili ni tatizo kubwa mno. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri, jambo la kwanza, kuwe na sheria ambayo inaweza ikawa kali kwa sababu tunaamini kabisa Watanzania imeshafika stage kwamba tukiwa na sheria laini, sheria nyepesi, hatutekelezi hiyo sheria. Kwa hiyo, mimi ningeomba kuwe na sheria ngumu… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja mkono.(Makofi)